Lowassa alisema hayo jana akizungumzia kauli ya Mkapa aliyoitoa Machi 17 mjini Dodoma kuwa kuna janga katika elimu nchini na kushauri kuitishwa kwa mdahalo wa wazi utakaoshirikisha makundi yote ya jamii kwa ajili ya kujadili suala hilo.
Rais huyo mstaafu ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza wakati wa hafla ya kumuaga Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Idris Kikula.
“Ninaamini kabisa kwamba tuna crisis (janga) ninasoma katika magazeti, ninaletewa presentation (mawasilisho) kutoka sekta binafsi, walimu na private universities (vyuo vikuu binafsi). Napata pia minongo’no kutoka kwa vyuo vya umma kwamba kuna (crisis) kwenye elimu,” alisema.
Jana, Lowassa alitoa taarifa kwa vyombo vya habari akisema hiyo ilikuwa ajenda yake kuu katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Hata hivyo, CCM imejibu madai hayo ikisema hoja hiyo ilikuwa ya chama hicho tawala iliyotolewa na waziri mkuu huyo wa zamani akiwa mwanachama wake, lakini alizipeleka upinzani alipohamia huko.
Katika uchaguzi huo, Lowassa alikuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema akiungwa mkono na vyama vya CUF, NCCR-Mageuzi na NLD vilivyokuwa chini ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
“Nimefurahi kuwa Mzee Mkapa ameliibua suala hili kwani hiyo ilikuwa ajenda yangu ya kwanza tangu nikiwa ndani ya CCM na nje ya CCM,” alisema Lowassa.
Alisema katika ajenda hiyo, waliahidi kuitisha mjadala wa kitaifa juu ya elimu kuangalia wapi nchi imekwama na nini kifanyike.
“Na zaidi tuliahidi elimu bure kuanzia shule ya awali hadi chuo kikuu. Serikali ya CCM imekuwa ikichukua ajenda zetu bila kukiri, zipo katika ilani yetu ya uchaguzi,” alisema na kuongeza kuwa hata pendekezo hilo la Mkapa ni mlolongo huohuo wa kukwapua ajenda zao.
“Wengi watakuwa mashahidi wa hali duni ambayo baadhi ya shule hizo (za umma) zinapitia ikiwamo ukosefu wa majengo hasa mabweni, vyumba vya madarasa, posho za walimu, mishahara midogo na uhamisho wa walimu uliofanyika hivi karibuni kwa walimu ambao ni sawa na kushushwa cheo.”
Lowassa ambaye kabla ya kuhamia Chadema alikwama katika mchujo wa urais kupitia CCM, alisema, “Nachelea kusema kuwa hii si ajenda yao (Serikali ya CCM), hawataweza kulisimamia kwa sababu wanataka kuendelea kutawala na hawataki kuwa na taifa lililoelimika vizuri, linaloweza kuhoji.”
Mwanasiasa huyo alisema hata takwimu za uchaguzi mkuu uliopita zinaonyesha kuwa maeneo ambayo CCM ilishinda kihalali maendeleo yako nyuma.
Alisema njia pekee ya kuiondoa CCM madarakani mwaka 2020 ni kuupa upinzani nchi ili utekeleze kwa ufasaha na umahiri ajenda ya elimu nchini, huku akikumbushia namna alivyosimamia shule za kata na kuzifanya zitoe elimu ya kiwango wakati akiwa waziri mkuu.
Tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, imekuwa ikitekeleza sera ya elimu bure kuanzia shule za msingi hadi kidato cha nne, ingawa zimekuwapo changamoto za ukosefu wa madarasa, madawati, maabara na huduma nyingine mbalimbali.
Kauli hiyo ya Lowassa imemwamsha katibu wa Itikadi na uenezi wa CCM Zanzibar, Catheline Peter Nao aliyesema si kweli kwamba CCM inachukua ajenda za Lowassa, bali yeye ndiye alizipeleka CCM na kuzipeleka upinzani.
Alisema Lowassa alikuwa CCM wakati ilani ya uchaguzi mkuu aliyokabidhiwa Rais John Magufuli inaandaliwa.
“CCM inapenda kuongoza watu wenye elimu na ndiyo maana inatoa elimu bure ili kuwapa watoto fursa ya kusoma na kuelimika zaidi, hivyo si kweli kwamba CCM inataka kuongoza wajinga,” alisema Catherine.
Akizungumzia kauli hiyo ya Mkapa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Leonard Akwilapo alisema wameupokea ushauri ulitolewa na Rais huyo mstaafu.
Dk Akwilapo alisema “Huyu (Mkapa) ni Rais mstaafu, tumepokea kwa heshima kabisa ushauri wake na tutaufanyia kazi na wadau wengine pia. Lengo la wizara hii ni kuwa na Taifa lenye watu walioelimika kwa kiwango kinachotakiwa,” alisema.
Alisema ushauri wa Mkapa utafanyiwa kazi kwa njia mbalimbali ikawamo kupitia Baraza la Ushauri la Waziri linalotarajiwa kuundwa hivi karibuni ambalo litajumuisha wanataaluma mbalimbali na wadau wa elimu.
Hata hivyo, Waziri Kivuli wa Elimu, Suzan Lyimo alisema anaunga mkono kauli ya Mkapa lakini akamlaumu akisema alikuwa na uwezo mkubwa wa kushughulikia jambo hilo akiwa madarakani kuanzia mwaka 1995 hadi 2005.
“Sitaki kumlaumu sana ila namshukuru kwa kuona makosa kwenye elimu. Haya mambo upinzani tumeyasema sana katika bajeti zetu mbadala, lakini utekelezaji wake hakuna,” alisema Lyimo ambaye pia ni mbunge wa Viti Maalumu (Chadema).
Mbali na Lyimo, kauli ya Mkapa iliungwa mkono na wadau wa elimu, waliompongeza wakisema inalenga kuboresha elimu ya Tanzania huku wengine wakisema ni nzuri lakini imechelewa.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirikisho la Watoaji Elimu Wasiotegemea Serikali Kusini mwa Jangwa la Sahara (CIEPSSA), Benjamin Nkonya alisema ni wazo zuri lakini anajua ni wapi litakwama kwa kile alichodai kuwa kuna baadhi ya watendaji wa wizara husika hawapo tayari kwa mabadiliko.
Mhadhiri Msaidizi wa Idara ya Lugha za Kigeni na Isimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Faraja Kristomus aliungana na Mkapa ingawa alisema uamuzi wake umechelewa.
“Ni jambo zuri lakini limechelewa, kwa sababu kilio cha kuhitimisha mjadala wa kujadili suala la elimu kimesemwa sana huko nyuma, ila nampongeza na endapo wahusika walioko madarakani watalifanyia kazi tutapiga hatua,” alisema Kristomus.
Comments
Post a Comment