Wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF) wakiwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam jana kusikiliza kesi inayohusu chama hicho. Picha na Said Khamis
Dar es Salaam. Mahakama Kuu imemzuia msajili wa vyama vya siasa kutoa ruzuku kwa CUF kutokana na mgogoro wa uongozi ndani ya chama hicho hadi kesi zote zilizofunguliwa zitakapotolewa uamuzi.
Wakati uamuzi huo ukitolewa, tayari kesi nyingine imefunguliwa ikipinga kuandaliwa uchaguzi mkuu.
Jaji Wilfred Dyansobera alitoa uamuzi wa kuzuia ruzuku jana kutokana na maombi ya zuio yaliyofunguliwa na chama hicho kambi ya katibu mkuu, Seif Sharrif Hamad.
CUF imekuwa katika mgogoro wa kiuongozi tangu Septemba, 2016 baada ya mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba anayetambuliwa na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kubadilisha uamuzi wa kujiuzulu wadhifa huo aliouchukua Agosti 2015.
Takriban mashauri 20 yamefunguliwa mahakamani na kambi hizo mbili, moja ikimuunga mkono Profesa Lipumba na nyingine Maalim Seif.
Kutokana na mgogoro huo, msajili aliiandikia barua CUF kuijulisha kuwa hatatoa ruzuku hadi utakapomalizika.
Hata hivyo, alitoa ruzuku kwa chama hicho upande wa Profesa Lipumba, jambo ambalo lilifanya kambi ya Maalim Seif kufungua maombi ya zuio mahakamani.
Maombi hayo namba 80 ya mwaka 2017 yalifunguliwa na bodi ya wadhamini ya CUF iliyoteuliwa na Maalim Seif dhidi ya msajili wa vyama vya siasa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Waombaji katika kiapo cha Maalim Seif, kilichounga mkono maombi hayo waliiomba mahakama itoe zuio kwa msajili kutoa ruzuku ya Serikali kwa CUF hadi kesi zote za chama hicho zitakapokwisha. Katika uamuzi wa jana, Jaji Dyansobera alikubali maombi hayo baada ya kuridhika kwamba mwaka 2016 msajili aliandika barua kwenda kwa chama hicho akieleza uamuzi wa kuzuia ruzuku kwa CUF. Katika barua hiyo iliyoambatanishwa katika maombi kama kielelezo, msajili alieleza ruzuku ni fedha za Serikali na haiwezi kukipatia chama ambacho kina mgogoro.
Jaji Dyansobera alieleza kushangazwa na kitendo cha msajili kuamua kutoa ruzuku wakati mgogoro haujaisha, huku mahakamani kukiwa na kesi nyingi ambazo hazijatolewa uamuzi.
“Ni busara kwamba fedha za ruzuku ambazo ni za Serikali, ambazo kimsingi ni fedha za umma zizuiwe ili kutoa nafasi ya kutatua mgogoro huu,” alisema Jaji Dyansobera.
Kabla ya uamuzi wa jana, Jaji Dyansobera alitupilia mbali hoja ya pingamizi la awali la AG aliyeomba mahakama iyatupilie mbali maombi hayo bila kuyasikiliza.
Mwanasheria mkuu alidai aliyesaini maombi hayo kwa niaba ya waombaji (bodi ya wadhamini), Joram Bashange hana mamlaka ya kufanya hivyo kwa kuwa hapakuwa na uamuzi wa bodi hiyo kumpa mamlaka hayo na bodi haitambuliki.
Jaji Dyansobera alitoa uamuzi kuwa, hoja za pingamizi hazina msingi kwa kuwa hazikukidhi vigezo vya kuwa pingamizi la awali, ambalo linapaswa kuhusu masuala ya kisheria lakini hoja hizo zilihusu ya ushahidi.
Wakili Mashaka Ngole wa upande wa Profesa Lipumba aliieleza Mwananchi kuwa wanakusudia kufungua maombi ya mapitio Mahakama ya Rufani akidai wateja wake walinyimwa haki ya kusikilizwa.
Wakati huohuo, kambi ya Maalim Seif imefungua kesi Mahakama Kuu kuzuia mkutano mkuu unaoandaliwa na kambi ya Profesa Lipumba.
Comments
Post a Comment