Pamoja na hali hiyo, hali ilikuwa tofauti katika mataifa matatu ya bara hili. Wakati Kenya ikionyesha ukomavu wa demokrasia baada ya Mahakama kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa rais kutokana na kesi iliyofunguliwa na upinzani, Liberia na Ghana zilishuhudia upinzani ukishinda katika uchaguzi mkuu.
Kwingineko, katika nchi kama Tanzania, Uganda, Rwanda na Congo DRC, wapinzani wameendeleza kilio cha kudai demokrasia. Zimbabwe nako kulikuwa na tukio la aina yake, jeshi lilimlazimisha kiongozi wa muda mrefu, Robert Mugabe kung’atuka katika hatua iliyoonekana ni ya kudhibiti mgogoro wa ndani ya chama tawala cha Zanu-PF.
DRC mkwamo wa kisiasa umeendelea baada ya Rais Joseph Kabila kukataa kuitisha uchaguzi kama ilivyokubaliwa, huku Rwanda ikiendesha uchaguzi ulioonekana kuwa wa upande mmoja kutokana na mpinzani wa Rais Paul Kagame kuingia matatizoni na vyombo vya dola.
Hali iliendelea kuwa kama hiyo nchini Uganda ambako Rais Yoweri Museveni anaendeleza utawala wake wa zaidi ya miongo mitatu huku akituhumiwa kutumia mabavu.
Nchini Tanzania kilio ni kilekile. Vyama vya upinzani vimeshindwa kuendesha mikutano ambayo vinaielezea kuwa ni muhimu kwa uhai na chama kukua, huku baadhi ya viongozi wake wakikamatwa kwa tuhuma za uchochezi, kufanya fujo na uharibifu.
Lakini pia katika siku za karibuni kumekuwa na wimbi la viongozi hususan wabunge na madiwani kuhama vyama, na waathirika wakubwa wa hili vikiwa ni vyama vya upinzani hususan Chadema.
Chadema kimepoteza mbunge mmoja na zaidi ya dazeni moja ya madiwani. CUF imepoteza mbunge mmoja na huku ikiendelea kukabiliana na mgawanyiko wa ndani ya chama.
Katika hamahama hiyo, mbunge mmoja wa CCM, Lazaro Nyalandu aliyekuwa Singida Kaskazini, alijivua uanachama wa chama hicho na kujiunga na Chadema.
Ukimuondoa Nyalandu, wabunge na madiwani waliokuwa upinzani waliibua siasa za aina yake kutokana na karibu wote kueleza kuwa sababu ya kujivua nyadhifa zao ni kumuunga mkono Rais John Magufuli katika jitihada zake za kupambana na ufisadi na kurekebisha uchumi.
Mwaka huu ulifanyika uchaguzi wa marudio katika kata 43 na ushindi mkubwa ulikwenda CCM iliyotwaa kata zote kasoro moja iliyokwenda Chadema. Chama hicho kikuu cha upinzani kilisusia uchaguzi huo katika baadhi ya kata ikidai mawakala wake walizuiwa kuingia vituoni na wagombea kukamatwa.
Viongozi wa CUF waliendelea kupambana mahakamani. Chama hicho kimekuwa katika mgogoro tangu Profesa Ibrahim Lipumba, mwenyekiti wake anayetambuliwa na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kutangaza kurejea madarakani mwaka mmoja tangu ajiuzulu.
Profesa Lipumba aliwavua uanachama wabunge wanane wa viti maalumu na madiwani wawili ambao ni watiifu kwa kundi la katibu mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad na nafasi zao kuchukuliwa na wanachama wanaomuunga mkono.
Wakizungumzia hali ya migogoro ya kisiasa Afrika, wachambuzi wa masuala ya siasa walitoa sababu kadhaa, Profesa Benson Bana wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) alisema umefikia wakati wa vyama vya upinzani barani Afrika kurudi kwenye majukumu yake ya awali na kuacha siasa za harakati.
“Kama kweli vinataka kushika dola ni lazima vijisahihishe. Viandae viongozi na kujenga ushawishi kwa wananchi ili ukifika uchaguzi viweze kuchaguliwa kwa wingi na kushinda,” alisema Profesa Bana.
“Kubwa visome CCM inafanya nini na wao wajipangaje kuwashawishi wananchi wawaunge mkono. Haya yote yatawezekana ikiwa wataachana na uanaharakati.”
Alisema havipaswi kutegemea wanachama wanaohamia na kuwapa nafasi ya kugombea papo kwa hapo kama ambavyo vimekuwa vikifanya.
“Wasisahau majukumu yao ya msingi ikiwamo kuandaa viongozi kwa hiyo watumie muda mwingi kuwaandaa kama kweli wana lengo la kuleta upinzani,” alisema.
Kwa mtazamo wake, Profesa wa Sayansi ya Siasa Chuo Kikuu cha Ruaha mkoani Iringa, Gaudence Mpangala alisema nchi nyingi za Afrika zinarudi kwenye mfumo wa chama kimoja ulioshindikana awali.
“Vyama vya upinzani havitakiwi vife, kwa sababu mfumo wa chama kimoja ulitushinda huko nyuma. Ulitufanya tuingie kwenye udikteta na matokeo yake nchi nyingi za Afrika zikaishia kuwa maskini. Ijapokuwa madikteta wa nchi za Asia walizitajirisha nchi zao,” alisema.
Profesa Mpangala ambaye hivi karibuni alitoa andiko lake kuhusu demokrasia kwa nchi za Maziwa Makuu alisema awali mfumo wa vyama vingi uliingia kwa matumaini makubwa lakini umeshindwa kwa sababu vyama tawala vimejipa uwanja mkubwa.
