Skip to main content

Featured

Maombolezo: Hii ndiyo Hali Ilivyo Tanzania Bendera Yapepea Nusu Mringoti

Agizo la Rais John Magufuli la Bendera ya Taifa kupepea kwa nusu mlingoti kwa siku tatu kuanzia leo Septemba 22 kufuatia ajali ya kivuko cha MV Nyerere iliyotokea mkoani Mwanza limetekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Chadema, ACT-Wazalendo wamerudia makosa ya Ukawa Segerea 2015



Jimbo la Buyungu wilayani Kakonko, Kigoma, litapata mbunge mpya baada ya uchaguzi mdogo uliopangwa kufanyika Agosti 12. Uchaguzi mdogo unafanyika kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Kasuku Bilago (Chadema), aliyefariki dunia Mei 26.
Uchaguzi huo unafanyika pamoja na wa madiwani katika kata 77, kujaza nafasi zilizo wazi kwenye mikoa tofauti. Julai 25, vyama vya Chadema na ACT-Wazalendo, kupitia kwa wakuu wao wa idara za uchaguzi, vilitangaza kwa vyombo vya habari makubaliano yao ya kuachiana nafasi za kugombea.
Makubaliano hayo yalisainiwa na mwenyekiti wa kampeni na uchaguzi wa ACT-Wazalendo, Mohamed Babu na mkurugenzi wa uchaguzi wa Chadema, Reginald Munisi. Baada ya maafikiano hayo, sasa ni kwenda kwenye utekelezaji.
ACT-Wazalendo wamekubali kuwaachia Chadema jimbo la Buyungu ambako anagombea Elias Kanjero. Makubaliano yamefikiwa katikati ya mchakato wa uchaguzi. Na tayari kwenye orodha ya wagombea ubunge wa Buyungu, lipo jina la Jonathan Kasigara wa ACT-Wazalendo.
Kuhusu Kasigara kuwemo kwenye orodha ya wagombea wa jimbo hilo, Julai 26, Ado Shaibu, ambaye ni katibu wa itikadi na uenezi wa ACT-Wazalendo, alisema baada ya makubaliano ya mwisho ndiyo sasa mchakato wa kumuondoa umeanza rasmi.
“Kama unavyoona, makubaliano yalifanyika jana (Julai 25) na leo (Julai 26), mgombea wetu anaanza mchakato wa kuliondoa jina lake kwenye orodha ya wagombea,” alisema.
Hesabu niliyoikamilisha ni hii; Julai 25, ACT-Wazalendo na Chadema walitia saini makubaliano kuwa Kanjero wa Chadema ndiye ataungwa mkono na vyama vyote viwili. Julai 26, ACT-Wazalendo, walianza utaratibu wa kuwasiliana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ili Kasigara aondolewe kwenye orodha ya wagombea. Hapohapo uchaguzi ni Agosti 12.
Kutoka Julai 26 ambayo ACT-Wazalendo walianza mchakato wa kuliondoa jina la Kasigara NEC kama mgombea ubunge Buyungu ni siku 17 tu. Swali linakuja, je, kwa hizo siku zilizobaki, inawezekana kweli NEC wawe hawajachapa karatasi za uchaguzi? Kama itakuwa tayari, watakubali kuingia gharama ya kuchapa karatasi nyingine upya ili kumuondoa Kasigara?
Ifahamike kuwa ni utaratibu wa uchaguzi kwa NEC kuchapa mapema karatasi za uchaguzi na kutoa mfano wake kwa wagombea ili wazitumie kuelimisha wapigakura namna ambavyo wanapaswa kuchagua bila kuharibu kura. Hata kama NEC watakuwa hawajachapa karatasi, je, kwa siku 17, hata maandalizi hayajafanyika?
Ikiwa maandalizi yameshafanyika na kwa sababu inafahamika maandalizi ni gharama, je, NEC watakubali kweli kuahirisha maandalizi ambayo tayari walishayafanya na gharama zake ili kuyapokea na kuyazingatia maombi ya ACT-Wazalendo, kisha kumuondoa Kasigara katika orodha ya wagombea?
Historia ni mwalimu
