Skip to main content

Featured

Maombolezo: Hii ndiyo Hali Ilivyo Tanzania Bendera Yapepea Nusu Mringoti

Agizo la Rais John Magufuli la Bendera ya Taifa kupepea kwa nusu mlingoti kwa siku tatu kuanzia leo Septemba 22 kufuatia ajali ya kivuko cha MV Nyerere iliyotokea mkoani Mwanza limetekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.

VIDEO-Mbowe, Dk Tulia wazungumzia mvutano mazishi ya Bilago


Dodoma. Katika siku ambayo Bunge lilitawaliwa na hotuba za kutaka amani na mshikamano wakati wa kuaga mwili wa mbunge wa Buyungu, mvutano baina ya Chadema na ofisi ya Bunge kuhusu mazishi uliwalazimisha viongozi wa vyombo hivyo viwili kuuzungumzia.
Mbunge huyo wa Chadema, Kasuku Bilago aliagwa jana na wabunge kwenye viwanja vya Bunge, ambako kulikuwa na hotuba za viongozi wa vyama na wabunge, lakini ikabidi mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na naibu spika, Dk Tulia Ackson kuzungumzia tarehe ya mazishi.
“Tunatoa ratiba hii na wenzetu wanatoa hivi,” alisema Mbowe akizungumzia mkanganyiko wa ratiba ya mazishi uliojitokeza juzi.
“Sasa tumepeana mikono ya amani hapa. Kwa hiyo amani hiyo isiwe ya kinafiki, bali tushikamane katika msiba huu na mimi najua misiba ndiyo huwaunganisha watu maeneo yote.”
Mbowe alisema kumekuwa na mvutano usiokuwa na maana ambao ulikuwa ni wa kugombea siku ipi mwili wa Kasuku uzikwe.
Kiongozi huyo wa kambi ya upinzani bungeni aliliomba Bunge liache kutumia madaraka ya wanafamilia na kulazimisha mwili wa mbunge huyo uzikwe leo badala ya siku ya Alhamisi iliyopendekezwa na familia na Chadema.
Alitaja sababu za kutaka maziko hayo yafanyike kesho kuwa ni kwa kuwa Kasuku alikuwa kiongozi wa chama kutokana na kuwa mbunge, pia alikuwa mwenyekiti wa Chadema wa Kanda ya Magharibi na mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho na hivyo anastahili kuagwa na wenzake.
Kauli ya Mbowe ni mwendelezo wa kile alichokisema juzi kwenye Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa kuaga mwili huo jijini Dar es Salaam, Mbowe alisema katika uhusiano wa kibinadamu wabunge wa pande hizo mbili wanaelewana kwa njia moja au nyingine, lakini wa kambi ya upinzani wanaelewa vizuri. “Upande wa pili wa wenzetu, wana urafiki wa mashaka. Popote wanapojipa jukumu la kufanya uamuzi kwa niaba ya kambi yetu, tunaona hauna nia njema,” alisema Mbowe.
“Bilago alifariki Jumamosi mchana, lakini saa 11:00 jioni ofisi ya Bunge ilitangaza ratiba ya mazishi jaribu ku-imagine (kufikiria).
“Wakati huo tulikuwa Muhimbili na ndugu wa marehemu tukihifadhi mwili na hatukukaa kikao lakini wenzetu wanatoa ratiba yao.”
Hata hivyo, Dk Tulia alitoa ufafanuzi wa mkanganyiko huo akisema kauli hizo haziwezi kuwavuruga katika mazishi hayo na badala yake watakuwa kitu kimoja mwanzo hadi mwisho.
Dk Tulia alisema Mbowe atakuwa na Spika Job Ndugai mkoani Kigoma kabla ya mazishi ili wajadili kwa pamoja suala hilo.
Alitaja chanzo cha mgongano kuwa ni kikao cha kamati ya uongozi kilichofanyika Jumapili jijini Dodoma ambako Mbowe alituma mwakilishi na walikubaliana kwa pamoja kuwa mazishi yafanyike leo, lakini baadaye walipokea taarifa nyingine kutokana na kikao kilichohusisha Chadema na familia.
Hata hivyo, sakata hilo halikuonekana kuwagawa wabunge ambao walionekana kuwa kitu kimoja muda wote wakikaa vikundi vikundi na kujadili kwa pamoja.
Mvutano huo ulisababisha wabunge waliopata nafasi ya kuzungumza jana wahimize amani na mshikamano na kukemea malumbano ya aina hiyo.
“Tumsitili mwenzetu kwa amani na utulivu. Tuache chama chake na watu wake wamuage kwa nafasi yao,” alisema kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe jana wakati wa kuaga mwili wa Bilago. “Tangulia mtu wa Wayungu. Walikuchagua na leo Wayungu wamekupoteza. Nenda kamsalimie Mheshimiwa Hafidh mwambie nasi tunakuja mtuwekee nafasi.” Zitto, ambaye ni mbunge wa Kigoma Mjini aliwataka wabunge kujifunza kuwa kifo kipo na kila mtu lazima atakufa, hivyo ni bora kujiandaa na kuishi na watu vizuri
Pia aliwataka watu wote kuwa wamoja katika kipindi cha msiba kwa kuwa ndiyo njia bora ya kumuenzi Bilago ambaye alihubiri umoja.
Wito kama huo ulitolewa na mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia ambaye aliwaonya wanasiasa kuchunga ndimi zao.
Mbatia alisema misingi iliyoachwa na mwasisi wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere inapaswa kulindwa na kuenziwa wakati wote kwa kuwa wote ni wa Taifa moja na wanapaswa kulinda masilahi ya Taifa.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge (CCM) aliwataka wananchi kuwa watulivu na kujiandaa katika maisha kwa kuwa hakuna anayejua siku wala saa ya kufa
Mwenyekiti wa wabunge wa Mkoa wa Kigoma, Daniel Nsanzugwako pia aliwaomba wabunge kuwa wamoja kama Bilago alivyotamani wakati wote.
Ibada hiyo iliongozwa na Padri Paul Mhindi ambaye ni mlezi wa vyuo vya kikatoliki mkoani Dodoma akisaidiwa na Padri Antipasi Shayo wa Parokia ya Swaswa ya Jijini hapa.

Comments

Popular Posts