Skip to main content

Featured

Maombolezo: Hii ndiyo Hali Ilivyo Tanzania Bendera Yapepea Nusu Mringoti

Agizo la Rais John Magufuli la Bendera ya Taifa kupepea kwa nusu mlingoti kwa siku tatu kuanzia leo Septemba 22 kufuatia ajali ya kivuko cha MV Nyerere iliyotokea mkoani Mwanza limetekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Mabasi yote ya abiria kudhibitiwa


MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) imesema kwamba mpaka ifikapo Juni 30, mwaka huu, mabasi yote ya abiria nchini yatakuwa yameunganishwa kwenye mfumo wa ufuatiliaji wa mwenendo wa mabasi.
Mfumo huo unaojulikana kama VTS (Vehicle Tracking System) una lengo la kuhakikisha usalama na ulinzi wa abiria na mali zao, unapewa kipaumbele wakati wote wa safari.
Imeelezwa kwamba, Mfumo wa VTS ambao ulianzishwa kwa majaribio mwezi Desemba mwaka 2016, umefanikiwa kwa sehemu kubwa kutokana na kupungua kwa ajali za mabasi nchini. Wakati mfumo huo unaanzishwa Desemba 2016, hadi kufikia Januari mwaka 2017 jumla ya mabasi 40 yalikuwa yameunganishwa.
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra, Gilliard Ngewe alisema mfumo wa VTS unaiwezesha Sumatra kufuatilia mwenendo mzima wa mabasi tangu yanapoanza safari hadi mwisho wa safari.
Alisema ikilinganishwa na miaka ya nyuma, hivi sasa ajali za mabasi nchini zimepungua kwa kiasi kikubwa, kwa kuwa wenye mabasi na madereva, wanajua kuwa wanafuatiliwa muda wote ili kubaini makosa yanayofanywa na madereva hao wawapo safarini.
"VTS inatuwezesha kufuatilia mwenendo mzima wa basi husika ikiwemo mwendokasi, matumizi mabaya ya breki ikiwemo kufunga breki kwa ghafla, basi kusimama njiani kwa muda mrefu, gari kubadilisha njia pamoja na ulevi kwa madereva," alieleza Ngewe.
Kwa mujibu wa Ngewe, mfumo huo ulianza rasmi mwezi Oktoba mwaka jana baada ya kupitishwa kwa Kanuni ya Mabasi ya Abiria ya mwaka 2017, ambapo mpaka sasa mabasi 859 tayari yameshaunganishwa kwenye mfumo huo.
Ngewe aliliambia Habari Leo kuwa hadi ifikapo Juni 30 mwaka huu, mabasi yote ya abiria nchini yatakuwa yameshaunganishwa kwenye mfumo wa VTS, na baada ya hapo yatafuata malori, magari madogo na pikipiki.
Alisema kwa sasa mfumo huo, unafanya kazi kwa mabasi yanayotoka Dar es Salaam kwenda Kanda ya Ziwa, Nyanda za Juu Kusini mikoa ya Sumbawanga, Mbeya, Iringa na Ruvuma. Mabasi yanayotoka Dar es Salaam kwenda Kilwa, Lindi hadi Masasi, yataunganishwa kwenye VTS wiki hii. Baada ya hapo itafuata Tanga, Moshi, Rombo na Arusha. "Mwaka 2015 tulitenga Shilingi bilioni 3 kwa ajili ya kuanzisha mfumo huu na kituo chake kipo Mikocheni hapa Dar es Salaam.
Kwa kutumia mfumo wa VTS, dereva wa basi anapokwenda kwa mwendokasi wa zaidi ya kilomita 86 kwa saa, kifaa (VTS) tulichokifunga kwenye basi hilo kinapiga kelele (alarm) kuashiria kwamba basi liko kwenye mwendokasi au kama limehama njia linaonekana, na sisi Mamlaka tunakuwa tunaona kila kitu kinachofanyika," alieleza Ngewe.
Alisema utekelezaji wa mfumo huo wa kufuatilia mwenendo wa mabasi ya abiria ni sehemu ya utekelezaji wa Kampeni ya miaka Kumi ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2011-2020 ya kupunguza ajali.
