Skip to main content

Featured

Maombolezo: Hii ndiyo Hali Ilivyo Tanzania Bendera Yapepea Nusu Mringoti

Agizo la Rais John Magufuli la Bendera ya Taifa kupepea kwa nusu mlingoti kwa siku tatu kuanzia leo Septemba 22 kufuatia ajali ya kivuko cha MV Nyerere iliyotokea mkoani Mwanza limetekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.

NFRA kuongezewa uwezo

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa leo anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa kuongeza uwezo wa uhifadhi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula(NFRA) mjini Dodoma.
Hafla hiyo itafanyika kwenye viwanja vya ofisi za Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula zilizopo Mtaa wa Kizota eneo la Viwanda katika Manispaa ya Dodoma.
Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa NFRA, Vumilia Zikankuba, amesema, mradi huo utagharimu dola za Marekani milioni 55, ambao ni mkopo wa masharti nafuu kutoka serikali ya Poland, ikiwa ni sehemu ya kiasi cha dola za Marekani milioni 110 kilichotolewa kwa serikali ya Tanzania.
Zikankuba alieleza kuwa mikataba ya ujenzi ilianza kutekelewa Desemba 9, 2017, mradi huo utatekelezwa na kampuni mbili za kandarasi kutoka Poland ambazo ni Feerum S.A na Unia Araj Realizacje Sp.o.o, huku msimamizi wa mradi ni Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).
“Mradi utahusisha ujenzi wa vihenge vya kisasa, maghala ya kisasa, ujenzi wa ofisi na kutekelezwa katika maeneo nane ambayo ni Babati – Manyara, Dodoma, Makambako – Njombe, Mbozi – Songwe, Shinyanga, Songea –Ruvuma, Sumbawanga – Rukwa na Mpanda – Katavi,” amesema.
Alisema baada ya mradi kukamilika, wakala utakuwa umeongeza uwezo wa kuhifadhi kwa tani za ujazo 250,000 zaidi (vihenge vya kisasa tani za ujazo 190,000 na maghala 60,000), jambo ambalo litakuwa chachu na mafanikio yenye tija.
Hifadhi ya chakula inayohitajika kukidhi mahitaji ya dharura kwa miezi mitatu ni zaidi ya tani 500,000 ukilinganisha na tani 150,000 iliyokuwa inahitajika miaka ya 2008 NFRA ilipoanzishwa.
Aidha, teknolojia itakayotumika katika ujenzi wa vihenge vya kisasa, itawezesha wakala kupunguza gharama za uendeshaji; kuhifadhi chakula kwa muda mrefu zaidi; kupunguza upotevu wa zao la mahindi baada ya kuvuna.

Comments