Kwa mujibu wa Sumatra, jiji hilo lina daladala zipatazo 10,154 na kutokana na upotevu wa tripu mbili kwa foleni, daladala moja ndogo inakadiriwa kupoteza Sh 40,000 kwa siku wakati kubwa hupoteza Sh 150,000. Maana yake ni kwamba kuna wastani wa Sh 80,000 ambazo hupotea kwa siku kwa kila daladala.
Hii inamaanisha kwamba endapo daladala zote 10,154 zitabeba abiria kwa siku katika jiji hilo, wastani wa mapato ya Sh800 milioni yatapotea kwa siku katika usafiri huo.
Vibonge husota zaidi vituoni
Kondakta wa Tegeta Nyuki-Ubungo, Barante Thomas anasema kutokana na changamoto ya foleni inayosababisha kupungua kwa ruti zake, imesababisha makondakta na madereva wengi kuwa na uchaguzi wa abiria wakati wa abiria wengi asubuhi na jioni.
Thomas anasema hukwepa abiria mnene asubuhi kwa sababu anachukua nafasi kubwa ndani ya daladala. Mbali na hilo, anasema watu wanene hususani wanawake wamekuwa si ‘shapu’ kujipanga ndani ya daladala.
“Si mimi tu kila konda huwa anaangalia sana mtu mnene, afadhali nichukue wembamba watatu nitawapanga vizuri kuliko mmoja mnene, ni hasara kwenye hesabu yangu,” anasema.
Anasema hatua hiyo hujitokeza zaidi katika mazingira ya kuchukua abiria vituoni baada ya daladala kuondoka kituo kikubwa cha Tegeta Nyuki. Anasema hulazimika pia kupanga abiria watatu hadi wanne katika ngazi moja ya mlango pamoja na kuchagua abiria wembamba.
Pamoja na usafiri wa daladala, kuna usafiri wa treni mbili za Mwakyembe usiotosheleza. Pia kuna usafiri wa kukodi kama taksi, Uber na bodaboda ambao hautumiki kwa wakazi wengi wa Dar.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), makadirio ya idadi ya watu jijini Dar es Salaam hadi Desemba mwaka jana ilikuwa ni milioni 5.7 lakini idadi hiyo inatajwa kukua kwa kasi huku usafiri wa daladala ukitumika zaidi.
Profesa wa uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Humphrey Moshi anasema muda unaopotea umeathiri kiwango cha ufanisi wa kazi na kuathiri mchango wake katika Pato la Taifa (GDP).
Kwa mujibu wa ripoti ya NBS, mchango wa jiji la Dar es Salaam katika GDP kwa mwaka 2016 ilikuwa ni asilimia 17.02 na mchango huo unaonekana kukua tangu mwaka 2007.
Anasema zipo tafiti zinazoonyesha jiji la Dar kupoteza Sh4 bilioni kwa siku kutokana na foleni. “Kwa tatizo la muda unaopotea, inawezekana mtumiaji usafiri huo anatumia saa nne tu badala ya nane kufanya kazi, kwa mantiki hiyo productivity (uzalishaji) inapungua, inapelekea hata kiwango cha GDP kilichotarajiwa kukosekana, kiwango hicho (asilimia 17) ni kidogo kwa shughuli za jiji hilo,” anasema Profesa Moshi.
Profesa Moshi pia anasema athari zinazojitokeza ni kubwa kuliko gharama za kuwekeza miradi ya kuondoa foleni. Anasema Serikali inatakiwa kuwa na mipango ya mudda mrefu katika miradi ya miundombinu kutokana na kasi ya ukuaji wa jiji.
Mwaka 2040 wakazi Dar huenda wakafikia hadi 12 milioni, kama inavyoelezwa katika utafiti wa Februari mwaka huu wa wataalamu wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (Jica).
“Kwanza Plan ya zamani ilivurugwa kwa watu kujenga holela, lakini hata kwa sasa Plan bado ina shida, barabara ya njia mbili iliyojengwa na Mwalimu Julius Nyerere, haiwezekani tena leo kujenga njia mbili, lazima tuwe na Plan ya miaka 50 mbele, mfano barabara ya Bagamoyo hakukuwa na sababu ya kujenga njia mbili ila ilitakiwa njia nne kutokana na kasi ya ukuaji wa jiji,”anasema Profesa Moshi.
Gazeti hili limefanya mahojiano na baadhi ya madereva wa usafiri huo walioomba kuhifadhiwa majina yao. Dereva wa mwendokasi wa Kimara-Kivukoni anasema katika njia hiyo wamepangiwa kutumia dakika 35 tu lakini kutokana na matumizi ya trafiki amekuwa akitumia wastani wa dakika 45.
“Si peke yangu tu, hata wewe unaweza kuwa shahidi wakati mwingine unakuta mwendokasi zimepanga foleni ndefu pale Ubungo, kutokana na mazingira hayo inabidi niende kwa kasi na wakati mwingine nipitilize kituoni bila kusimama ili kufidia muda uliopotea kwenye foleni,” anasema.
Kuhusu mahitaji ya usafiri anasema bado ni makubwa, abiria ni wengi asubuhi: “Mimi basi langu linatakiwa kubeba abiria 80 lakini ninabeba 200 hadi 250 na abiria anasubiri zaidi ya dakika 30 kituoni, kwa hiyo ile maana ya mwendokasi inapotea, anakuwa ametumia wastani wa dakika 70 kufika ofisini kwake,” anasema.
Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (Dart) ulianza Mei 10, 2016. Novemba mwaka jana Mtendaji Mkuu wa Dart, Ronald Lwakatare anasema wanatarajia kuongeza mabasi kutoka 140 ya sasa hadi 305 awamu ya kwanza ya mfumo huo itakapokamilika Juni mwakani.
Lwakatare anasema ongezeko la mabasi litasaidia kuongeza idadi ya abiria kutoka 200,000 wanaohudumiwa sasa kwa siku hadi kati ya 400,000 na 500,000.
Mradi huo hutoa huduma katika njia nane, vituo vikuu vitano, vituo vidogo 28 kwa kutumia mabasi 140 na hujumuisha mabasi makubwa 39 yenye uwezo wa kubeba abiria 160 kila moja na mabasi madogo 101 yenye uwezo wa kubeba abiria 60 kila moja.
Mhandisi Rwakatare anasema katika mabasi 165 yatakayonunuliwa na Serikali, yatahudumia vituo vya Morocco, Tegeta, Masaki, Makumbusho na maeneo mengine ambayo hayajafikiwa na huduma hiyo.
Mmoja kati ya madereva wa basi dogo anasema kwa siku hubeba abiria wastani wa 120 na huzunguka wastani wa ruti 14 lakini abiria wengi hutumia muda mwingi kituoni hasa asubuhi na jioni.
Katika kukabiliana na tatizo hilo, Sumatra imeanzisha njia mpya zaidi ya 59 huku ikiongeza urefu wa ruti katika njia 82 ndani ya miezi sita iliyopita.
Kutokana na kasi ya ukuaji wa jiji, Mkurugenzi wa Sumatra, Johansen Kahatano anasema mamlaka hiyo imezuia magari madogo kuingia katikati ya jiji tangu Aprili mwaka jana na kuruhusu makubwa ili kupanua huduma katika njia zenye changamoto.
“Magari yote yenye abiria chini ya 40 tumeyazuia katikati ya mji, imetusaidia hata wenye magari mapya kuomba njia zenye changamoto,”anasema Kahatano.
Hatua ya tatu ni kuongeza urefu wa njia za daladala kuanza ruti za mbali ili kupunguza mrundikano wa abiria wanaosubiri usafiri muda mrefu vituoni.
“Kwa mfano, njia ya Buguruni- Muhimbili ilikuwa fupi lakini sasa zinakwenda hadi Gongo la Mboto, Tabata, abiria waliopanda mabasi mawili wamepungua sana , wanapanda basi moja,” anasema.
Januari mwaka huu Sumatra imeanzisha njia mpya za daladala zitakazoanzia Mbezi Luis au Kibamba Shule kwenda Makumbusho au Kawe kupitia Barabara ya Morogoro na kurudi Mbezi au Kibamba Shule kupitia Goba.
Hali katika jiji hilo, wakazi hutumia huduma ya usafiri wa treni, mabasi yaendayo haraka na daladala lakini Sumatra inakiri mahitaji bado makubwa.
Kahatano anataja njia tano zinazohitajika ili kupunguza msongamano wa foleni Dar ambazo ni kuanzisha miundombinu ya reli ya kisasa kwa treni za huduma ya usafiri wa umma, kuimarisha mfumo wa huduma ya usarifi wa mabasi yaendayo haraka na kuanzisha mradi wa treni za chini ya ardhi.
Februari mwaka huu, Serikali ilisema itakamilisha upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa barabara saba za juu (flyover) maeneo ya barabara za Chang’ombe, Uhasibu, Mwenge, Morroco, Kamata, Magomeni na Tabata ili kupunguza foleni katika jiji hilo.
Kahatano anasema njia nyingine ni kubadili utamaduni wa kutumia magari binafsi na kutumia usafiri wa umma.
“Kuwepo na mfumo ambao mtu akiwa nyumbani anaweza kutumia simu yake kujua basi lipo wapi, litafika kituoni saa ngapi, nafasi ya siti ipo aweze kufanya ‘booking’ kabla,” anasema.
Njia ya tatu ni kuondoa mrundikano wa huduma muhimu katika sehemu moja na kuzielekeza sehemu mbalimbali za jiji zikiwamo wizara, mabenki na ofisi nyingine kupitia Mipango Miji ya kisasa.
Mbali na hilo, pia Serikali inatakiwa idhibiti uagizaji magari binafsi kwa kiwango cha hali ya juu, ikiwamo kuongeza kiwango cha kodi.
Kahatano anasema ni muhimu pia kuanzisha mfumo wa utambuzi wa maegesho ya kisasa kupitia teknolojia itakayomsaidia dereva kujua wapi kuna eneo la kuegesha gari kabla ya kuingia katikati ya jiji.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi Madereva Tanzania (Tudo), Abdallah Lubala anasema sheria zinatakiwa kuwa kali ili kudhibiti maegesho yasiyofuata taratibu barabarani, kudhibiti madereva wasiokuwa na sifa. Pia, kupunguza matumizi ya trafiki na kupunguza ukaguzi unaosababisha foleni.
Comments
Post a Comment