KATIKA mwaka wa fedha 2017/18, Wizara ya Katiba na Sheria ilitaifisha mali zenye thamani ya Sh bilioni 5.68 kutoka kwa washtakiwa waliotiwa hatiani, ikiwemo dhahabu kilogramu 24.5 zenye thamani ya Sh bilioni mbili.
Pamoja na hayo, wizara hiyo ilitaifisha fedha za kigeni kutoka mataifa 15 zenye thamani ya Sh milioni 908 na magari matano ya kifahari aina ya Rangerover Vogue na moja aina ya Audi yaliyokamatwa katika bandari ya Dar es Salaam yakisafirishwa kama nguo za mitumba.
Hayo yalibainishwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, wakati akiwasilisha bungeni Dodoma Mpango wa Makadirio ya Bajeti ya wizara hiyo, kwa mwaka wa fedha 2018/19.
Ametaja mali nyingine zilizotaifishwa kutoka kwa washtakiwa hao waliotiwa hatiani kuwa ni pamoja fedha zilizotozwa kwa washtakiwa hao kama faini kiasi cha Sh bilioni 2.4, pikipiki 34, mafuta, mashine za kuhesabia fedha na basi la abiria lililokuwa likitumika kusafirishia meno ya tembo.
"Pia katika kipindi hicho mali za vyama vya ushirika vya Mwanza, Nyanza Cooperative Unioni na Shinyanga (Shirecu) zikiwemo nyumba, viwanja na viwanda vilirejeshwa serikalini kutoka mikononi mwa watu waliozichukua bila kufuata utaratibu wa kisheria," alieleza.
Pia Profesa Kabudi alisema wizara hiyo katika mwaka wa fedha 2017/18 ilipokea jumla ya maombi 14 ya kurejesha watuhumiwa wa makosa mbalimbali ya jinai waliopo katika nchi za Rwanda, Zambia, Kenya, Malawi, Marekani na Uingereza.
"Wizara pia katika kipindi hicho iliwasilisha maombi manne ya kurejeshwa nchini kwa watuhumiwa wanaokabiliwa na makosa mbalimbali waliopo katika nchi za Rwanda, Uganda, Zambia na Afrika Kusini," alisema.
Alieleza kuwa makosa hayo yalihusisha makosa ya usafirishaji wa dawa za kulevya, mauaji ya kimbari, wizi, mauaji, makosa ya kimtandao na ubakaji.
"Wizara itaendelea na kushirikiana na mataifa mengine katika kukabiliana na uhalifu unaovuka mipaka kwa kuzingatia sheria zetu na mikataba ya kimataifa iliyosainiwa na kuridhiwa nchini."
Alisema pia wizara hiyo imeandaa rasimu ya mapendekezo ya marekebisho ya sheria inayosimamia ushirikiano wa kimataifa katika masuala ya jinai ili kuweza kunufaika zaidi na ushirikiano huo.
Halikadhalika, Profesa Kabudi alisema katika mwaka wa fedha 2017/18, Kamati ya Nidhamu ya Mawakili ilipokea malalamiko 18 ya mawakili na kufanya jumla ya malalamiko yaliyokuwa mbele ya kamati hiyo kufikia 48.
Alisema katika kipindi hicho, malalamiko 22 yalisikilizwa na kutolewa uamuzi ambapo mawakili sita wamesimamishwa kufanya kazi ya uwakili kwa muda wa kati ya miezi sita hadi miaka mitano.
Pamoja na hayo alisema katika mwaka wa fedha 2017/18, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iliendelea kutoa ushauri wa kisheria kwenye mikataba na makubaliano mbalimbali yanayofanywa na wizara, idara na taasisi za serikali.
Alisema hadi kufikia Machi, mwaka huu, ofisi hiyo ilihakiki na kutoa ushauri wa mikataba 1,068 yenye thamani ya Sh trilioni 2.36 na dola za Marekani bilioni 6.42.
"Hii ni mikataba inayohusu ununuzi, ukarabati wa majengo, utoaji wa huduma za jamii na ujenzi wa miundombinu ikiwemo barabara. Pia tulitoa ushauri kwa serikali katika masuala ya sheria zinazohusu sekta mbalimbali kupitia mikutano ya kikanda na kimataifa hususani mikutano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, SADC, AU na UN," alisema.
Aidha, waziri huyo alieleza jitihada zilizofanywa na wizara hiyo katika kupunguza tatizo la mlundikano wa mashauri mahakamani ambapo hadi kufikia Machi, mwaka huu, mahakama iliamua jumla ya mashauri 141,107 katika ngazi zote za mahakama sawa na asilimia 98 ya mashauri yote yaliyosajiliwa na asilimia 67 ya mashauri yote yaliyokuwepo mahakamani kipindi hicho.
Alisema katika kupunguza mlundikano, serikali ilifanikiwa kupunguza tatizo hilo katika Mahakama za Mwanzo, wilaya ba za Hakimu Mkazi. Hadi mwishoni mwa Machi, mwaka huu, kulikuwa na jumla ya mashauri 26,259 katika Mahakama za Hakimu Mkazi na za wilaya, mashauri 5,220 yalikuwa na miezi zaidi ya 12 ikiwa ni sawa na asilimia 19.
Katika Mahakama za Mwanzo, takwimu zinaonesha kati ya mashauri 16,639 yaliyobaki Machi, mwaka huu, ni mashauri 253 tu yalikuwa na umri zaidi ya miezi sita tangu kusajiliwa sawa na asilimia 1.5 ambao kwa Mahakama ya Mwanzo huhesabiwa kuwa ni mlundikano.
Akielezea mwenendo wa uendeshaji wa mashtaka, Profesa Kabudi alisema hadi Machi, mwaka huu, jumla ya mashauri ya jinai 17,339 yalifunguliwa Mahakama Kuu na 2,341 yalifunguliwa kama rufaa za Mahakama Kuu.
Kati ya hayo mashauri 1,719 yalihitimishwa sawa na asilimia 49 ya mashauri yaliyopo na mashauri 1,788 yanaendelea katika hatua mbalimbali. Alisema pia katika kipindi hicho jumla ya mashauri 886 yanayohusu wanyamapori yalifunguliwa katika mahakama mbalimbali nchini pamoja na mashauri 2,593 ya dawa za kulevya pamoja na mashauri sita yanayohusu vitendo vya ukatili dhidi ya watu wenye ualbino yaliyoshughulikiwa.
"Kati ya mashauri hayo manne yalikamilika na watuhumiwa kutiwa hatiani na kuhukumiwa adhabu ya kifungo cha kati ya miaka minne hadi 20 na mashauri yaliyobaki yanaendelea kusikilizwa," alisema.
Katika mwaka wa fedha wa 2018/19 waziri huyo aliliomba Bunge liidhinishe jumla ya Sh bilioni 189 kati ya fedha hizo Sh bilioni 141 ni kwa ajili ya matumizi ya Mfuko wa Mahakama.
Comments
Post a Comment