Skip to main content

Featured

Maombolezo: Hii ndiyo Hali Ilivyo Tanzania Bendera Yapepea Nusu Mringoti

Agizo la Rais John Magufuli la Bendera ya Taifa kupepea kwa nusu mlingoti kwa siku tatu kuanzia leo Septemba 22 kufuatia ajali ya kivuko cha MV Nyerere iliyotokea mkoani Mwanza limetekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Chaguzi za marudio zabakiza miezi 14

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dk Athuman Kihamia akiwasili katika ofisi za Halmashauri ya jiji la Arusha alipokwenda kukabidhi ofisi, hivi karibuni.
Dar/Tarime. Chaguzi ndogo za madiwani na wabunge ambazo zimekuwa zikifanyika kutokana na wawakilishi hao wa wananchi kufa riki dunia au kuhama vyama vyao zitakoma miezi 12 kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao.
Hii ina maana kuwa madiwani na wabunge ambao wamekuwa wakihama na kuteuliwa na vyama wanavyohamia kugombea tena, wana miezi 14 kufanya hivyo la sivyo watahitajika kusubiri uchaguzi mkuu ujao mwaka 2020.
Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na wimbi la madiwani hususan wa upinzani kutimkia CCM kwa kile wanachoeleza kuwa ni kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli.
Jumamosi iliyopita, mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara alitangaza kuhamia CCM akiwa ni mbunge wa tatu wa upinzani kutimkia chama hicho tawala.
Wengine waliomtangulia Waitara ni Maulid Mtulia (Kinondoni-CUF) na Dk Godwin Mollel (Siha-Chadema) ambao baadaye walipitishwa na chama hicho tawala kugombea tena ubunge na kushinda kwenye majimbo hayo. Kwa upande wa pili, Lazaro Nyalandu aliyekuwa mbunge wa Singida Kaskazini (CCM) alitimkia Chadema, lakini hakugombea tena.
Wakati hayo yakiendelea, katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole ametamba kuwa wabunge na madiwani zaidi wa upinzani watajiunga na chama hicho tawala, kauli ambayo imejibiwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akisema hawatikisiki na wapo imara.
Mbali ya wabunge hao, tangu hamahama hiyo ilipoanza, zaidi ya madiwani 50 wa upinzani wametimkia CCM na kuifanya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuitisha uchaguzi mdogo na uamuzi huo wa Waitara unamaanisha kuwa uchaguzi mwingine mdogo katika jimbo hilo utafanyika.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dk Athuman Kihamia akizungumza na Mwananchi jana alisema kwa sasa jimbo au kata ikiwa wazi uchaguzi unafanyika, “Lakini ikibaki, miezi 12 kabla ya Bunge la mwisho kuvunjwa mwaka 2020 hautafanyika.”
Jana, spika wa Bunge Job Ndugai alisema amepokea barua kutoka kwa Waitara ya kujivua uanachama wa Chadema.
Kiongozi huyo wa Bunge alitoa kauli hiyo jana akiwa Ikulu jijini Dar es Salaam wakati Rais John Magufuli alipokuwa akitoa hati za utambuzi za viwanja kwa mabalozi 62 wa nchi mbalimbali na mashirika matano ya kimataifa kwa ajili ya kujenga ofisi na makazi katika jiji la Dodoma.
“Napenda nitangaze kuwa leo asubuhi (jana) nimepokea barua kutoka kwa mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara kuwa amejivua uanachama wa chama chake na kujiuzulu ubunge” alisema.
Kutokana na hatua hiyo, Ndugai alisema ataiandikia NEC barua ili taratibu nyingine zifuate.
“Kilichobakia ni kuiandikia Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa Jimbo la Ukonga liko wazi,” aliongeza
Wabunge, madiwani kutimka
Juzi, katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole akihutubia mkutano wa kampeni za udiwani katika Viwanja vya Rebu katika Mji wa Turwa, Tarime mkoani Mara alisema kuna wabunge wawili na madiwani kibao ambao watajiunga na chama hicho.
