Skip to main content

Featured

Maombolezo: Hii ndiyo Hali Ilivyo Tanzania Bendera Yapepea Nusu Mringoti

Agizo la Rais John Magufuli la Bendera ya Taifa kupepea kwa nusu mlingoti kwa siku tatu kuanzia leo Septemba 22 kufuatia ajali ya kivuko cha MV Nyerere iliyotokea mkoani Mwanza limetekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Mwenyekiti wa tume ya Shellukindo atoa ya moyoni kero za Muungano




Mwaka 1992 hoja ya kero za Muungano ilipoendelea kupamba moto Serikali iliunda Tume ya Shellukindo iliyokuwa chini ya mbunge wa Bumbuli kwa wakati huo, William Shellukindo. Tume hiyo ilijumuisha wajumbe kutoka Serikali zote mbili. Serikali ya Zanzibar nayo iliunda Kamati ya Amina Salum Ali.
Tume ya Shellukindo ilichambua mambo yote ya Muungano na kutoa mapendekezo ya kuboresha utekelezaji. Lakini pia ilitoa mapendekezo ya baadhi ya mambo kuondolewa kwenye orodha ya mambo ya Muungano, kwa mfano bandari. Kwa upande mwingine Kamati ya Amina, pamoja na mambo mengine, ilipendekeza mambo kumi na mbili yaondolewe kwenye orodha ya mambo ya Muungano.
Septemba 27 mwaka 1994 tume hiyo ilipitishwa na Bunge kuanza rasmi kazi ya kushughulikia mambo ambayo ni vikwazo katika kutekeleza Muungano na Ilijulikana kwa jina la (Kamati ya Shellukindo ya kushuhgulikia vikwazo vinavyokwamisha kutekeleza Muungano).
Pia, tume hiyo ilibainisha kuwa kero kubwa ni mgawanyo wa mali na jinsi kila upande utakavyochangia kwenye Serikali ya Muungano. Tume hiyo ndiyo iliyozaa kamati ya pamoja ya fedha ya masuala ya Muungano.
Mwaka 2003, Rais Benjamini Mkapa aliunda Tume ya pamoja ya fedha iliyoitwa Tume ya Shellukindo , tume hii ilikuwa ni utekelezaji wa mambo yaliyoibuliwa na kamati ya Shellukindo iliyokuwa imeundwa na Rais Mwinyi. Tume hii ilifanya kazi kwa miaka mitano hadi mwaka 2007 ikioongozwa na William Shellukindo.
Tume hiyo ilifanya kazi kubwa ya kujifunza katika nchi mbalimbali duniani namna ya kugawana mali na kuchangia muungano ambapo walitoa utaratibu wa namna ya ukokotoaji wa mgawanyo na uchangiaji.
Mwaka 2008 Rais Jakaya Kikwete aliunda tume ya pili ya pamoja ya fedha ya Shellukindo iliyoendeleza kazi iliyoishia mwaka 2007 na ikamaliza muda wake mwaka 2013.
Kazi ya tume hiyo ilikuwa ni kuendeleza kazi ya kutafuta namna bora ya kugawana mali na kuchangia muungano, kazi waliyoifanya kwa miaka mitano na walitoa mapendekezo ambayo mpaka sasa hayajafanyiwa kazi.
Yafuatayo ni mahojiano kati ya mwandishi wa makala hii na Shellukindo.
Swali: Ulikuwa mwenyekiti wa tume ya kushughulikia kero za Muungano maarufu Kamati ya Shellukindo. Je, mapendekezo yaliyotolewa na tume yako yamefanyiwa kazi.
Jibu: Kwanza ifahamike kwamba kuundwa kwa tume ya pamoja ya fedha inayojulikana kama Tume ya Shellukindo ni matokeo ya mapendekezo ya tume ya jitihada za kuondoa mambo ambayo ni vikwazo katika kutekeleza Muungano nayo mwenyekiti wake nilikuwa mimi.
Kwa hivyo, Tume ya Shellukindo ya kutafuta jitihada za kuondoa vikwazo katika kutekeleza muungano iliundwa Mei 1992 na Rais wa awamu ya pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi na kujadiliwa kisha kupitishwa na Bunge Septemba 27 mwaka 1994.
