Skip to main content

Featured

Maombolezo: Hii ndiyo Hali Ilivyo Tanzania Bendera Yapepea Nusu Mringoti

Agizo la Rais John Magufuli la Bendera ya Taifa kupepea kwa nusu mlingoti kwa siku tatu kuanzia leo Septemba 22 kufuatia ajali ya kivuko cha MV Nyerere iliyotokea mkoani Mwanza limetekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Mjadala uenyekiti wa Freeman Mbowe wafunika uchaguzi Chadema



Wakati Chadema ikiendelea na mchakato wa kuwapata viongozi wake katika ngazi za nchini, nafasi ya mwenyekiti imeonekana kuwa ni mwiba na ndiyo inayozungumzwa ndani na nje ya chama hicho.
Mwanzoni mwa mwaka huu, chama hicho kilitangaza kuanza kwa uchaguzi kulingana na kalenda yake kuanzia ngazi ya Msingi hadi Taifa, lakini wakati chaguzi hizo zikiendelea katika ngazi za awali za misingi, matawi na kata minong’ono imeibuka kwamba kuna wanachama wanaotaka mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ang’atuke madarakani.
Kulingana na minong’ono hiyo, Mbowe anatakiwa ang’atuke apishe wengine kukiongoza chama hicho kikuu cha upinzani nchini, huku nyingine ikitaka aendelee na uongozi kwa kuwa hakuna mbadala wake.
Mbowe aliyeanza kukiongoza chama hicho mwaka 2004 akichukua kijiti kutoka kwa Bob Makani, anaelezwa kukijenga chama hicho ikiwamo kukiongoza kupata madiwani na wabunge wengi.
Chini ya uongozi wake kwa sasa Chadema ndiyo chama cha upinzani kinachoinyima CCM usingizi, chenye wabunge wengi na idadi kubwa ya madiwani ukilinganishwa na vyama vingine, ukiondoa chama tawala.
Kutokana na idadi kubwa ya madiwani chama hicho kimeweza kuongoza halmashauri nyingi ikiwamo Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Upande wanaotaka Mbowe aendelee wana hoja kwamba, kwa sasa ndani ya chama hicho hakuna mbadala, labda kwa siku za usoni na wasingependa kuona aking’atuka kwa kuwa hakuna wa kumuachia kijiti hicho cha uongozi.
Vilevile, wanaitazama minong’ono ya kumpinga Mbowe kama imechagizwa na wapinzani wake nje ya chama.
Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema anasema ndani ya chama hawana taarifa za mtu yeyote aliyeonyesha nia ya kugombea uongozi nafasi ya juu ya chama hicho.
Wachambuzi wa masuala ya siasa wanalitazama jina la Mbowe kama ndilo limeubeba uchaguzi ndani ya Chadema na linazungumzwa licha ya kwamba uchaguzi bado uko hatua za chini.
Pengine bila jina la Mbowe au nafasi yake kutajwa, uchaguzi wa Chadema ungeendelea kimyakimya kwa kuwa hakuna msisimko uliokuwa wazi.
Hata hivyo, sehemu kubwa ya wana Chadema, na hasa viongozi wanaamini kwamba lengo la minong’ono hiyo kuhusu mshikemshike juu ya uenyekiti ni kuwavuruga.
Mbowe na Ferguson
Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu anasema kuwa kitu kizuri ni kwamba wanajua kwamba wapo watu wenye nia ovu ya kutaka kuwavuruga lakini kamwe hawatawapa nafasi hiyo.
Mwalimu anasema kwake yeye, anaamini kwamba hakuna ubaya wowote kwa Mbowe kuendelea kubaki katika nafasi hiyo kwa kuwa bado anatosha.
Anatoa mfano wa timu ya mpira wa miguu ya Manchester United ya Uingereza ambayo baada ya kufanya vizuri na kunyakua vikombe vitatu, mashabiki walimtaka kocha wake wakati huo, Sir Alexander Ferguson kuachia ngazi na kumpisha mwingine kwa kile walichodai kuwa hakuwa na jipya tena.
“Lakini kila mtu leo ni shahidi nini kimetokea baada ya Ferguson kuondoka katika timu ile; washabiki na wanaofuatilia mpira wanajua kilichotokea, Manchester United iliporomoka na mpaka leo haijasimama vizuri kwa kuwa kocha huyo hakuondoka kwa muda muafaka.
Kwa mujibu wa Mwalimu, kwa sasa hakuna kijana ambaye yuko tayari kuchukua kijiti cha Mbowe, ingawa pia anaamini kwamba kiongozi huyo hawezi kuongoza milele kwani hata mwenyewe analijua hilo.