Polepole aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba alitumia mkutano huo kumzungumzia Mbowe kwamba uking’ang’anizi wake katika nafasi ya uenyekiti utawakimbiza wabunge na madiwani.
“Kukosa ushirikiano kutoka uongozi wa juu wa chama na kutoambilika kwa Mbowe ni kati ya sababu zinazowakimbiza wanaohama Chadema. Natabiria chama kile kuendelea kuporomoka zaidi.”
“Kuna wabunge wawili ambao kwa sasa nahifadhi majina yao nao watahamia CCM wakati wowote kuanzia sasa; madiwani wanaoomba kuja idadi yao haihesabiki,” alisema Polepole.
Akimnadi mgombea wa CCM, Mwita Chacha maarufu ‘Chacha Kamanda’ Polepole aliwaomba wapigakura wa kata hiyo kumchangua ili akashirikiane na viongozi wa CCM inayoongoza Serikali kuwaletea maendeleo.
Polepole alitumia mkutano huo kutaja baadhi ya miradi inayotekelezwa ikiwamo ununuzi wa ndege, ujenzi wa reli ya kisasa, elimu bure, ujenzi wa barabara na madaraja kuwa ni mifano tu ya utekelezaji wa ilani na ahadi za CCM wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Akiomba kura, mgombea Mwita Chacha aliwaomba wapigakura kumwamini na kumchagua ili akasimamie utekelezaji wa ilani ya CCM ambayo ndiyo inatekelezwa licha ya halmashauri na Jimbo la Tarime kuongozwa na Chadema.
Mbowe asema hawatishiki
Akizindua kampeni za kata hiyo ya Turwa, Mbowe aliwataka viongozi, wanachama, wafuasi na wapenzi wa chama hicho kutotishika na wimbi la viongozi na wanachama wanaohamia vyama vingine akisema linakipa chama hicho fursa ya kujiimarisha.
“Wale wanaokimbilia vyama vingine wanakiimarisha zaidi chama chetu kwa sababu kinatupa fursa ya kubaki na viongozi na wanachama wenye uchungu na nia ya dhati ya kukijenga chama chao,” alisema.
Mbowe, ambaye pia ni kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni alisema Chadema iko imara kulinganisha na wakati mwingine kutokana na kubakiwa na watu wenye nia ya dhati ya kuipigania.
“Wanaofika bei kwa ahadi ya fedha au vyeo waondoke mapema na ninawahakikishia Chadema itaendelea kuwa taasisi imara zaidi kuliko ilivyo sasa,” alisema.
Bila kutaja majina, kiongozi huyo alisema chama hicho kimewahi kuondokewa na viongozi wa ngazi za juu kiasi cha wengi kudhani kingeyumba lakini ikawa kinyume chake kwa kuimarika na kupata wabunge, madiwani na wanachama wengi zaidi.
Viongozi wa kitaifa waliowahi kujiondoa Chadema ni aliyekuwa katibu mkuu, Dk Wilbrod Slaa na makamu mwenyekiti na katibu mkuu wa zamani, Dk Amani Walid Kaborou (sasa marehemu). Pia yumo makamu mwenyekiti wa zamani, Saidi Arfi.
Kuhusu mgombea wa Turwa, kwa tiketi ya Chadema, Charles Mnanka mwenyekiti huyo aliwaomba wapigakura wa kata hiyo kutumia haki yao kikatiba kumchagua mgombea wa Chadema ili akaungane na madiwani wa chama hicho kuiongoza Halmashauri ya Wilaya ya Tarime inayopaa kimaendeleo tangu chama hicho kishike ushukani kulinganisha na ilipokuwa inaongozwa na CCM.
“Shahada yako ndiyo ushindi wako, itumie kuleta mabadiliko kimaendeleo Tarime. Msiogope vitisho na ninajua watu wa Tarime siyo waoga na hawarudi nyuma katika kile wanachokiamini,” alisema.
Ili kuimarisha chama, Mbowe alitumia mkutano huo kuwaagiza viongozi wa Chadema kote nchini kuhakikisha wanahamasisha wanachama kujitolea kujenga ofisi za wilaya katika maeneo yao kukiwezesha kuondokana na adha ya kupanga.
“Nimeweka jiwe la msingi la ofisi ya Chadema Wilaya ya Tarime inayojengwa kwa nguvu na michango ya viongozi na wanachama; moyo huu uenee kote ili chama kiwe na ofisi zake za kudumu.”
Mbowe alichangia Sh2 milioni mbili kuunga mkono juhudi hizo na kuwaagiza wabunge wote na wenyeviti wa halmashauri zinazoongozwa na Chadema Mkoa wa Mara kila mmoja kuchangia milioni moja.

Comments