Siha. Aliyekuwa mbunge wa Siha, Dk Godwin Mollel amewaomba msamaha wanachama wa Chadema kwa uamuzi wake wa kujivua ubunge na kujiunga na CCM.
Dk Mollel aliyetangaza uamuzi wa kujivua ubunge Desemba 14,2017 na kukabidhiwa kadi ya CCM Desemba 15,2017 amesema upepo wa kisiasa umebadilika na safari aliyoianzisha ni ya kusafisha upinzani kanda ya kaskazini.
Amesema hayo wakati wa kukabidhiwa kadi za CCM madiwani wawili waliojiuzulu nyadhifa zao na kuhama Chadema hivi karibuni, ambao ni wa Donyomurwak, Lwite Ndosi na wa Gararagua aliyekuwa pia mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Siha, Zakaria Lukumay.
Dk Mollel alisema jana Alhamisi Desemba 28,2017 kuwa amelitazama goli na ndiko alikokwenda ili kuweza kufunga.
“Natambua kuna watu walipoteza muda mwingi, walitumia fedha zao kunichangia na wengine walimwaga damu ili niweze kuwa mbunge lakini hivi majuzi nilijivua ubunge hatua ambayo iliwaumiza wengi. Niombe mnisamehe kwa kuwa nilishindwa kuwafuata siku ile nikihama kwa kuwa nilijua mngeweza kunipiga au kusababisha sintofahamu kubwa,” amesema Dk Mollel.
Amesema uamuzi wenye tija siku zote lazima ulete machungu.
Dk Mollel amesema ameingia kwenye vita kuhakikisha anayafikia malengo ya kuwaletea wananchi wa Siha maendeleo waliyoyatarajia kwa kipindi kirefu.
“Niwahakikishie wananchi wa Siha kwamba hamtajuta mimi kuhama chama, kwa kuwa niliisoma ramani yote ya Siha na kuelewa maendeleo yaliko, hivyo sijawaaibisha, niungeni mkono sasa na ninaahidi sitawaangusha,” amesema.
Pia, ametaka viongozi wa CCM kutambua kuwa wana kazi kubwa ya kuhakikisha walio nje ya chama hicho wanavutiwa na matendo ya chama na si kukatishwa tamaa.
Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Jonathan Mabihya amesema, “Kuna watu wanawatisha watu kuwa wakiondoka na kuja CCM hawatapata nafasi, tunawakaribisha kwa kuwa nafasi ziko wazi na wakihitaji kugombea watapata nafasi.”
Mabihya amesema CCM imeongeza idadi ya wapambanaji ambao wameamua wenyewe kuungana na timu ya maendeleo.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi amesema milango iko wazi kwa anayetaka kujiunga na chama hicho.
“Wanaorudi CCM wanarudi nyumbani, ninaomba Watanzania waelewe kuwa hakuna biashara ya binadamu na CCM hatuwezi kufanya biashara hiyo,” amesema.
Ndosi aliyekuwa diwani wa Donyomurwak ametaka maneno yanayoendelea kuhusu kuhama kwake Chadema yaishe, kwa kuwa haitaji mashindano ya maneno bali kufanya kazi ili kuyafikia maendeleo.
Comments
Post a Comment