HAKIMU wa Mahakama ya Watoto Zanzibar, Naila Abdulbasit amewataka mahakimu kutumia lugha nyepesi ambayo haiwezi kumtisha mtoto wakati wanaposikiliza kesi za watoto mahakamani.
Akizungumza katika warsha ya kujenga uelewa wa sheria kwa mahakimu, polisi na wanasheria, Abdulbasit alisema ni vyema kesi za watoto hasa zile za udhalilishaji wa kijinsia zikasikilizwa faragha na sio kila mtu kuweza kusikiliza anachohojiwa mtoto.
“Mtoto kama hawezi kujieleza vizuri, mahakimu mnao uwezo wa kuahirisha kesi kwa siku hiyo na kuja kuisikiliza tena au kutumia ushahidi kwa njia ya kieletroniki,”alisema.
Aidha alisema sauti za wanaharakati wa kupinga vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia zimesaidia kufanya baadhi ya sheria kurekebishwa, hali ambayo imesaidia kuongezeka kwa hukumu kwa mtu atakayebaini na kosa la udhalilishaji.
Alieleza kuwa baadhi ya mahakama zimeongezewa uwezo wa kuwatia hatiani watakaobainika kufanya matendo hayo. "Hapo mwanzo mahakama za wilaya uwezo wake ulikuwa kufunga miaka mitano lakini hivi sasa inao uwezo wa kutoa hukumu miaka saba na Mahakama ya Mkoa zimepewa uwezo wa kufunga hadi miaka 14,"alisema.
Hakimu wa Mahakama ya Wilaya, Ali Abdulrahman alisema hivi sasa kesi nyingi zinazowasumbua mahakamani ni kesi za kutoroshwa wasichana ambazo walalamikaji wake wanakuwa wameshakubaliana na wenza wao, hivyo wakifikishwa mahakamani huwa hawataki kutoa ushahidi.
"Sheria inamtambua mtoto ni aliye chini ya umri wa miaka 18, ambao wengi wakifika miaka 15 au 16 ambao wamekubaliana na wenza wao, hivyo mtu huyo huwa hayupo tayari kutoa ushahidi mahakamani, hili liangaliwe,"alisema.
Naibu Mrajisi wa Mahakama Kuu Zanzibar, Salum Hassan Bakar aliitaka jamii endapo ikiwa kuna hakimu anakwenda kinyume na kazi zake ni vyema kufuata sheria ili kuweza kumripoti katika sehemu husika ili aweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Comments
Post a Comment