Skip to main content

Featured

Maombolezo: Hii ndiyo Hali Ilivyo Tanzania Bendera Yapepea Nusu Mringoti

Agizo la Rais John Magufuli la Bendera ya Taifa kupepea kwa nusu mlingoti kwa siku tatu kuanzia leo Septemba 22 kufuatia ajali ya kivuko cha MV Nyerere iliyotokea mkoani Mwanza limetekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Baada ya kupandisha mishahara, Dk Shein sasa ataka juhudi 2018


Zanzibar. Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema kuwa juhudi za kuimarisha ukusanyaji wa mapato zimeiwezesha Serikali kutekeleza ahadi aliyoitoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ya kupandisha mishahara ya kima cha chini kwa asilimia mia.
Alisema mishahara hiyo ilipandishwa kutoka Sh150,000 mpaka Sh300,00 kwa mwezi kwa watumishi wa Serikali.
Dk. Shein alisema hayo jana katika hotuba yake ya kuukaribisha Mwaka Mpya aliyoitoa kupitia vyombo vya habari, Ikulu mjini Zanzibar.
Alisisitiza kuwa Serikali yake imeweza kuongeza pensheni kwa wastaafu na kuendelea kutoa fedha za Pensheni ya Jamii kwa wazee wote wanaostahiki.
Alisema tangu Aprili, 2017 walengwa wa nyongeza hizo walikuwa wakifaidika na neema hiyo.
Dk Shein alisema katika mwaka 2017 Serikali imezidi kuimarisha masilahi ya wafanyakazi wa sekta binafsi wanaopata mshahara wa kima cha chini.
Pia, alisema ni faraja kuona waajiri wengi katika sekta hiyo wameshaitikia wito, licha ya kuwapo baadhi waliotaka kurejesha nyuma juhudi hizo za Serikali.
Kuhusu uchumi wa Zanzibar, alisema unaendelea kuimarika na katika robo mwaka ya kwanza ya mwaka 2017 (Januari-Machi), kasi ya ukuaji ilifikia asilimia 6.3 ikilinganishwa na kasi ya ukuaji wa asilimia 5.2 kwa kipindi kama hicho cha robo mwaka ya kwanza ya mwaka 2016.
Katika kipindi cha robo mwaka ya pili (Aprili-Juni) kwa mwaka 2017, alisema ukuaji wa uchumi nao uliimarika na kufikia asilimia 8.2.
Dk Shein alieleza kuwa ni jukumu la kila mmoja katika mwaka huu wa 2018 kuongeza juhudi ili kuhakikisha malengo ya maendeleo yanaendelea kutekelezwa vizuri.
Alitoa pongezi kwa wananchi wa mikoa yote ya Zanzibar kwa juhudi zao za maendeleo yaliyopatikana katika sekta mbalimbali.
Alisema lengo kutekeleza Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2015-2020, Dira ya Maendeleo ya 2020, Mkuza 111 (Mpango wa Kitaifa wa Kupunguza Umaskini Zanzibar) na Malengo ya Maendeleo Endelevu yaliyowekwa na Umoja wa Mataifa (UN).
Pia, Dk Shein alisema Serikali imepiga hatua kubwa katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali katika sekta ya afya na hivi sasa juhudi kubwa zimeelekezwa katika kuimarisha huduma ikiwamo upatikanaji wa dawa na vifaa vya matibabu katika hospitali na vituo vya afya.
Alisema katika mwaka wa fedha uliomalizika, Serikali imetenga Sh 7 bilioni kwa ununuzi wa dawa na vifaatiba, sawa na ongezeko la asilimia 42.9 ikilinganishwa na kiwango kilichotengwa kwa mwaka 2016/17.
Elimu na kazi
Kwa upande wa sekta ya elimu, Dk Shein alisema Serikali imeshaanza ujenzi wa mradi wa shule tisa za ghorofa katika sehemu mbalimbali za Unguja na Pemba.
Alisema ili kuimarisha mazingira ya kusomea kwa wanafunzi hapa nchini, ujenzi wa shule hizo utagharimu Sh24.4 bilioni ambazo ni mkopo kutoka Mfuko wa OPEC ili kufanikisha ujenzi huo ifikapoJanuari, 2019.
Dk Shein alieleza kuwa katika sherehe za elimu bila ya malipo zilizofanyika Septemba 23, 2017 alitangaza rasmi kuondoa michango katika elimu ya sekondari kuanzia Julai, 2018.
Hatua hiyo inalenga kuendeleza utoaji elimu bure kwa shule zote za msingi na sekondari.
Dk Shein alisema taarifa rasmi kuhusu tatizo la kupoteza fedha za mishahara kwa wafanyakazi wanaochukua likizo bila ya malipo, wanaotoroka kazini na wanaolipwa kinyume na utaratibu (hewa), itatolewa na Serikali hivi karibuni.
Gesi na mafuta
Alisema katika mwaka 2018, Serikali inaendeleza utafiti wa mafuta na gesi kwa kutegemea taarifa itakayotolewa na wataalamu na kutoa wito kwa wananchi kuwa watulivu.
Alisema Serikali itatoa taarifa rasmi ya matokeo ya utafiti huo unaofanywa kwa masilahi ya Zanzibar.
Aliwataka wananchi kutosikiliza maneno ya mitaani na kwenye mitandao wakati Serikali yao ipo.
Pia, aliwataka kuendelea kuunga mkono juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika kuiendeleza sekta ya mafuta na gesi asilia.
Kilimo cha karafuu
Pamoja na hayo, Dk Shein alisema kuwa Mpango Maalum wa Kulifufua Zao la Karafuu ulioanzishwa baada ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba kuingia madarakani mwaka 2010 kwa kupanda mikarafuu mipya, umeanza kutoa matokeo mazuri.
Alisema Desemba 20, 2017 wakulima wa karafuu walikuwa wameshauza karafuu ZSTC zenye thamani ya Sh108.8 bilioni.
Kiwango hicho cha fedha kimekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha mzunguko wa fedha na kukuza sekta nyingine za kiuchumi.
Kuuawa kwa wanajeshi DRC
Dk Shein alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wote wanaendelea kuwakumbuka wakati wote wanajeshi 15 wa Jeshi la Wanachi wa Tanzania (JWTZ) waliofariki huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambako walikuwa katika shughuli za kusimamia amani chini ya uongozi wa Umoja wa Mataifa.
Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kupanga na kutekeleza mikakati mbalimbali ya kulinda na kudumisha amani nchini, Barani Afrika na duniani kote kwa jumla.
Malengo
Dk Shein pia, aliwasisitiza wananchi wakati wakiupokea Mwaka Mpya wa 2018, kila mmoja aweke dhamira ya dhati ya kufanya kazi kwa bidii na maarifa na kuongeza jitihada za kuongeza kipato na kupambana na umasikini.
Aliwataka wananchi kushirikiana na Serikali kwa lengo la kuimarisha utawala bora, kukuza uadilifu na uwajibikaji pamoja na kusimama imara katika mapambano dhidi ya rushwa, uhujumu uchumi na dawa za kulevya.
Sambamba na hayo, Dk Shein aliwataka wananchi kuanza kusherehekea mwaka 2018 kwa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Sherehe za miaka 54 ya Mapinduzi Zanzibar Januari 12 pamoja na kushiriki katika ufunguzi na uwekaji wa mawe ya msingi ya miradi mbalimbali ya maendeleo.

Comments