Naibu Spika, Dk Tulia Ackson
Dodoma. Naibu Spika, Dk Tulia Ackson amesema mvutano wa mazishi ya aliyekuwa mbunge wa Buyungu (Chadema), Kasuku Bilago usiwavuruge, kwamba Bunge haliwezi kupoka madaraka ya familia ya marehemu na chama chake.
Dk Tulia ametoa kauli hiyo leo Jumanne Mei 29, 2018 katika viwanja vya Bunge mjini hapa wakati akitoa salamu za chombo hicho cha Dola katika misa ya kumuaga mbunge huyo.
Amesema kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe atakutana na Spika mkoani Kigoma na watalijadili jambo hilo na kufikia muafaka.
Akizungumzia mvutano huo, amesema umetokana na kikao kilichofanyika Jumapili iliyopita ambapo kiongozi wa upinzani alituma mwakilishi, kubainisha kuwa alikuta kikao kingine cha familia jijini Dar es Salaam huku akisisitiza kuwa hakuna jambo lililoharibika.
Akizungumza katika viwanja hivyo na kutoa salamu za upinzani, Mbowe amesema kumekuwa na mvutano usiokuwa na maana kuhusu mazishi ya Bilago
Amelitaka Bunge kutopoka madaraka ya familia kwa kutaka mazishi yafanyike kesho Jumatano wakati familia inataka mazishi yafanyike Alhamisi.
"Tunatoa ratiba hii na wenzetu wanatoa hivi, tumepeana mikono ya amani hapa kwa hiyo amani hiyo isiwe ya kinafiki naomba tushikamane,"amesema Mbowe.
Amesema mbali na takwa la familia, mbunge huyo alikuwa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Magharibi, mjumbe wa kamati kuu ya Chadema, hivyo wananchi na viongozi wenzake wanatakiwa kumuaga.
Amesema ndani ya Bunge hakuna umoja badala yake kuna mivutano ambayo wakati mwingine huumiza lakini katika misiba wanakuwa wamoja.
Bilago alifariki dunia Jumamosi iliyopita katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Comments
Post a Comment