Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Jumuiya ya Benki Tanzania (TBA), Dk Charles Kimei ameonya kuwa umakini unahitajika katika mamlaka za Serikali kwa kuwa kutoa siri za mteja kutoka benki na kuziweka hadharani kunaweza kuua sekta hiyo.
Kimei, ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa CRDB alisema hayo wakati akitoa mada katika kongamano la maendeleo ya viwanda lililofanyika katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Kigamboni jijini hapa jana .
Onyo la Kimei limekuja siku tatu tangu Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), iweke hadharani taarifa ya akaunti ya Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF) iliyopo katika Benki ya NBC kuwa ina zaidi ya Sh8 bilioni.
Februari 19, TRA ilitoa taarifa ya matokeo ya uchunguzi iliyoufanya baada ya kiongozi wa kanisa hilo, Askofu Zachary Kakobe kutoa kauli katika mkesha wa Krismasi mwishoni mwa mwaka jana kwamba ana fedha nyingi kuliko Serikali.
Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere akitoa taarifa ya uchunguzi huo, alisema Askofu Kakobe hana akaunti wala fedha katika taasisi yoyote ya kifedha nchini zaidi ya kuwa mmoja kati ya wasimamizi wakuu wa akaunti ya kanisa analoliongoza.
Kichere alikwenda mbali zaidi na kusema akaunti za kanisa hilo zipo NBC zikiwa na zaidi ya Sh8 bilioni, ambazo ni fedha za sadaka, zaka na changizo zinazotolewa na waumini. Hata hivyo suala hilo halijakubalika miongoni mwa benki.
Dk Kimei alisema miongoni mwa masuala muhimu katika biashara ya benki ni usiri wa taarifa za mteja na mamlaka za Serikali katika kutekeleza majukumu yake taarifa za benki hazipaswi kuwa kitu cha kwanza bali zitolewe iwapo Mahakama itahitaji.
Jambo hilo ambalo limezua mjadala miongoni mwa wachumi na wataalamu wa sekta za fedha lilizungumzwa pia na Mkurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Godfrey Simbeye katika kongamano hilo.
Simbeye alisema ni muhimu kwa mamlaka husika kupima matokeo ya jambo wanalotaka kulifanya kabla ya kuchukua hatua.
“Jambo la kutoa taarifa za mteja ni baya kwa jicho la kiuwekezaji, wafanyabiashara wakubwa hawatataka kuja nchini kuwekeza kwa kuhofia kutokuwa na usiri katika mambo yao ya kifedha,” alisema Simbeye.
Alisema hali kama hiyo inaongeza hatari na imani hasi ya wawekezaji juu ya mazingira ya kufanya biashara nchini.
Nayo benki ya NBC, ambako kanisa hilo ndio huweka fedha zake imetoa kauli kuhusu hatua ya TRA kuweka wazi taarifa za kifedha za Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), huku wadau wa sekta ya benki wakiendelea kulaani jambo hilo.
NBC baada ya kuulizwa na Mwananchi Jumanne wiki hii kuhusu namna ilivyotimiza jukumu lake la kulinda taarifa za mteja kama sheria na utaratibu unavyotaka, jana ilijibu kwa njia ya barua pepe ikisema mambo yote yalifuata utaratibu na matakwa ya kisheria.
“Kulinda taarifa za mteja ni miongoni mwa vipaumbele vya benki yetu na tunafanya hivyo kwa kufuata sheria, kanuni na utaratibu wa nchi, katika suala la Kakobe taratibu zote zilifuatwa kwa mujibu wa sheria na NBC haina utaratibu wa kutoa taarifa za mteja bila kumhusisha,” ilieleza taarifa ya benki hiyo.
Mwanzoni mwa wiki, Kichere aliliambia Mwananchi kuwa TRA walitoa taarifa kwa kuongozwa na busara kwa kuwa kabla ya kufanya uchunguzi waliutaarifu umma hivyo hata baada ya uchunguzi waliona ni vyema kuweka wazi matokeo ya kile walichokichunguza.
Katika kongamano la jana, wadau wa sekta ya fedha walisema ili taasisi za fedha ziweze kushiriki kikamilifu katika sekta ya viwanda nchini, Serikali imetakiwa kupunguza kukopa nchini, kutoa elimu ya benki kwa wananchi na kuanzisha chombo maalumu cha ukopeshaji wa mitaji kwaajili ya viwanda.
Akifungua mkutano huo, naibu waziri wa Viwanda na Biashara, Mhandisi Stella Manyanya alisema taasisi za fedha zinapaswa kuisaidia Serikali kufikia adhima yake ya kuwa na nchi ya uchumi wa viwanda kwa kuwezesha uwekezaji katika eneo hilo.
“Kama taasisi za fedha zitaelekeza nguvu katika kuendeleza viwanda lengo la Serikali yetu litafikiwa, Watanzania wengi wanathubutu, lakini wanapata changamoto ya mitaji na elimu ya biashara,” alisema Mhandisi Manyanya.
Akichangia mada hiyo, Kimei alisema asilimia 70 ya fedha zilizopo katika mzunguko hapa nchini zipo katika benki za biashara na asilimia 30 katika taasisi za mitaji kama mifuko ya hifadhi za jamii.
“Kuna fursa ya kuwekeza na kupata faida kubwa katika sekta ya viwanda sasa, lakini benki za kibiashara hazina uwezo wa kutoa mikopo ya muda mrefu kwakuwa fedha zake nyingi ni amana za watu huku amana za mtu mrefu zikiwa asilimia 40 tu,” alisema Dk Kimei.
Alisema mifuko ya jamii ina uwezo wa kutoa mikopo ya muda mrefu lakini hilo si jukumu lake ni si salama kwao kwa sababu hawana uwezo mkubwa wa kujua taarifa za mkopaji na kukokotoa hatari na faida za mikopo yao.
Alisema wanasiasa na viongozi wa dini wanatakiwa kusaidia kuishauri jamii kuhusu umuhimu wa kuweka akiba katika benki kwa ajili ya kukuza uchumi wa nchi na kinga yao wakati wa dharura.
Simbeye alisema ni muhimu kuwa na mfuko maalumu kwaajili ya viwanda kwasababu benki za biashara zinalenga zaidi faida kuliko huduma ndiyo maana mikopo yao mingi ni kwa wafanyabiashara.
“Mwaka jana fedha ambazo zilikopeshwa kwa sekta binafsi ni trilioni 16.3, asilimia 9.8 tu ndo zimekwenda kwenye viwanda ... kujenga uchumi wa viwanda ni mradi wa kitaifa kama ilivyo SGR hivyo ni muhimu serikali ikatenga fedha mahususi kwaajili yake,” alisema Simbeye.
Comments
Post a Comment