Mkuu wa mkoa Arusha Mrisho Gambo na waombolezaji wengine wakibeba Geneza la Leyla Mtumwa kupelekwa msikitini kuswaliwa kabla ya kwenda kuzikwa Jana.
Arusha. Mamia ya wakazi wa Jiji la Arusha, wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa Mrisho Gambo wameshiriki kuaga na kumzika Mtanzania Leyla Mtumwa (36) aliyefariki, Uingereza, Machi 30 mwaka huu.
Mwili wa Leyla uliwasili juzi saa 12 jioni na ndege ya Shirika la Qatar na kupelekwa katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru.
Jana mchana mwili ulipelekwa nyumbani kwao, eneo la Kaloleni ambako ibada ya kuswalia mwili huo ilifanyika.
Leyla alifariki dunia kwa kuchomwa visu na mume wake, Kema Kasambula, nyumbani kwao, Kirkstall Avenue, Haringey, Uingereza.
Gambo pamoja na mamia ya waombelezaji jana walijitokeza katika msiba huo, licha ya kuwapo mvua kubwa jijini hapa.
Mwili uliwasili saa saba mchana kutoka Hospitali ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru na kupelekwa nyumbani.
Mwili huo ulizikwa katika makaburi ya familia, Sinoni, Arusha.
Sheikh Rajabu Kihungiza alitoa wito kwa vijana kuacha tabia ya kugombania mali za wazazi waliofariki dunia hadi kufikia hatua ya kuuza nyumba. Leyla ameacha mtoto mmoja, Tyrese Mtumwa (12).
Comments
Post a Comment