Dar es Salaam. Zikiwa zimebaki siku mbili kabla ya kuuanga mwaka 2017, mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu ametoa waraka akilaani ukiukwaji wa haki za binadamu na kuminywa kwa uhuru wa kutoa mawazo.
Waraka huo alioutoa jana Alhamisi Desemba 28,2017 akiwa katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya anakopatiwa matibabu tangu Septemba 7,2017 aliposhambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi kwenye makazi yake Area D mjini Dodoma.
Lissu pia amezungumzia tukio la kutoweka mwandishi wa habari wa kujitegemea wa kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), Azory Gwanda ambaye leo ni siku ya 39 tangu alipotoweka akiwa wilayani Kibiti mkoani Pwani anakofanyia kazi zake.
“Watanzania ambao wamekuwa wakitumia uhuru wao wa maoni kutoa mawazo wamekuwa wakikamatwa na kushtakiwa mahakamani... mwanachama wa Chadema, Ben Saanane na mwandishi wa Mwananchi (Azory Gwanda) wametoweka na hawajulikani walipo. Hakuna uchunguzi au taarifa za kutoweka kwao,” amesema.
Lissu ambaye pia ni mwanasheria wa Chadema amesema vyombo vya habari vimekuwa katika wakati mgumu baada ya kukutana na mkono wa sheria, ikiwamo kufungiwa pale vinapoandika habari zinazotafsiriwa kuwa ni za kichochezi au uongo.
Kupitia waraka huo alioupa jina ‘Barua kutoka kitanda cha Hospitali ya Nairobi’ amezungumzia pia mambo yaliyojitokeza na yanayoendelea katika kipindi cha miaka miwili ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Waraka huo ameutoa siku tatu baada ya kusimama kwa mara ya kwanza tangu Septemba 7,2017 aliposhambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi.
Amesema kumekuwa na ukiukwaji wa haki za binadamu na utawala bora, huku viongozi wa upinzani na wanaharakati wakikamatwa na kuwekwa mahabusu.
Lissu amesema kutokana na watawala kuwashughulikia wanaowakosoa, uhuru wa kutoa maoni umeminya na mijadala haipo.
“Mikutano ya kisiasa imezuiwa na polisi, viongozi wanakamatwa, wabunge nikiwemo mimi (Lissu) tumekamatwa mara nyingi kwa sababu zinazohusu majukumu yetu ya kazi,” amesema.
Amesema, ‘’Hakuna njia rahisi kufikia uhuru sehemu yoyote na wengi wetu tutapitia bonde la kivuli cha kifo kabla ya kufikia mlima wa matamanio yetu.”
Pia, amevilaumu vyombo vya dola akisema tangu Septemba 7,2017 aliponusurika kuuawa akiwa eneo lenye ulinzi mpaka sasa hakuna mtuhumiwa hata mmoja anayeshikiliwa kuhusika na tukio hilo.
Kuhusu onyo la Serikali kwa viongozi wa dini kutojihusisha na masuala ya kisiasa lililotolewa jana Alhamisi Desemba 28,2017 na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Lissu amesema ni mwendelezo wa kuwazuia watu wasitumie uhuru wao kuzungumza na kukosoa.
Comments
Post a Comment