Edward Lowassa alikuwa mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano kwa tiketi ya Chadema na kuungwa mkono na Ukawa, na Seif Sharif Hamad alisimama Zanzibar. Kutokana na sheria za nchi kutotoa mwanya kuunda ushirikiano wa uchaguzi, vyama hivyo vilikubaliana kuachiana nafasi mahali ambako chama fulani na mgombea wake walikuwa na nguvu zaidi.
Hiyo ndiyo sababu Lowassa alibeba mwavuli wa Ukawa upande wa Jamhuri ya Muungano, vilevile Seif na CUF Zanzibar. Changamoto kubwa ikazuka kwenye majimbo na kata. Maeneo mengi yalipatiwa ufumbuzi, ingawa kujichanganya kwa vyama vya Ukawa, kulisababisha CCM ishinde kwa urahisi kata nyingi, vilevile jimbo la Segerea.
Mpaka kampeni za Uchaguzi Mkuu 2015 zinazinduliwa, kuna baadhi ya majimbo hayakuwa yamepata mwafaka. Kutaja majimbo matatu kama mfano ni Temeke na Segerea, Dar es Salaam ambako vyama vya Chadema na CUF vilivutana, vilevile Masasi, Mtwara ambako NLD na CUF walikuwa wakivutana, kila chama kikiamini kina nguvu na kina mgombea mwenye ushawishi zaidi.
Agosti 29, 2015, wakati Ukawa walipozindua kampeni zao Viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam, jimbo la Segerea walitambulishwa wagombea wawili; Julius Mtatiro wa CUF na Anatropia Chadema. Ilielezwa kwenye mkutano huo kwamba ufumbuzi hasa wa nani angesimama kama mgombea ungetolewa siku mbili baadaye.
Changamoto kama hiyo pia ilionekana Temeke, Chadema alikuwepo Bernard Mwakyembe na Cuf ni Abdallah Mtolea. Agosti 31, 2015, viongozi wa Ukawa walitoa taarifa kuwa Segerea mgombea aliyepitishwa ni Mtatiro wa Cuf, vilevile Temeke alibaki Mtolea wa Cuf, kwa maana hiyo Anatropia na Mwakyembe walipaswa kujitoa ili kukidhi vigezo na masharti ya hati ya makubaliano ya Ukawa.
Rekodi za NEC zinaonesha kuwa Mwakyembe aliwasilisha Tume ya Uchaguzi kiapo na barua ya kujitoa Septemba 4, 2015 na Septemba 7, 2015, NEC walikiri kupokea maombi hayo. Na katika orodha ya wagombea ubunge Temeke, kama yalivyoandikwa kwenye karatasi za uchaguzi, jina la Mwakyembe halikuwemo, kuonesha kuwa maombi yalikubaliwa.
Uchaguzi Mkuu 2015 ulifanyika Oktoba 25. Mwakyembe aliwasilisha maombi ya kujitoa Septemba 4, yaani mwezi mmoja na siku 21 kabla ya uchaguzi. Upande wa Segerea, ulianza mvutano, ikawa inadaiwa Anatropia hakutaka kujitoa. Vuta nikuvute hiyo ikafanya Anatropia achelewe kutimiza vigezo vya kujitoa, kwa maana ya kupeleka barua ya kujitoa na hati ya kiapo.
Kupitia kile alichokitolea ufafanuzi Mtatiro Februari 3, 2016 kwenye ukurasa wake wa Facebook, ni kwamba Anatropia aliwasilisha NEC hati ya kiapo Septemba 14, 2015 bila barua ya kujitoa, kwamba mchakato wote wa kujitoa, Anatropia aliutimiza Oktoba 12, 2015, yaani siku 13 kabla ya uchaguzi.
Mkanganyiko huo wa Anatropia na Mtatiro, ulisababisha jimbo la Segerea liwagharimu Ukawa, hivyo kuipa mwanya CCM. Wagombea wawili wa Ukawa, yaani Mtatiro na Anatropia walipata kura 124,367, sawa na asilimia 44.4 ya wapigakura 279,779 waliojiandikisha jimboni humo, wakati mgombea wa CCM, Bona Kalua, alipata kura 94,640, sawa na asilimia 33.8. Bona akawa mshindi.
