TEMBO watatu wamemvamia kikongwe, Sixbertha Mtundu (88), mkazi wa kitongoji cha Mbuyuni mtaa wa Ihanga, kata ya Rujewa wilayani Mbarali na kumjeruhi na hatimaye kumsababishia kifo.
Akizungumzia tukio hilo, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Rujewa wilayani Mbarali, John Mpangala alisema lilitokea Aprili 20, mwaka huu saa 11 za jioni maeneo yaliyopo jirani na Ikulu ndogo ya wilaya ya Mbarali kwenye mashamba yaliyo na mimea ya mahindi, karanga na alizeti.
Mpangala amesema, kikongwe huyo alivamiwa na tembo hao wakati akitokea shambani kwake na inasadikika kutokana na umri wake mkubwa huenda hakuwaona wanyama hao mapema na pia alishindwa kukimbia baada ya kuvamiwa.
Ofisa Mtendaji huyo alisema tukio hilo liligunduliwa na msamaria mwema aliyepita eneo hilo na kukuta kikongwe huyo akiwa amelala njiani huku amejeruhiwa vibaya kwa kukanyagwa na tembo na ndipo alikwenda kwa mwenyekiti wa kitongoji na kumjulisha na wakaenda eneo husika ikiwa ni majira ya saa moja na nusu usiku lakini wakakuta amekufa.
"Mwenyekiti alichokifanya ni kumpigia mkuu wa kituo cha polisi ambaye alikwenda eneo husika akiwa na askari na ndipo waliuchukua mwili na baadaye kuupeleka Hospitali ya Wilaya iliyopo mjini Rujewa,” amesema Mpangala na kuongeza:
"Wapo watu wengine ambao walikuwa wamewaona tembo hao wakiwa watatu na miongoni mwao ni mwenyekiti wa kitongoji hicho hicho. Wananchi wengine waliopo jirani na kata ya Mawindi waliowaona tembo hao wakiendelea na safari wakati wao wanavuna karanga lakini wao walitulia na tembo wakapita."
Ofisa Mtendaji huyo alisema eneo la tukio kwa miaka ya nyuma ilikuwa njia (Shoroba) ya wanyama lakini baada ya shughuli mbalimbali za kibinadamu hususani kilimo na makazi kukithiri wanyama hawakuendelea kupita tena.
Comments
Post a Comment