Skip to main content

Featured

Maombolezo: Hii ndiyo Hali Ilivyo Tanzania Bendera Yapepea Nusu Mringoti

Agizo la Rais John Magufuli la Bendera ya Taifa kupepea kwa nusu mlingoti kwa siku tatu kuanzia leo Septemba 22 kufuatia ajali ya kivuko cha MV Nyerere iliyotokea mkoani Mwanza limetekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Dk Slaa azungumzia maandamano nchini Sweden, polisi waonya



Wakati polisi wakitoa tahadhari kwa wananchi kuhusu maandamano yaliyoratibiwa kwenye mitandao ya kijamii na kupangwa kufanyika leo, Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Dk Wilbrod Slaa amesema ofisi yake ilipokea barua kutoka polisi wa nchi hiyo kuhusu taarifa za Watanzania waliotaka kuandamana jana.
Hata hivyo, hapa nchini polisi imeonya ikisema maandamano hayo ni batili na atakayeshiriki atashughulikiwa.
Akizungumza na gazeti hili kutoka nchini Sweden, Dk Slaa alisema jana kuwa, polisi walisema wameshawapa kibali waandamanaji na watawapa ulinzi unaostahili.
“Ilipofika saa tatu asubuhi, walifika watu kumi, polisi hawakuwa na kazi kubwa waliwapangia wapi wasimame, walikuja na mabango yao. Lakini hakukuwa na muziki kwa sababu huku hawatakiwi kupiga muziki,” alisema.
Alisema baada ya kuwaona waandamanaji hao wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali, walikubaliana na polisi kuwa waingie ndani ili kujua nini wanachohitaji.
“Walikataa kuingia ndani na wakasema hawana sababu ya kujadiliana. Tukawaambia tunawaomba watupe viongozi wawili ili wawe wawakilishi na viongozi hao waseme nini wanachotaka. Lakini pia walikataa,” alisema.
Dk Slaa alisema Sweden ni moja ya nchi zenye vyama vya Watanzania vilivyosajiliwa kuanzia ngazi ya mkoa na kuendelea na viongozi wa vyama hivyo walipiga simu ubalozini wakimsifu Rais Magufuli.
“Nimepokea simu kutoka sehemu mbalimbali, kwamba wanamuunga mkono Rais John Magufuli. Wanataka Rais asilegeze kamba katika vita dhidi ya rushwa na matumizi mabaya ya mali za umma kwa sababu vita hivyo vinatengeneza maadui ndiyo maana mambo kama haya yanatokea,” alisema.
Kuhusu ujumbe aliosema ni wa upotoshaji ulioandikwa kwenye mabango ya waandamanaji hao, Balozi Slaa alisema unamhukumu Rais kwa mambo ambayo mahakama haijathibitisha.
Polisi nchini yaonya
Akizungumza na waendesha bodaboda jana, kaimu kamanda wa polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Sweetbert Njolike alisema jeshi hilo limejipanga kuhakikisha kila mtu anafanya shughuli zake kama kawaida bila uvunjifu wowote wa amani.
“Niwahakikishie Jeshi la Polisi tumejipanga na mkoa wetu utaendelea kubaki salama hakuna maandamano yatakayofanyika, hivyo kila mtu aendelee na shughuli zake kama kawaida,” alisema.
Wakati hayo yakijiri Dar es Salaam, polisi mkoani Mwanza walifanya onyesho la utayari wa kiutendaji na vifaa vyao kwa kuzunguka mitaa kadhaa jijini humo.
Msafara wa magari zaidi ya 15 yaliyokuwa yamewasha taa na kupiga ving’ora ulihusisha askari wenye sare za kikosi cha kutuliza ghasia (FFU), waliobeba silaha na kujihami kwa zana na vifaa vya kudhibiti na kukabiliana na ghasia. Miongoni mwa magari yaliyozungushwa mitaani ni ya doria ya kila siku, gari la maji ya kuwasha na malori, yote yakiwa na askari.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema wamejiandaa kikamilifu kukabiliana na kuwadhibiti wote watakaothubutu kujitokeza mitaani leo kushiriki maandamano yanayohamasishwa kupitia mitandao ya kijamii.
“Kutakuwa na doria ya askari wenye sare na wasio na sare mitaani na maeneo yote ya Mkoa wa Mwanza, watakaothubutu kuandamana watasimulia wengine kitakachowapata,” alisema.
Mkuu wa mkoa huo, John Mongella aliunga mkono kauli hiyo akisema maandamano hayo ni haramu kisheria kwa sababu hadi leo hakuna taarifa iliyotolewa polisi kwa mujibu wa sheria.
Kutoka Dodoma polisi walipita mitaani baadhi wakiwa kwenye magari na wengine wakikimbia.
Kamanda wa polisi mkoani humo, Gilles Muroto alisema watakaothubutu kuandamana watakabiliwa na jeshi hilo ipasavyo.
Mkoani Mtwara, kamanda wa polisi wa mkoa huo, Lucas Mkondya alisema watu wachache wanaohamasisha maandamano wasithubutu kuandamana kwa kuwa watapambana na nguvu ya dola na madhara yatakayotokea jeshi hilo lisilaumiwe.
Alisema katika kufuatilia wanaochochea, kuyahamasisha na kumkashifu Rais, wanafunzi tisa wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine tawi la Mtwara wanashikiliwa.
“Wawili kati yao upelelezi tumekamilisha na kuwafikisha mahakamani, waliobakia tunaendelea kukamilisha upelelezi,” alisema.
Kwa upande wa Morogoro, mkuu wa mkoa huo, Dk Stephen Kebwe alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kushirikiana kudhibiti maandamano yasiyo halali yaliyopangwa kufanyika leo.
“Kama kuna watu wanataka kuandamana basi wajifungie chumbani waandamane lakini wakijaribu kuingia barabarani polisi hakikisheni mnawashughulikia,” aliagiza Dk Kebwe.
Kamanda wa polisi mkoani humo, Ulrich Matei alisema kwamba wapo askari na vifaa vya kutosha kukabiliana na maandamano hayo.
Marekani waandamana
Wakati huohuo, baadhi ya Watanzania wanaoishi nchini Marekani waliandamana hadi katika ofisi za ubalozi wa Tanzania mjini Washington kuwasilisha madai yao.
Baadhi ya picha zilizotumwa kwenye mitandao ya kijamii ziliwaonyesha waandamanaji hao wakiwa na mabango wakiwa nje ya ubalozi huo huku wengine wakisikika wakizungumza mambo mbalimbali.
Baadaye watu hao waliokuwa wakizungumza Kiswahili walijipanga kando ya barabara wakiimba na kuendelea kuonyesha mabango yao.
Imeandikwa na Fortune Francis, George Njogopa (Dar), Saada Amiri (Mwanza), Florah Temba (Moshi), Hamida Shariff (Morogoro) na Haika Kimaro (Mtwara).

Comments

Popular Posts