Skip to main content

Featured

Maombolezo: Hii ndiyo Hali Ilivyo Tanzania Bendera Yapepea Nusu Mringoti

Agizo la Rais John Magufuli la Bendera ya Taifa kupepea kwa nusu mlingoti kwa siku tatu kuanzia leo Septemba 22 kufuatia ajali ya kivuko cha MV Nyerere iliyotokea mkoani Mwanza limetekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Wanufaika Tasaf waomba kuongezewa ruzuku


Kaya masikini zinazopata ruzuku kupitia fedha za Tasaf awamu ya tatu zimeomba kuongezewa ruzuku hiyo ili waweze kupanua na kuboresha shughuli zao za ujasiriamali  ambazo zimewatoa kwenye masikini uliokithiri.
Wakizungumza  leo Januari 28 wakati wa kupokea ruzuku baadhi ya wananchi wa kaya zilizonufaika na fedha hizo kutoka kata ya Mbuyuni na Kauzeni Manispaa ya Morogoro wamesema  pamoja na kwamba fedha hizo zimewakwamua kwenye umasikini lakini bado wanatamani kuongeza shughuli zao za ujasiliamali.
Mmoja wa wanakaya waliopata fedha hizo za ruzuku Anatalia Thomas ameiomba Tasaf imuongeze ruzuku kwani kiasi anachopata sasa hivi ni Sh. 40,000 na kwamba anatamani kufuga kuku, mbuzi na kufungua mgahawa ambapo anahitaji kuwa na mtaji zaidi ya kiasi hicho anachopewa.
Anatalia amesema kuwa ufugaji anaoufanya sasa hivi ni mdogo hivyo anashindwa kupata faida itakayoboresha mazingira yake ya ufugaji.
“Sina hata banda kufugia, bata wangu wanazurura tu mtaani watu wanawaiba wengine wanawapiga na kuwaua usiku nalala chumba kimoja, kwa kweli ningeongezewa ruzuku ningeweza kujenga banda,” amesema Anatalia.
Hata hivyo amesema kuwa fedha hizo zimemsaidia kwa  kubadilisha maisha yake kwani kwa sasa anaweza kupata milo mitatu, ameweza kusomesha wajukuu zake wawili kati ya 12 anaoishi nao na pia aliweza kujiunga na mfuko wa bima ya afya ya jamii CHF.
Mnufaika mwingine wa ruzuku hizo Karista Laurence kutoka kata ya Kauzeni alisema kuwa kama Tasaf ingemuongezea ruzuku angeongeza ukubwa wa shamba lake na kulima mazao mchanganyiko.
Karista amesema kuwa kwa sasa anapata ruzuku ya Sh. 32,000 na kwamba kutokana na kilimo cha mbogamboga anachofanya ameweza kusomesha watoto wake wawili na kujenga nyumba yake ya vyumba viwili.
Hata hivyo yapo malalamiko kutoka kwa baadhi ya kaya zilizoondolewa kwenye ruzuku hizo na kudai kuwa wameonewa kwa vile wana nyumba kubwa na watoto wanaojitegemea.
Mmoja wa wanakaya hao walioondolewa kwenye ruzuku hiyo kutoka kata ya Mbuyuni Halima Said alisema kuwa nyumba anayoishi ni ya urithi hivyo ndugu zake wamekuwa wakichukua fedha zote za kodi ya nyumba.
Akijibu malalamiko hayo Ofisa  mwezeshaji wa Tasaf kata ya Mbuyuni Joyce Mugambe amesema kaya hizo ziliondolewa kwenye ruzuku hizo baada ya kubainika kuwa wana uwezo wa kujikimu kimaisha kwa kuwa wana nyumba zilizopangishwa.
Mugambe amesema kuwa utaratibu wa kuziondoa kaya hizo ulifanywa kupitia mikutano ya mtaa kwa kuwashirikisha wenyeviti wa mitaa ambapo miongoni mwa vigezo vya kuziondoa kaya hizo ni kuwa na nyumba kubwa yenye wapangaji.

Comments

Popular Posts