Skip to main content

Featured

Maombolezo: Hii ndiyo Hali Ilivyo Tanzania Bendera Yapepea Nusu Mringoti

Agizo la Rais John Magufuli la Bendera ya Taifa kupepea kwa nusu mlingoti kwa siku tatu kuanzia leo Septemba 22 kufuatia ajali ya kivuko cha MV Nyerere iliyotokea mkoani Mwanza limetekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Wadau wakinzana mpango wa sheria ya kuruhusu kujipima Ukimwi



Dar es Salaam/Dodoma. Siku moja baada ya Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kusema amepeleka ombi kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutaka kuundwa kwa sheria ya kuruhusu mtu kujipima Virusi vya Ukimwi, wadau wametofautiana kuhusu hatua hiyo.
Baadhi wanapinga mpango huo kwa hoja kuwa una madhara kulinganisha na faida na wengine wakisema iwapo miongozo itafuatwa, utakuwa na manufaa.
Mwalimu, ambaye pia anahusika na maendeleo ya jamii, jinsia na wazee, alisema hayo bungeni jana alipokuwa akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Mtambulie (CUF), Masoud Abdalla Salim.
Mbunge huyo alitaka kujua kama Serikali ina mkakati wa ziada kutambua wale wanaopata athari za VVU, hasa mkoani Dodoma ambako maambukizi yameongezeka.
Akijibu swali hilo, Mwalimu alisema wamewasiliana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa lengo la kufanya mabadiliko ya sheria ili mtu aweze kujipima mwenyewe ugonjwa huo.
Alisema kipimo hicho kinamuwezesha mtu kujua hali yake ndani ya dakika 15 na hivyo kitasaidia katika mapambano dhidi ya Ukimwi.
Lakini mkurugenzi mtendaji wa taasisi binafsi ya Sikika, Irenei Kiria alisema hatua hiyo ina athari zaidi ya faida kwa kuwa mtu akijipima nyumbani anatakiwa awe na ujasiri wa kwenda hospitali kupima upya na kuanza dawa.
Alisema walio wengi hupima kwa sababu wanataka kuoa au kuolewa, wana ujauzito au wana wasiwasi kwa kuwa walijamiiana na mtu wanayemuhisi ana maambukizi.
“Hivyo majibu yakiwa mazuri hakuna madhara, yakiwa mabaya ndiyo kuna madhara. Ndiyo maana kuna ushauri nasaha kabla na baada ya kupima. Anayejipima nyumbani atakuwa hajapata ushauri.” alisema
Alisema kwa anayekosa ushauri, lolote linaweza kutokea na likahatarisha maisha ya wahusika au muhusika.
“Kama wamepima wenyewe nyumbani kwa ajili ya kuoana, mmoja wao akikutwa nao na mwingine hana, kama hawajaandaliwa kwa ushauri ni rahisi aliyekutwa nao akafanya kitu kibaya,” alisema Kiria.
“Katika suala la majibu ya Ukimwi hakuna bingwa na lolote linaweza kutokea, ndiyo maana watoa ushauri huwasoma wanaowashauri kwanza kabla ya kuwapa majibu.”
Kiongozi wa Chama cha Madaktari (MAT) ambaye hakuwa tayari jina lake kuandikwa gazetini, alisema haina maana mtu kujipima bila kupata ushauri nasaha kabla na baada. Alisema kufanya hivyo ni kazi bure kwa kuwa anaweza kwenda hospitali kuanza dawa au akaamua kulipiza kisasi kwa anaodhani wamemuambukiza.
Alifafanua kuwa ushauri ni wa maana kwa anayekutwa nao na asiyekutwa nao, hivyo kujipima kuna madhara hata kwa ambao hawatabainika kuwa nao.
“Mtu akijipima bila kupata ushauri nasaha wa jinsi ya kujilinda asipate maambukizi, akijikuta hana anaweza kudharau asiwe makini kwa kulinganisha alivyokuwa anaishi kabla hajapima (hakuwa makini) na hajaambukizwa,” alisema
Kwa upande wa mkurugenzi mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids), Dk Leonard Maboko alisema kama mpango huo utawekewa utaratibu mzuri, utaongeza ari ya watu kutambua afya zao.
Alisema kuna ambao wanataka kufahamu afya zao, lakini wanaogopa kwenda kwenye mikusanyiko ya watu kama hospitali na zahanati, hivyo kwa njia hii watapata fursa ya kujitambua.
“Kwa sasa bado ni wazo na ni majaribio, yatakapokamilika kutakuwa na miongozo mbalimbali ya kufanya itakayomuongoza muhusika afanye nini iwapo atajikuta ameambukizwa na afanye nini iwapo atakuwa hajaambukizwa,” alisema
Dk Maboko alisema waliojaribu njia hiyo wamepata matokeo mazuri, hivyo cha msingi taratibu na miongozo izingatiwe.

Comments

Popular Posts