“Huwezi kubadili mwenyekiti tu kama unavyoamua kubadili runinga yako nyumbani; mwenyekiti ni taasisi na ni lazima ujiridhishe kwamba atakayebadilishwa ana mlengo gani na chama, hilo ndiyo la msingi, tusije kuweka kirusi mwisho wa siku kikawa mwiba kwa chama,” anasisitiza Mwalimu.
Hata hivyo, Mwalimu anasema huwezi kumfananisha Mbowe na wenyeviti wengine wa vyama vya upinzani ambao wanang’ang’ania madaraka, kwa kuwa yeye ni tofauti kutokana na utendaji wake wa kuwaandaa vijana wasimame wenyewe.
“Ndiyo maana leo unakuta Chadema kuna vijana weye uwezo ambao wameandaliwa vema kama Halima Mdee, John Mrema, John Mnyika, Salumu Mwalimu, John Heche na wengine wengi kwa sababu chama chetu kinatoa nafasi kwa kila mmoja,” anaongeza Mwalimu.
Hata hivyo, Mwalimu anasema kuwa katika kuandaa huko vijana wapo waliopewa nafasi na matokeo yake wakageuka wasaliti kisha kuanza chokochoko za kutaka kukidhoofisha chama.
“Sisi sote ni mashahidi, wapo vijana waliopewa nafasi na uongozi wa chama wakaonekana na kuwa wakubwa lakini matokeo yake wakageuka wasaliti na kutaka kukisambaratisha chama lakini waliishia kufukuzwa na chama kikaendelea kwa sababu hakuna aliye mkubwa zaidi ya chama,” anasisitiza Mwalimu bila kutaja vijana hao.
“Lazima uwe na mpango maalumu na si leo unaamka unasema mwenyekiti hafai, kwanza katiba yetu haijaweka ukomo; ni kweli kama binadamu mwenyekiti ana makosa na mapungufu yake na siyo malaika, lakini lazima tuwe makini kwa kumuweka mtu sahihi atakayekuwa msaada kwa chama na si ndumilakuwili,” anasisitiza.
Profesa Baregu atia neno
Akizungumzia hilo Profesa wa sayansi ya siasa nchini, Mwesiga Baregu anasema suala la kuendelea au kutoendelea kwa Mbowe ni la wanachama wenyewe na chama chao na si vinginevyo.
Anasema kuwa katiba ya chama hicho haijatoa ukomo wa mwenyekiti kugombea vipindi vingapi hivyo kama wanachama na chama chao wataona anastahili kuendelea, hakuna mtu wa kuwapinga kwa kuwa wao ndiyo wenye madaraka.
“Hiyo minong’ono ni hisia tu, nadhani tuwaachie wenyewe wenye chama chao waamue wanataka nini na sisi tufuate kwa kuwa hatuna tunachoweza kubadili,” anaongeza Profesa Baregu.
Hata hivyo, Profesa Baregu anasema jambo lingine linalosababisha minong’ono hiyo ni fitina kutoka kwa wapinzani wa chama hicho ili kukidhoofisha.
“Sasa kuna fitina sana. Mfano tumeona kilichotokea katika uchaguzi wa marudio katika jimbo la Kinondoni, hivyo uwezekano wa watu wafitini kutumia nafasi ya uchaguzi wa ndani kwa lengo la kuwasambaratisha ni mkubwa,” anaongeza.
Anasema wafitini hao wana lengo la kuleta mgawanyiko na endapo hicho hakitagundua mapema kitakwenda mrama.
“Mimi sitarajii Chadema leo kuachwa bila kudhoofishwa, imepitia mengi na yaliyotekea Kinondoni kwenye uchaguzi mdogo yanaleta funzo kubwa,” anaongeza Profesa Baregu.
Profesa Baregu anasema kwa sasa chama hicho kinapaswa kuwa macho na kisiamini mtu au kitu chochote hasa kipindi hichi kinapoelekea katika uchaguzi wa ngazi mbalimbali mpaka Taifa.
Hata hivyo, Profesa Baregu anasema kuwa hali hiyo ni kawaida katika siasa za vyama vingi na kwamba anaamini chama hicho kitavuka salama kama ilivyokuwa katika vipindi vingine vya uchaguzi.
“Wote ni mashahidi, misukosuko katika chaguzi za Chadema ni hali ya kawaida lakini mwisho wa siku mambo yanasonga. Kinachopaswa ni umakini wa hali ya juu ili kuvuka na kuendelea na maisha kama kawaida,” anaongeza.
Hatua za uchaguzi
Wakati Profesa Baregu akisema hayo, Mrema anasema; “Chadema kwa sasa kimeelekeza nguvu kubwa kwa uchaguzi wa ngazi za chini (msingi, matawi na mashina) na kwamba baada ya hatua hiyo kukamilika watafuata nyingine.
Kwa mujibu wa Mrema, tayari viongozi wakuu akiwamo Mbowe wanashiriki kikamilifu katika mchakato huu na kwamba wataendelea kushiriki mpaka pale itakapofikia hatua ya kitaifa.

Comments

Popular Posts