Skip to main content

Featured

Maombolezo: Hii ndiyo Hali Ilivyo Tanzania Bendera Yapepea Nusu Mringoti

Agizo la Rais John Magufuli la Bendera ya Taifa kupepea kwa nusu mlingoti kwa siku tatu kuanzia leo Septemba 22 kufuatia ajali ya kivuko cha MV Nyerere iliyotokea mkoani Mwanza limetekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Bunge latishia kumfunga jela Mugabe



Bunge la Zimbabwe limetishia kumshtaki rais wa zamani Robert Mugabe kwa kudharau wito ikiwa hatakwenda tena kwenye kikao cha kusikiliza mapato ya madini ya almasi yanayofikia dola za Marekani 15 bilioni yalivyopotea enzi za utawala wake.
Mugabe, 94, alishindwa kuhudhuria kikao cha Jumatatu kilichoitishwa na Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ili aweze kutoa ufafanuzi juu ya madai ya upotevu wa kiasi hicho cha fedha mwaka 2016.
Hiyo ilikuwa mara ya pili kwa Mugabe kutofika mbele ya watungasheria hali iliyosababisha wajumbe wa kamati hiyo kukasirishwa na wakatoa amri kwamba lazima afike kujieleza Juni 11 au ashtakiwe kwa kosa la kudharau Bunge na kujiweka katika uwezekano wa kufungwa jela.
"Tunatarajia kwamba atapata muda wa kufika bungeni. Tunamtarajia atoe ushirikiano na Bunge lina mamlaka ya kumwita,” alisema mwenyekiti wa kamati hiyo Temba Mliswa mbele ya wanahabari Jumatatu jijini Harare.
Aliongeza: "Barua tunayomwandikia, ambayo itakuwa ya mwisho ni ya kumkumbusha kuwa sasa itabidi tumwite kwa samansi na sisi tunadhani tusifike kiwango cha kumwita hivyo rais mstaafu.”
"Hebu nikukumbushe kwamba aliyekuwa mbunge hayati Roy Bennett alifungwa jela na Bunge. Kwa hiyo tunapenda uweke moyoni juu ya mamlaka ambayo Bunge linayo,"alisema Mliswa.
Katika sherehe fupi za kuzaliwa kwake alipotimia miaka 92 mwaka 2016, Mugabe aliliambia shirika la utangazaji la Zimbabwe kwamba taifa lilipoteza dola 15 bilioni kutokana na mapato ya almasi kuvuja, jambo lililosababisha aamue kutaifisha medani hiyo.
Mugabe aliyetawala Zimbabwe kwa karibu miaka 38 aliondolewa kwa nguvu Novemba mwaka jana baada ya kusalimu amri kutokana na shinikizo la jeshi.
Tangu alipoondolewa amekuwa haonekani hadharani na alizungumza mara moja na vyombo vya habari mapema mwaka huu alipomshutumu aliyekuwa makamu wake na sasa Rais Emmerson Mnangagwa kwa kumwondoa madarakani kinyume cha katiba.
Katika hatua nyingine serikali imetangaza kwamba uchaguzi mkuu wa Zimbabwe utafanyika Julai 30.

Comments

Popular Posts