Katibu wa itikadi, uenezi na mawasiliano ya Umma Chama cha ACT-Wazalendo, Ado Shaibu akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana baada ya kupitia kauli, miongozo na taarifa za Serikali zilizotolewa hivi karibuni.
Dar es Salaam. Uongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo umeendelea kuishinikiza Serikali kuipa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) tozo za mauzo ya nje za korosho zinazouzwa nje, ili iweze kusimamia zao hilo.
Akizungumza jana, katibu wa uenezi na mawasiliano ya umma, Ado Shaibu alisema madhara ya kuchelewesha fedha hizo ni makubwa kwa sekta ya korosho.
Shaibu alisema asilimia 65 ya tozo hizo huingizwa kwenye mfuko wa bodi ya korosho kwa ajili ya kugharamia uendeshaji wa zao hilo, lakini kwa miaka miwili Serikali haijatoa fedha hizo.
Alisema madhara ya kuchelewesha fedha hizo ni kupanda maradufu kwa bei ya pembejeo.
“Bei ya pembejeo ya salfa kwenye maeneo mengi imepanda kutoka Sh16,000 hadi Sh70,000,” alisema Shaibu.
Alisema kupanda kwa bei kunatokana na ununuzi wa pembejeo nje ya nchi kutegemea kwa asilimia 100 kutoka katika tozo hizo.
“Kama Serikali haiipi bodi ya korosho tozo hizo kwa wakati, gharama za uzalishaji kwa wakulima zinaendelea kuwa kubwa,” alisema.
Alisema kituo cha Utafiti Naliendele kinategemea fedha kwa asilimia 90 kujiendesha na kwamba, kisipopata kitashindwa kufanya kazi ikiwamo kutafiti.
Katibu huyo alisema mafunzo ya kilimo bora cha korosho kwa wakulima na maofisa ugani hutegemea tozo hizo kwa asilimia 100.
Pia, alisema mfumo wa stakabadhi ghalani hutegemea fedha kutoka katika tozo hiyo.
Shaibu alisema uchaguzi wa viongozi wa kitaifa wa chama hicho utafanyika katika mkutano mkuu wa chama hicho utakaofanyika jijini Mbeya kuanzia Agosti 25 hadi 27.
Alisema uchaguzi huo utafanyika baada ya kukamilika ule wa ngazi ya chini unaoendelea.
Alisema chama hicho kinataka kukamilisha uchaguzi huo ili kujiandaa na uchaguzi wa Serikali unaokuja.
Aliwataka wanachama wenye sifa kugombea nafasi za kitaifa ili wakitumikie chama hicho katika nafasi za uongozi.
Alizitaja baadhi ya nafasi za kitaifa zitakazowaniwa na wanachama katika uchaguzi huo kuwa ni kiongozi wa chama, mwenyekiti, makamu mwenyekiti na katibu mkuu.
Comments
Post a Comment