MSAJILI wa Vyama vya Siasa nchini ameagizwa atoe muda wa mwezi mmoja kwa vyama vyote vya siasa nchini vilivyosajiliwa, viwasilishe taarifa za hesabu zao ili chama kitakachobainika kuwa na upungufu na kile kisichowasilisha taarifa zake hizo kwa mujibu wa sheria, kichukuliwe hatua stahiki.
Moja ya adhabu kwa mujibu wa sheria ya vyama vingi endapo chama kitashindwa kuwasilisha kwa msajili taarifa zake za hesabu zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) au kuwa na mapungufu ni pamoja na kusitishiwa ruzuku au kushtakiwa.
Katika ripoti hiyo ya CAG, imeonesha chama cha Chadema kilichowasilisha ripoti yake kwa ukaguzi, hesabu zake zinaongoza kuwa na upungufu ikiwemo kuwepo kwa malipo yasiyo na nyaraka au nyaraka zenye upungufu.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hoja zilizobainishwa katika ripoti ya CAG zinazogusa wizara yake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama alisema katika ripoti hiyo imebaini kuwa vyama vya siasa takribani tisa kati ya 19 havijawasilisha ripoti zake za hesabu kwa CAG ili ziweze kukaguliwa.
"Katika mwaka unaoishia Juni mwaka jana, ripoti ya CAG inaonesha ni vyama 10 tu kati ya 19 vilivyosajiliwa ndio vimewasilisha taarifa zao za hesabu kwa CAG, baadhi ya vyama hivyo ni CCM, SAU, Chadema, NLD, DP, CCJ, ADC, AFP na Demokrasia Makini," amesema Mhagama.
Amesema kati ya vyama hivyo vitatu ambavyo ni CCM, Chadema na NLD ndio vinavyopata ruzuku. Vyama tisa ambavyo havijawasilisha taarifa zake za hesabu kwa CAG baadhi yake ni Chama cha Wananchi (CUF), UPDP, NCCR-Mageuzi, NARA, ACT-Wazalendo na UMD. Kati yao CUF, NCCR na UDP vinapata ruzuku ya Serikali.
"Ripoti hii ya CAG inaonesha kuwa vyama hivi vya siasa vinazidi kutoiheshimu Sheria ya Vyama vingi ambapo miaka ya nyuma ni vyama vine tu ndio havikuwasilisha taaifa zake za hesabu kwa CAG lakini mwaka huu vimepanda na kufikia tisa," alisema.
Akielezea mapungufu yaliyobainishwa na ripoti hiyo ya CAG kwa vyama vilivyowasilisha taarifa ya hesabu zake, Waziri Mhagama, alisema baadhi ya vyama kama vile SAU, CCJ na AFP hesabu zake zilikuwa chini ya viwango, muundo wa hesabu haukuwa sawa na hesabu kutofautiana.
Amesema baadhi ya vyama kama vile Chadema, NLD na Demokrasia Makini viliwasilisha hesabu zao bila kuwa na rejista za mali zao za kudumu jambo ambalo ni kinyume cha sheria ya vyama vya siasa.
Alisema pia baadhi ya vyama hivyo havikuwa na usuluhishi wa fedha wa kibenki jambo ambalo ni takwa la kisheria.
Pia vingine vikiwemo Chadema, SAU na ADC vilikuwa na mapungufu katika malipo yenye nyaraka ya zaidi ya Sh milioni 735.9.
"Katika ripoti hii Chadema iliongoza kwa kuwa na malipo yasiyo na nyaraka au kuwa na nyaraka zenye mapungufu. Pia ilikuwa na masurufu yasiyorejeshwa yenye thamani ya kiasi cha Sh milioni 400," amesema.
Alieleza kuwa pia ripoti hiyo ya CAG ilibaini kuwa chama cha Chadema kilikuwa na mkopo wa mwaka 2014/15 wa Sh milioni 158.8 uliorejeshwa bila nyaraka iliyothibitisha uhalali wa malipo pamoja na mkopo mwingine wa Sh bilioni mbili uliorejeshwa bila nyaraka hiyo muhimu.
Aidha, alisema pia chama hicho cha Chadema kilionekana hesabu zake zina malipo ya tax invoice yenye thamani ya Sh milioni 866.6 zilizolipwa kwa ajili ya mabango, pia Sh milioni 715 zililipwa kwa mwanachama kama fedha iliyokopwa kwa ununuzi wa mabango bila nyaraka.
"Kulikuwa pia na makusanyo ya Sh bilioni 2.3 yaliyolipwa kinyume cha Sheria ya chama hicho cha Chadema. Yapo manunuzi ya bilioni 2.1 yaliyofanyika bila ushindani," amesema.
Kwa upande wa CCM alisema ripoti hiyo ilibaini uwepo wa Sh milioni 33.1 zilizohamishwa kutoka kwenye akaunti ya pensheni kwenda kwa Katibu Mkuu pamoja na uwepo wa mikopo iliyowekezwa kwenye kampuni kadhaa kama vile Uhuru na TOT ambayo haioneshi faida.
Alitaja hatua ambazo msajili wa siasa anaweza kuchukulia chama endapo kitabainika kwenda kinyume cha Sheria ya Vyama vya Siasa, ni kusitisha ruzuku ya serikali kwa chama kilichokiuka kuwasilisha maelezo ya matumizi ya fedha hiyo na kiasi cha fedha kuondolewa kwenye ruzuku kama hakina maelezo.
Comments
Post a Comment