Mwaka 2003,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa awamu ya tatu, Mheshimiwa Benjamin Mkapa aliunda tume hii inayoitwa ya Shellukindo ili iweze kufanyia kazi mapendekezo ya Kamati ya Shellukindo, tume ambayo ilifanya kwazi hadi mwaka 2008 na mwaka 2009 nikateuliwa tena kuiongoza nikiwa na baadhi ya wajumbe wa tume ya awali.
Wajumbe wa Tume ya Shellukindo iliyoundwa Machi 2003 hadi Machi 1 mwaka 2008 walikuwa Hamis Omari aliyekuwa makamu mwenyekiti, Balozi Charles Nyirabu kwa sasa ni marehemu, Dk Edmond Mndolwa, Dk Hawa Sinare, Amina Zidikheri na Simai Makame.
INAENDELEA UK 20
INATOKA UK 17
Tume ya pili niliyoiongoza kuanzia mwaka 2009 hadi 2013 iliundwa na Abdurahman Jumbe aliyekuwa Makamu Mwenyekiti na makamisha ni Khamis Omar, Othman .M .Othman, Edmond Mndolwa,
Dk Alhaji Juma Ngasongwa na Dk Pindi Chana na sasa ipo ya tatu ambayo baadhi ya wajumbe wa awamu ya pili walikuwemo.
Mapendekezo ya msingi ya Tume ya Shellukindo yalikuwa ni Suluhisho la kero za Muungano litapatikana pale Serikali itakapofanyia kazi kanuni “fomula” kwenye eneo la kugawana mapato na kuchangia gharama za Muungano, kama ilivyotolewa katika mapendekezo ya Tume ya pamoja ya fedha ijulikanayo kwa jina maarufu la “Tume ya Shellukindo”.
Fomula hiyo inapendekeza pande mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ziweke vigezo vya asilimia ya mgawanyo wake na ukokotolewe kulingana na raslimali na mapato yatokanayo na mambo ya muungano na siyo gawio la Benki Kuu.
Naamini kwamba kama mapendekezo hayo yangekuwa yamefikishwa kwa Rais John Magufuli, yangekuwa yameanza kufanyiwa kazi kwa sababu ni kiongozi mwenye nia ya dhati ya kuondoa mambo yanayosababisha nchi isisonge mbele.
Nimeamua kusema hayo kwa sababu kuna mkanganyiko kwani baadhi ya watu wanadhani mapendekezo ya Tume ya Shellukindo yameshafanyiwa kazi na wengi hawajui ni nini cha msingi kilichopendekezwa.Nimekaa na dukuduku la muda mrefu kuhusu suala hili, nahisi hawajamfikishia Rais Magufuli, leo nashukuru nimepata fursa ya kulisemea, tumefanya kazi hii kwa miaka 10, tumekwenda nchi 13 zenye muundo wa muungano na mashirikisho kujifunza, kote tumeambiwa kama hatutaweka fomula ya mgawanyo wa raslimali na mapato, manung’uniko hayatakwisha.
Hadi tulipokaa na Tume ya Jaji Joseph Warioba alipokuwa wakiwasilisha kwa Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete mapendekezo ya rasimu ya Katiba mpya mwaka 2014, mapendekezo ya vigezo vya fomula ya mgawanyo wa mapato yalikuwa hayajafanyiwa kazi,” alisema Shellukindo.
Ni jambo la kusikitisha kuona Tume ya Shellukindo iliundwa kisheria na tulilazimika kutembelea nchi 14 zenye muundo wa muungano au mashirikisho kujifunza zikiwa zimeteketea fedha nyingi za Serikali.
Nchi tulizo kwenda kujifunza ni Brazil, Thailand, India, Urusi, Ethiopia, Ujerumani, Canada, Uswis, Hispania, Nigeria, Australia, Denmak, Finland, Norway na Uingereza, huko kote tuliambiwa bayana kwamba kama hakutakuwa na vigezo vya fomula ya mgawanyo wa raslimali na gharama za mambo ya muungano migogoro itakuwepo tu. Nikupe mfano wa mfano wa nchi ya Nigeria ambayo ina shirikisho lenye majimbo 37 ambayo imeimarisha mambo 20 ambayo ni ya shirikisho na asilimia 13 ya mapato ya maliasili huenda kwenye jimbo linalozalisha. Vigezo vilivyotumika Nigeria kuweka mgawanyo wa mapato ya shirikisho
