Mkuu wa wilaya ya Arumeru mkoa wa Arusha ,Jerry Muro akiapa kufuatia uteuzi uliofanywa hivi karibuni,kushoto ni Mkuu wa Arusha,Mrisho Gambo.
Arusha. Unaweza kusema mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro ameanza majukumu yake mapya kwa kufuata mtazamo wa Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola.
Leo Jumanne Julai 31, 2018 Muro amekula kiapo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo huku akiwataka viongozi wa wilaya hiyo wanaoona hawawezi kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM wampishe kabla hajaingia ofisini.
Kauli hiyo inafanana na iliyotolewa na Lugola katika mahojiano na MCL Digital Julai 8, 2018 kwamba akifa anatamani azikwe na ilani ya chama hicho itakayokuwepo wakati huo.
Alisema hakuna ilani kama ya CCM miongoni mwa vyama mbalimbali vya siasa nchini, anapenda kutembea nayo kila wakati ikiwa anatekeleza shughuli mbalimbali za Serikali
Wakati Lugola akitembelea na ilani hiyo, Muro amesema anataka kuona watendaji katika wilaya hiyo wanatekeleza ilani hiyo na wale watakaoshindwa, “watapata tabu sana.”
“Najua Rais John Magufuli anataka nini, nitashangaa kama watajitokeza watu wachache kutupinga,” amesema Muro huku akibainisha kuwa katika kipindi cha miaka miwili anataka kuibadilisha Arumeru.
“Nimekuja Arumeru kuwatumikia na hii (Ilani ya uchaguzi) ndio nakuja kuitekeleza,” amesema.
Mbali na kumshuruku Rais Magufuli kwa kumteua amesema kiongozi mkuu huyo wan chi ni zawadi kutoka kwa Mungu, kwa maelezo kuwa amefanya mambo makubwa ndani ya muda mfupi.
Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Longido, Frank Mwaisumbe amemshukuru rais kwa kumteua na kuahidi kuchapa kazi.
Akiwakaribisha wakuu hao wa wilaya, Gambo amesema, “mmepewa majukumu makubwa kuna tabia ukipewa nafasi unaona kubwa, lakini ukiizoea unaona ya kawaida. Awamu hii ni tofauti lazima utendaji wenu uendane na katiba, sheria na miongozo ya Serikali.”
Comments
Post a Comment