Dar es Salaam. Mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba anastaafu rasmi nafasi hiyo baada ya kuitumikia kwa miaka 22.
Dk Bisimba anastaafu rasmi wadhifa huo Juni 30 akiacha rekodi na historia katika taasisi hiyo inayojishughulisha na masuala ya haki za binadamu.
Tayari LHRC imemteua Anna Henga kuwa mkurugenzi mpya wa kituo hicho, na ataanza rasmi majukumu yake ifikapo Julai Mosi.
Akizungumza na Mwananchi jana, Dk Bisimba alikumbuka mambo makubwa aliyoyafanya wakati wa uongozi wake, ikiwamo kusaidia kutatua mgomo wa madaktari mwaka 2012.
“Mwaka 2012 niliumizwa sana na hali hii, tulikuwa tunapambana kuhakikisha mgogoro unaisha, lakini Serikali iliamini tunauchochea na raia waliamini hivyo wakidhani tunafurahia watu kufa.
“Kibaya zaidi tulifanikiwa kuomba mkutano na waziri wa Afya wakati ule wenye lengo la kuwakutanisha na madaktari waliogoma, tukatafuta na watu wenye hekima kama viongozi wa dini, lakini baadaye wizara ikaghairi na kusema hao madaktari warudi tu kazini,” alisema Dk Bisimba.
Tukio jingine lililomuumiza ni lile la kushindwa kuwasaidia watoto watatu wa Kimasai waliokuwa wakikimbia kukeketwa.
Alisema watoto hao walikwenda kanisani, polisi, kwa mkuu wa mkoa na wilaya (ambao hakuwataja) kwa siku 19 wakitafuta msaada, lakini hakuna aliyewasaidia na mwisho walikamatwa na kurudishwa kwa baba yao wakakeketwa na kuozeshwa.
“Tulikuja kupata taarifa wakiwa tayari wameshakeketwa na kuozeshwa, mmoja wao aliolewa mke wa 11 akiwa na miaka 13 iliniuma sana,” alisema Dk Bisimba.
Alilitaja jambo analojivunia kuwa ni watu kutambua nini maana ya neno haki. “Hapo awali watu walikuwa hawaelewi neno haki, tulipokuwa tunaanza ukimwambia mtu haki yako hafahamu unamaanisha nini, lakini kwa uelewa uliopo sasa najivunia sana,” alisema.
Alisema aliomba kuondoka kwenye nafasi hiyo tangu aliporudi kutoka masomoni mwaka 2011, lakini alibaki kutokana na maombi ya bodi ya kituo hicho.
Comments
Post a Comment