Kimahesabu, Mtatiro alipata kura 75,744, wakati Anatropia zake zilikuwa 48,623. Hivyo, kama wapigakura 19,000 tu kati ya 48,623 waliompigia Anatropia, wangempigia Mtatiro, maana yake Ukawa wangeshinda jimbo la Segerea. Ukiangalia kosa la jumla ni kutocheza vizuri na muda, kujua nini kifanyike wakati gani.
Makosa yanarudiwa Buyungu
Anatropia alikamilisha kujitoa NEC siku 13 kabla ya uchaguzi na ACT-Wazalendo walianza mchakato wa Kasigara kujitoa siku 17 kabla ya uchaguzi. Tofauti ni siku nne tu. Je, hizo siku nne zinatosha kufanikisha mgombea wa ACT-Wazalendo atolewe, wakati Anatropia ilishindikana mwaka 2015? Tutaona kitakachotokea kwenye karatasi za uchaguzi.
Swali la kujiuliza ni hili; viongozi wa Chadema na ACT-Wazalendo walikuwa wapi kuhakikisha makubaliano yao yanawekewa saini mapema ili kuepusha yaliyotokea Segerea yasijirudie Buyungu? Ukipiga mahesabu unaona kwamba kulikuwa na muda wa kutosha, lakini kilichotokea ni kwamba wamesuasua mpaka ulipobaki mdogo.
Mei 30, mwaka huu, Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, walitangaza kukubaliana kusimamisha mgombea mmoja jimbo la Buyungu. Kutoka walipotangaza mpaka kutiliana saini ulipita mwezi mmoja na siku 25. Swali; siku zote walikuwa wapi ikiwa walitambua uchaguzi mdogo unafuata?
Kuchelewa kwao kufanya uamuzi ni sababu ya wagombea wa ACT-Wazalendo na Chadema kuchukua fomu ya kugombea ubunge, vilevile waliachwa mpaka wakazirejesha kwa msimamizi wa uchaguzi Wilaya ya Kakonko, hivyo kukamilisha taratibu zote za kupitishwa kuwa wagombea halali. Hili lilikuwa kosa la ufundi.
Kwa kuchukua matokeo ya jimbo la Segerea kwa wapigakura 48,623 kumpigia kura Anatropia ambaye ilikuwa imeshatangazwa si mgombea wa Ukawa, haishindikani kwa Buyungu wapigakura kumchagua Kasigara wa ACT-Wazalendo, wakati chama chake kimeshatangaza kumuunga mkono Kanjero wa Chadema. Ikitokea hivyo, inaweza kuathiri kura za Kanjero kama Mtatiro alivyoathiriwa na Anatropia.
Zitto na Mbowe
Mei 30, Zitto na Mbowe walipotangaza kuunganisha nguvu Buyungu, Zitto aliwaita viongozi wa ACT-Wazalendo Mkoa wa Kigoma na Wilaya ya Kakonko, kuwaambia kuhusu makubaliano yao hapohapo na kuwataka kwenda kutekeleza. Matokeo yake utekelezwaji umefanyika kitaifa mwezi mmoja na siku 25 baadaye.
Viongozi wa vyama hivyo Kakonko na Kigoma baada ya makubaliano ya Mei 30, ilishindikana nini kukutana na kufanya mchakato wa kumpata mgombea ubunge wa Buyungu mwenye kukubaliwa na pande zote mbili? Ni kwa nini walichelewa na kuacha Kasigara na Kanjero wachukue fomu na kurejesha? Swali ni lilelile; viongozi wa Chadema na ACT-Wazalendo walikuwa wapi?
Ushauri kwa viongozi wa Chadema, ACT-Wazalendo na vyama vingine, wanapoamua kufanya ushirikiano kwa ajili ya uchaguzi, wahakikishe wanakwenda vizuri na muda. Wasifanye makosa ya kuchelewa kuamua wagombea, kwani wanaweza kusababisha karatasi za uchaguzi ziwe na wagombea wa vyama vyote vyenye ushirikiano, hivyo kuathiri ushindi.
Kuchelewa kunaelekea kusababisha karatasi za uchaguzi Buyungu ziwe na majina ya Kasigara na Kanjero. Na inaweza kufanya Kasigara aathri kura za Kanjero. Hali hiyo, inaweza kutoa mwanya kwa mgombea wa CCM, Christopher Chiza kupata mpenyo wa katikati ya Kasigara na Kanjero kama Bona aliposhinda katikati ya Anatropia na Mtatiro.

Comments

Popular Posts