Mkurugenzi Mkuu huyo alisema kuwa kwa sasa adhabu zinazotolewa kwa madereva, wanaokiuka sheria za usalama barabarani, ambao mabasi yao yameshaunganishwa na mfumo wa VTS, ni zile zinazotolewa na Jeshi la Polisi ikiwemo faini ya Sh 30,000.
Alisema baada ya mabasi yote kuunganishwa kwenye VTS ifikapo Juni 30 mwaka huu, ndipo adhabu ya Sumatra ya faini ya Sh 250, 000 itaanza kufanya kazi.
"Kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa sheria na alama za barabarani, hivyo kupitia mfumo huu tunataka tuwe na madereva wenye taaluma ya udereva na wenye leseni Daraja 'C' inayowaruhusu kuendesha mabasi ya abiria; wawe wamepitia mafunzo maalumu ya udereva ya wiki mbili kwenye Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT) au VETA," alisisitiza Ngewe.
DAR LUX WAZUNGUMZIA VTS
Mmoja wa wamiliki wa mabasi aliyezungumza na gazeti hili, ameipongeza Sumatra kwa kuanzisha mfumo huo wa kufuatilia mwenendo wa mabasi yao wakati wote wa safari.
Mkurugenzi ambaye pia ni mmiliki wa Kampuni ya Mabasi ya Dar Lux, Donald Simagunga aliliambia HabariLeo kuwa kupitia mfumo wa VTS, ameweza kuokoa lita 80 za dizeli kwa kila basi kwa safari moja linalosafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza.
Simagunga alisema kuwa kabla ya kuanza kwa mfumo wa VTS, alikuwa akitumia lita 500 za mafuta ya dizeli kwa safari moja tu, lakini hivi sasa anatumia lita 420 tu kwa kila safari.
Alisema basi linapokwenda kwa mwendo kasi, ndivyo mafuta yanavyotumika zaidi, hivyo utaratibu wa kuyaunganisha kwenye VTS umempunguzia gharama za matumizi ya mafuta.
Faida zingine alizozitaja ni matairi kudumu kwa muda mrefu, kwa kuwa mwendo unakuwa wa kawaida, gharama za matengenezo zimepungua kwa sababu uwezekano wa basi kuharibika umekuwa mdogo, umakini wa madereva barabarani umeongezeka na kupungua kwa ushindani kati ya wamiliki wa mabasi, kwa kuwa wote wanasafiri kwa mwendokasi sawa.
CHANGAMOTO
Mbali na faida hizo, Simagunga alisema kuwa changamoto wanayokumbana nayo ni tochi za polisi, ambazo wakati mwingine zinasoma mwendokasi, tofauti na VTS.
Alisema hilo ni tatizo kwa sababu mabasi yake, yanazingatia mwendokasi uliowekwa na Sumatra kupitia VTS, lakini tochi za polisi wakati mwingine zinasoma tofauti.
Ili kukabiliana na tatizo hilo, Simagunga aliiomba Serikali pamoja na Sumatra, kulifanyia kazi tatizo hilo ili mamlaka au idara zote za Serikali, zifanye kazi kwa usawa na kuondoa kero hiyo. Kero nyingine aliyoitaja ni mabasi kuamuliwa kulala njiani nyakati za usiku.
Alisema kwa kuzingatia umuhimu wa kukuza uchumi kwa nyakati hizi, kama kaulimbiu ya Serikali ya Awamu ya tano inavyosema, alitoa wito kwa Serikali kupitia upya maamuzi hayo, iliyoyatoa miaka ya 1990 ili mabasi yafanye kazi saa 24.
"Hivi sasa barabara ni nzuri ikilinganishwa na zamani, usalama upo na kwa maeneo hatarishi polisi wasaidie kuyalinda mabasi ili watu wafanye kazi saa 24, hilo ni tatizo linaloturudisha nyuma badala ya kwenda mbele," alieleza Simagunga na kuongeza,
"Nilishawahi kukutana na kesi kama mbili hivi za baadhi ya abiria ambao wagonjwa kufia njiani kutokana na amri ya mabasi kutosafiri usiku. Ukosefu wa huduma muhimu kama vile chakula, malazi na vyoo kwenye maeneo ambayo mabasi hulazimika kulala nayo ni changamoto, kwa kuwa baadhi ya abiria kujisaidia ndani ya basi kwa kuogopa kutoka nje usiku," alisema.

Comments

Popular Posts