LEO ni siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, zilizoungana miaka 54 iliyopita. Maadhimisho hayo yanaendelea kwenye uwanja wa Jamuhuri mjini Dodoma. Sherehe hizo zinapambwa na mgeni rasmi, Amri Jeshi Mkuu wa Majeshi la Ulinzi na Usalama, Rais John Magufuli na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein. Siku hii ni kumbukumbu ya kuzaliwa Tanzania baada ya nchi hizo mbili kuungana pamoja na wananchi wa pande zote mbili.
Maadhimisho ya mwaka huu ni ya 54 tangu kuzaliwa kwa Tanzania na ni mara ya pili mfululizo, kufanyika katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma.
Katika maadhimisho hayo ya mwaka jana, mgeni rasmi alikuwa ni Rais Magufuli.
Aprili 26, 1964 waasisi wa taifa hili, Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume waliunganisha nchi mbili, Tanganyika na Zanzibar, kwa kuchanganya udongo wa pande hizo mbili.
Kwa miaka mingi maadhimisho hay,a yalikuwa yanafanyika katika Uwanja wa Uhuru (Shamba la Bibi) jijini Dar es Salaam.
Lakini tangu Rais Magufuli aingie madarakani, huu ni mwaka wa pili mfululizo yanafanyika Dodoma, mahali ambapo ni makao makuu ya nchi.
Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inasema Muungano huu ni wa mfano pekee duniani: Tuulinde, Tuutunze, Tuuimarishe na Kuudumisha kwa maendeleo ya Taifa letu".
Maadhimisho ya mwaka huu, pamoja na vikundi vya makomandoo, vijana zaidi ya 500 kutoka katika shule mbalimbali mjini Dodoma, wataonesha sanaa, michezo na burudani kwa matukio katika picha za viongozi waasisi wa nchi.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Binilith Mahenge aliwataka wakazi wa Dodoma na mikoa jirani kufika kwa wingi kwenye sherehe hii muhimu.
Katika kuhakikisha siku ya leo inasheherekewa kwa amani na usalama, Jeshi la Polisi nchini limesema limejipanga kuhakikisha kunakuwa na amani na utulivu.
Hayo yalisemwa jana na Msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini, Barnabas Mwakaluka wakati akizungumza na gazeti hili.
“Jeshi la polisi halijajipanga kudhibiti shughuli nyingine, jeshi limejipanga kila siku kupambana na uhalifu na kwa mfano sasa tunashiriki katika tukio hili muhimu la muungano, hivyo litahakikisha kunakuwa na amani na utulivu,” amesema Mwakaluka.
Aliongeza na kusema kuwa kutakuwepo na askari wanaozunguka mitaani ikiwa ni sehemu ya kusimamia usalama wakati wa hayo.
Comments
Post a Comment