Kitendo cha mawaziri wawili kutohudhuria mkutano muhimu wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) kimemkwaza mwenyekiti wa baraza hilo, Rais John Magufuli.
Mkutano huo uliwakutanisha wafanyabiashara na watendaji waandamizi wa Serikali, lakini mawaziri wawili, Dk Charles Tizeba (Waziri wa Kilimo) na Luhaga Mpina (Mifugo na Uvuvi) hawakuhudhuria huku Rais akiwa hana taarifa zao na hawakutuma wawakilishi kwenye mkutano huo.
Kutokuwapo kwa mawaziri hao kulibainika baada ya Rais Magufuli kumtaka Mpina ajibu masuala mbalimbali yaliyoibuliwa na mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Asas Dairies ya Iringa, Fuad Abri kuhusu bidhaa za maziwa. Pia alitaka ataje idadi ya viwanda vya maziwa vilivyopo hapa nchini.
Hata hivyo, si waziri huyo, wala mwakilishi yeyote kutoka wizarani kwake aliyekuwapo kwenye mkutano huo wa kumi na moja wa baraza hilo na ndipo Rais Magufuli alipomtaka waziri wa kilimo kujibu swali hilo kwa sababu alikuwa akisimamia wizara hiyo kabla ya kuitenganisha. Hata hivyo, naye hakuwapo na hapakuwa na mwakilishi yeyote.
Jambo hilo lilionekana kumshangaza Rais ambaye alihoji iwapo mawaziri hao walipewa mwaliko. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisimama na kujibu kwamba walipewa kwa kuwa ni wajumbe wa mkutano huo.
“Mawaziri wote wanaoguswa na sekta za uwekezaji na hasa kwenye uchumi huu wa viwanda, kilimo ni facilitator (mwezeshaji) wa viwanda, mifugo nayo pia ni viwanda. Walikuwa wanapaswa kuwepo hapa kwa sababu walishapewa taarifa wote,” alisema Majaliwa.
Rais Magufuli alisema inasikitisha kuona baadhi ya watu aliowateua hawajaelewa anataka nini. Alisema inashangaza kuona wafanyabiashara kutoka sehemu mbalimbali nchini wamekutana na Serikali kuzungumzia masuala ya kilimo na mifugo, lakini mawaziri wa sekta hizo hawapo.
“Tunaongelea mambo ya kilimo na mifugo, lakini waziri au katibu mkuu hayupo hapa, itabidi waziri mkuu achukue hizi kero zenu akazifanyie kazi,” alisema Rais Magufuli na kumtaka Waziri Mkuu Majaliwa kuunda timu itakayowahusisha mawaziri wanaohusika ili wakayafanyie kazi malalamiko yaliyoibuliwa na wafanyabiashara katika mkutano huo.
Alipotafutwa kuzungumzia kutokuwapo kwake katika mkutano huo, Mpina alisema hawezi kuzungumzia jambo hilo, bali anafuatilia kwa ukaribu kujua nini kimetokea katika mawasiliano hayo.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega alipoulizwa alisema hakuwa na taarifa kwani alikuwa katika safari ya kikazi mkoani Kigoma tangu Ijumaa akiwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mifugo, Uvuvi na Maji.
“Sikuwa na taarifa yoyote ya kuhudhuria mkutano huo, na nilipangiwa kazi na mkuu wangu ambaye ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, nitembelee na kukagua miradi mbalimbali ya Serikali mkoani Kigoma,” alisema kwa simu jana.
Ulega alisema hakuwa na taarifa yoyote kama Rais aliuliza uwapo wa viongozi wa wizara hiyo wakati wa mkutano huo, “Nilikuwa ndani ya ndege tangu saa nane mchana nilipotoka Kigoma na hadi muda huu (saa 10 alasiri) unanipigia simu ndiyo kwanza nashuka kwenye ndege.”
Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Yohana Budeba alisema yupo kikazi mjini Dodoma.
Hata hivyo hakutaka kuzungumza chochote kuhusiana na kutokuwapo kwenye mkutano huo.
“Niko Dodoma kwa sasa na siwezi kuongelea hayo masuala kwenye simu, ni vizuri tukionana ana kwa ana, maana sijui hata ninaongea na nani,” alisema.
Wakati viongozi hao wa wizara ya mifugo wakitoa maelezo hayo, Dk Tizeba na naibu wake, Mary Mwanjelwa hawakutaka kuzungumza lolote kuhusu kikao hicho wakisema walikuwa kwenye kikao.
Hii si mara ya kwanza kwa mawaziri hawa kuingia matatani. Katika mkutano wa Bunge wa Februari, Mpina na Dk Tzeba waliwekwa ‘kitimoto’ baada ya wabunge baadhi yao kuibua hoja mbalimbali dhidi yao wakati wakichangia taarifa za utekelezaji wa shughuli za kamati mbili za kilimo, mifugo, maji na Ardhi, Maliasili na Utalii.
Mbunge wa Busega (CCM), Dk Raphael Chegeni alimshukia Mpina akisema anakuwa na kiburi na kumtaka aache kwa kuwa anawaumiza wafugaji.
Hata hivyo, Mpina alijibu ‘mashambulizi’ yaliyoelekezwa kwake akisema ataendelea kufanya kazi kwa weledi bila woga wa kumshughulikia mtu yeyote anayekwenda kinyume cha sheria.
Dk Tizeba alishambuliwa na wabunge wanaotoka katika ukanda wa kilimo cha mahindi waliotaka kujua mkakati wa Serikali wa kuongeza bei ya mahindi.
Hata hivyo, kiu ya wabunge hao haikukatwa baada ya Dk Tizeba kuweka msimamo kuwa mazao hayo yanasimamiwa kwa mujibu wa sheria.
Dk Tzeba pia aliwahi kukutana na joto la Dk Magufuli Januari mwaka huu wakati Rais akimwapisha Doto Biteko kuwa naibu waziri wa madini.
Rais Magufuli alisema haiwezekani baadhi ya mikoa, ikiwamo inayotegemewa kwa uzalishaji wa chakula kwa wingi, kushindwa kupata mbolea, huku yeye (Dk Tizeba) akiwa hajachukua hatua.
Alitoa maagizo kwa waziri huyo kushughulikia malalamiko ya uhaba wa mbolea katika Mkoa wa Rukwa na maeneo mengine ya jirani na kutaka hadi Ijumaa ya Januari 12 mbolea iwe imefika katika mikoa hiyo.
“Ninapozungumza hapa ndugu zangu, ipo mikoa haijapelekewa mbolea, ikiwamo mikoa ya Rukwa sijui na mkoa gani. Wakati tunaizungumzia kama ‘the big four’ kwa ‘production’ ya chakula, mbolea bado haijapelekwa, lakini waziri wa kilimo yupo.
“Nimempa maagizo Waziri Mkuu mbolea isipofika huko ndani ya wiki hii, huyo anayehusika na kupeleka mbolea aache kazi, labda tukianza kukimbizana tutajifunza.”
Comments
Post a Comment