Dar es Salaam. Hukumu ya Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ ya kutumikia kifungo cha miezi mitano jela, inaweza kuhamia vichwani mwa baadhi ya wabunge wanaokabiliwa na mashtaka mbalimbali.
Sugu amekuwa mbunge wa pili kuhukumiwa kifungo akitanguliwa na Mbunge wa Kilombero (Chadema), Peter Lijualikali.
Lijualikali na dereva wake, John Kibasa kwa walihukumiwa Januari 11, 2017 na Mahakama ya Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro kwenda jela miezi sita kwa kosa la kufanya vurugu wakati wa uchaguzi wa mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero na kushtakiwa kwa kuwashambulia polisi siku hiyo.
Hata hivyo, Machi 31, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilimuweka huru Lijualikali na dereva wake.
Jana, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema mpaka sasa wabunge 13 wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini wanakabiliwa na kesi katika mahakama mbalimbali nchini.
Aliwataja wabunge hao kuwa ni Godbless Lema (Arusha Mjini), Tundu Lissu (Singida Mashariki), Lijualikali, Susan Kiwanga (Mlimba) na Zubeda Sakuru wa viti maalumu.
Wengine ni Pascal Haonga (Mbozi), Halima Mdee (Kawe), Frank Mwakajoka (Tunduma), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini), Ester Bulaya (Bunda Mjini), Kunti Yusuph (Viti Maalumu), Cecil Mwambe (Ndanda) na Saed Kubenea wa Ubungo.
Lissu, ambaye pia ni rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) anayeendelea na matibabu katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Leuven, Ubelgiji anakabiliwa na kesi zaidi ya tatu za uchochezi.
Lema anakabiliwa na kesi ya uchochezi ambayo ilimfanya kuwekwa mahabusu kwa siku 121 baada ya ofisi ya mwendesha mashtaka wa Serikali kuweka zuio la dhamana huku Mdee akikabiliwa na kesi ya kutoa lugha ya uchochezi pia.
Wengine wenye kesi za uchochezi au kuikashfu Serikali au viongozi waliopo madarakani ni Haonga na Mwakajoka.
Mchungaji Msigwa anakabiliwa na kesi kadhaa ikiwamo ya hivi karibuni katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa akishtakiwa kwa kesi mbili.
Mbunge huyo ni mshtakiwa wa saba katika kesi hizo, moja anadaiwa kuchoma moto nyumba ya Mary Tesha aliyokuwa akiishi Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Alphonce Muyinga na ya pili, mbunge huyo na wenzake sita wanadaiwa kupanga njama ya kutenda uhalifu kinyume cha sheria.
Kwa upande wao, Lijualikali, Kiwanga na wanachama 34 wa Chadema mkoani Morogoro wanatuhumiwa kwa makosa manane likiwamo la kuchoma moto ofisi ya Kata Sofi iliyopo wilaya ya Malinyi.
Comments
Post a Comment