ni kwamba Serikali Kuu hupata asilimia 52.68, Serikali ya majimbo asilimia 26.72 wakati Serikali za mitaa hupata asilimia 20.60. Finland ambayo ni muungano wa nchi mbili yaani kisiwa cha Aland na Finland, alisema walikuta uwiano wa mgawanyo wa mapato na gharama za muungano unafurahiwa na pande zote.
Swali: Unadhani mgogoro wa Muungano bado upo?
Jibu: Mgogoro upo hili si jambo la kuuliza, kila mtu amesikia mzozo wa Wazanzibari kugoma mafuta yanayodaiwa kugunduliwa baharini upande wao yasiwekwe kwenye orodha ya raslimali za muungano. Hili si jambo dogo.
Swali: Unadhani bado upo umuhimu wa kupeperushwa bendera ya Zanzibar wimbo wa Taifa hilo?
Jibu: Zanzibar wana wimbo wa Serikali za Mapinduzi (SMZ) na siyo wimbo wa Taifa kwa sababu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina wimbo mmoja tu wa Taifa.
Sioni tatizo kwa Zanzibar kupeperusha bendera na kuimba wimbo kwa sababu unaitambulisha Serikali ya SMZ, lakini kama wanauita ni wimbo wa Taifa basi hilo ni tatizo kwa sababu Taifa la Tanzania lina bendera moja tu na wimbo wa taifa mmoja.
Swali: Una maoni gani kuhusiana na hali ya kisiasa inavyoendelea nchini hususani kuzuiwa mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, utekaji na mauaji?
Jibu: Uelewa wa wananchi kuhusu siasa umekuwa mkubwa ikilinganishwa na siku za nyuma, hivi sasa hadi vijiji wanajua nini kinaendelea. Sioni tatizo kwa watumishi wa Mungu kuzungumzia siasa kwa sababu huwezi kutenganisha dini na siasa, lakini linakuwa tatizo pale viongozi wa dini wanapoingilia masuala ya kiserikali na kuegemea chamafulani kwa maslahi yasiyo ya Taifa.
Kuhusu mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa naona ni vyema Serikali iachwe itekeleze maendeleo ya wananchi isipokuwa kuna mbegu mbaya iliyoanza kuoteshwa ya kubaguana kwa itikadi za kisiasa. Hii italeta madhara makubwa siku za usoni kama itaendelea.
utulity
Tume/Kamati zilizoundwa kuangalia kero za Muungano
Kamati ya Mtei
Tume ya Jaji Francis Nyalali (1991)
Kamati ya Shellukindo (1994)
Kamati ya Shellukindo 2 ya kuandaa Muafaka juu ya Mambo ya Muungano baina ya SMZ na SMT.
Kamati ya Jaji Mark Bomani (1995)
Kamati ya Jaji Robert Kisanga (1998)
Kamati ya ‘Harmonization’
Kamati ya Masuala ya Simu (Kamati ya Kusila)
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) nayo kwa upande wake iliunda Kamati zifuatazo kwa madhumuni hayo hayo:
Kamati ya Baraza la Mapinduzi (Kamati ya Amina) ya 1992
Kamati ya Rais ya Kupambana na Kasoro za Muungano (Kamati ya Shamuhuna) ya 1997
Kamati ya Rais Kuchambua Ripoti ya Jaji Kisanga (Kamati ya Salim Juma Othman)
Kamati ya Kuandaa Mapendekezo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar juu ya Kero za Muungano (Kamati ya Ramia) ya 2000
Kamati ya Baraza la Mapinduzi juu ya Sera ya Mambo ya Nje
Kamati ya Rais ya Wataalamu juu ya Kero za Muungano ya 2001
Kamati ya Baraza la Mapinduzi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki
Kamati ya Mafuta
Kamati ya Madeni baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Muungano wa Tanzania
Kamati ya Suala la Exclusive Economic Zone (EEZ)
Kamati ya Masuala ya Fedha na Benki Kuu
Kamati ya Rais ya Masuala ya Simu (1996 –1999)
Kamati ya Baraza la Mapinduzi juu ya matatizo na kero za Muungano na taratibu za kuyaondoa (2004)

Comments

Popular Posts