“Kwanza chaguzi zinazofanyika haziko huru, halafu kumekuwa na migogoro mingi. Mfumo wenyewe ni sawa na wa chama kimoja kilicho ndani ya vyama vingi, kina nguvu kuliko vyama vingine,” alisema.
Profesa Mpangala alisema hakuna njia nyingine inayoweza kuvisaidia vyama wakati huu zaidi ya kuwa na umoja.
Alitoa mfano wa Tanzania akisema ina vyama 20 vya upinzani idadi ambayo ni kubwa ikilinganishwa na umuhimu wa uwepo wake.
“Kama wangeungana wangekuwa na nguvu, vyama hivi vina kazi gani wakati vingine havisikiki kabisa? Wakati huu mambo yameshaharibika ni bora wangeungana kama kweli wana nia ya dhati ya kuleta upinzani,” alisema Profesa Mpangala.
Alielezea pia umuhimu wa kuwapo kwa Katiba Mpya inayoendana na mfumo wa vyama vingi na kuwa na sheria nzuri zinazosimamia mfumo huo akisema hiyo itasaidia upinzani kuimarika.
“Wakati tunaanzisha vyama vingi nilikuwapo kwenye tume iliyokusanya maoni, moja ya mambo tuliyoshauri ilikuwa ni kuwapo Katiba Mpya. Suala hili halijaanza leo,” alisema.
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Emmanuel Mallya alisema demokrasia ya vyama vingi barani Afrika bado inakua.
“Demokrasia ni kama mtoto. Anazaliwa, anakua, anaugua anatibiwa. Kwa Afrika bado demokrasia ni changa, tofauti na nchi za Ulaya na Marekani ambako ilianza muda mrefu,” alisema Dk Mallya.
Hata hivyo, alisema demokrasia si lazima iwe na vyama vingi, bali hata kukiwa na chama kimoja chenye mfumo shirikishi nayo pia ni demokrasia.
Mhadhiri mwingine wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI), Dk Jimson Sanga alisema jambo la kwanza vyama hivyo havipaswi kukata tamaa kwenye safari yao licha ya kukutana na vizingiti vinavyowarudisha nyuma.
Dk Sanga alisema kwa umoja wao, vyama vya Tanzania, vinapaswa kukaa mezani na Rais John Magufuli kuzungumzia hatima yao kwa sababu kama sera na katiba haivipi nafasi vyama hivyo, vitaendelea kusota.
Upinzani unaonekana kuwa katika hali mbaya zaidi hasa kutokana na jinsi unavyovutana na Rais Yoweri Museveni ambaye haonyeshi nia ya kuondoka madarakani siku za usoni.
Mpinzani wake wa karibu tangu mwaka 2001, ambaye zamani alikuwa daktari wake, Dk Kizza Besigye bado anapambana naye, amekuwa akikamatwa na Polisi mara kwa mara.
Dk Besigye ameshapambana na Museveni katika chaguzi za mwaka 2001, 2006, 2011 na mwaka 2016 bila mafanikio.
Hivi karibuni wabunge wa Uganda walipitisha mabadiliko ya Katiba ambayo sasa yanamruhusu Rais Museveni kuwania nafasi hiyo kwa muhula wa sita.
Mabadiliko hayo yalipitishwa baada ya siku tatu za majadiliano mazito na mivutano na hatimaye kuondoa ukomo wa umri wa miaka 75 kwa mgombea urais.
Rais Kagame aliyeingia madarakani kwa kuchaguliwa mwaka 2000, licha ya kushinda chaguzi zote kwa kishindo, wapinzani wake akiwamo Victoire Ingabire wamekuwa wakikumbana na misukosuko kadhaa.
Ingabire alifungwa jela baada ya uchaguzi wa mwaka 2010. Mpinzani mwingine, Diane Rwigara aliyegombea urais katika uchaguzi wa mwaka huu alizuiwa na Tume ya Uchaguzi akidaiwa kughushi saini katika fomu za uchaguzi na kwamba alipeleka saini 572 wakati zilitakiwa 600. Hata hivyo, mwenyewe alisema alikusanya saini 912.
Wagombea wengine wawili pia waliondolewa kwenye kinyang’anyiro hicho ambacho Kagame alishinda kwa asilimia 98.
Baadaye, Diane alikamatwa na polisi kwa madai ya kukwepa kodi na kutishia usalama wa Taifa akishtakiwa pamoja na mama yake na dada yake.
Hali pia si shwari Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) baada ya Rais Joseph kabila kuahirisha uchaguzi mkuu uliokuwa ufanyike mwaka huu, huku akidaiwa kufanya mbinu za kung’ang’ania madarakani.
Kabila ni Rais wa tatu wa nchi hiyo ambayo haijawahi kukabidhiana madaraka kwa njia ya sanduku la kura.
Aliingia madarakani mwaka 2001 baada ya kifo cha baba yake Laurent Kabila aliyempindua aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Mobutu Sese Seko mwaka 1997.
Awali, uchaguzi mkuu ulitakiwa ufanyike mwaka 2017, lakini uliahirishwa kwa kile kilichoelezwa kuwa Tume ya Uchaguzi imeshindwa kuuandaa.
Hata hivyo, hivi karibuni tume hiyo imetangaza kuwa uchaguzi huo sasa kufanyika Desemba 2018. Hata hivyo, tangazo hilo limepingwa na upinzani ukimtaka Kabila aondoke madarakani.
Mpinzani wake wa karibu, Moise Katumbi ambaye ni gavana wa Jimbo la Katanga alijikuta matatizoni baada ya kutangaza nia yake ya kugombea urais.
Comments
Post a Comment