Matukio ya utekaji, mauaji, ukiukwaji wa haki za binadamu na utawala bora yamemuibua mbunge wa viti maalum (Chadema), Upendo Peneza akisema viongozi waliopo madarani na wale wa dini wanapaswa kusimamia haki na kukemea pale inapobidi.
Pia, Peneza ameitaka Serikali kuurejesha mchakato wa Katiba uliotumia mabilioni ya fedha ili uhitimishwe na kujibu kiu ya Watanzania wengi ya kupata Katiba mpya inayoendana na mazingira ya wakati huu.
Mbunge huyo ameyasema hayo katika mahojiano na MCL Digital Februari 21, 2018 baada ya kutembelea ofisi za gazeti la Mwananchi zilizopo Tabata- Relini jijini Dar es Salaam.
Amesema viongozi waliopewa dhamana wana wajibu mkubwa wa kulinda na kudumisha amani kwa kukubali kukosolewa, viongozi wa kiroho kutokubali kuzuiwa kukemea pale inapobidi kufanya hivyo kwani ni moja ya wajibu wao.
“Kama nchi, viongozi tuliopewa dhamana lazima tukubali kukosolewa, mtu anayekosolewa avumilie...kukosolewa ni lazima labda lugha inayotumika iwe inayoheshimu utu wa mtu na kuheshimu mila na tamaduni zetu lakini tukubali kukosolewa,” amesema Peneza na kuongeza,
“Tukiheshimu misingi ya uwazi, uwajibikaji na kusimamia utawala bora, kila mmoja kutekeleza wajibu wake ipasavyo nchi itakuwa na amani. Vyombo vinavyopaswa kusimamia haki vifanye hivyo, Bunge litekeleze wajibu wake na Mahakama hivyo hivyo.”
Kuhusu viongozi wa dini na kukemea masuala kadhaa amesema “wanasiasa tunakuwa hatukumbuki, hawa hawa viongozi wa dini tunazunguka makanisani, misikitini kuomba watuchague, sasa hawa hawa waliotuweka kama viongozi wa kiroho kwa nini wasitukosoe? Kama wananchi wa kiroho wanaowaongoza kwa nini wasiwasemee walioshiriki kukuweka.”
Peneza ametolea mfano matukio ya mauaji ya mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline, mwenyekiti wa Chadema, mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo, Katibu wa Chadema, Kata ya Hananasif, Daniel John, kushambuliwa kwa risasi mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, kutekwa kwa mwandishi wa Mwananchi, Azory Gwanda ambaye mpaka leo ni siku ya 94 hajulikani alipo.
Katika mahojiano hayo, Peneza amesema matatukio na matatizo yanayojitokeza suluhisho ni kuwa na Katiba mpya ambayo itaweka mfumo madhubuti wa utawala kwa watawala na watawaliwa.
“Mchakato wa Katiba ulitumia mabilioni ya fedha lakini uliharibiwa na wachache ambao misimamo yao imekuwa inabadilika badilika. Tukiwa na Katiba bora Bunge litakuwa huru, litaweza kutekeleza majukumu yake vyema, Mahakama hivyo hivyo na hii Tume ya Uchaguzi nayo itakuwa huru kwa hiyo Katiba mpya haiepukiki,” amesema Peneza.
Comments
Post a Comment