Mbunge wa Mtwara Mjini, Maftaha Nachuma akichangia mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Madini kwa mwaka wa fedha 2018/2019, jijini Dodoma leo.
Dodoma. Mbunge wa Mtwara Mjini (CUF), Maftaha Nachuma amependekeza madini ya Tanzanite yafanywe kuwa nyara ya Taifa na atakayeyatoroshwa auawe.
Akichangia bajeti ya wizara ya nishati ya mwaka 2018/19 bungeni leo Mei 31, 2018; Nachuma amesema madini ya Tanzanite yanapatikana Tanzania pekee lakini yamekuwa yakitoroshwa ovyo ovyo.
“Udhibiti wa haya madini unahitajika, napendekeza yawe nyara ya Taifa na mtu akikamatwa anatorosha ovyo ovyo ikiwezekana auawe na napendekeza iwe fundisho,” amesema Nachuma.
Amesema kama Serikali ingekuwa na nia ya dhati, ingenunua mashine za kuchakata madini.
“Tanzanite ichakatwe hapa Tanzania, itatoa ajira nyingi sana na ni jambo la ajabu sana ajira zinatengenezwa nje ya nchi. Madini yanayopatikana Tanzania yanatoa ajira watu zaidi ya 600 nchini India,”amesema.
Nachuma amesema anasikitishwa na Shirika la Stamico kuendelea kuwa shirika la madini kwani limeshindwa kusimamia vyema wajibu wake na kuendelea kuliingizia taifa hasara.
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Catherine Magige ameungana na Nachuma na kusema wanaoyatorosha wachukuliwe hatua kali.
Kwa upande wake, Mbunge wa Tanga Mjini (CUF) amesema Mussa Mbarouk amesema kuna tatizo la mashine za kukata madini jambo linalosababisha usumbufu na kuchukua muda mrefu ikiwamo kwenda nchi za nje hivyo mashine ziongezwe kwa haraka.
Amesema Tanzania kulikuwa hakuna sababu ya kuezeka nyumba kwa majani au tembe kwani kuna madini ya bati lakini hatuna mtambo wa kuyachakata.
“Mabati yanatumika sana na yana soko kubwa na kama Serikali ingekuwa na mtambo ingekusanya fedha nyingi,”amesema.
“Huu mpango wa kukosa mtambo ni hujuma za wenye viwanda ili tuendelee kununua bati zao, nitataka majibu ya suala hili.” amesema Mbarouk.
Comments
Post a Comment