Waziri Mkuu Mstaafu na Mjumbe wa Kamati Kuu CHADEMA, Edward Lowassa ameweka wazi kwamba ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo wataondoka watu wengi kwa kujivua uanachama hivyo amewataka wafuasi wao wasikate tamaa bali vitendo hivyo vizidi kuwatia nguvu.
Lowassa ametoa kauli hiyo kupitiwa ujumbe wa maandishi ikiwa ni katika hali ya kuwafariji wananchi wa jimbo la Monduli ambao Mbunge wao Julius Kalanga, amejuzulu na kujivua uanachama usiku wa kuamkia leo na kutimkia CCM kwa madai ya kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli.
"Nimesikia taarifa za kujiuzulu kwa mbunge wangu wa Monduli Mh Julius Kalanga. Najua wana Monduli wote nikiwemo mimi uamuzi huo umetuhuzunisha na kutuumiza, lakini nawaomba msife moyo hata dakika moja zaidi kitendo hicho cha Kalanga kizidi kutupa nguvu, ari, hamasa na mori zaidi ya kuendeleza mapambano ya kuitafuta demokrasia na mabadiliko ya kweli," Amesema Lowassa.
"Wataondoka kina Kalanga wengi tu lakini kasi ya moto ule jinsi ilivyo hivi sasa ndani ya mioyo ya watanzania ni ya “Moto wa kiangazi” Edward Lowassa.
Lowassa ameongeza kwamba "Hakuna jipya katika hili, ni kawaida kwa wana siasa duniani kuhama vyama vyao na kubadilishana vijiti. Kwasababu zozote zile atakazokuwa amezitoa, hiyo ni haki yake kikatiba. Moto ule tuliyouwasha 2015 hauwezi hata mara moja kuzimwa na mbinu hizi".
Comments
Post a Comment