Waziri wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola amemtaka mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe kujisalimisha kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi kwa maelezo kuwa ametoa kauli za uchochezi.
Lugola ametoa kauli hiyo leo Jumanne Julai 31, 2018 wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Amesema Zitto ametoa kauli za uchochezi na kuwatukana viongozi wa Serikali wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika jimbo la Kilwa Kusini.
Katika mkutano huo Zitto alialikwa na mbunge wa jimbo hilo, Seleman Bungara maarufu Bwege.
“Kosa jingine la Zitto ni kwenda kufanya mkutano eneo ambalo sio la kwake kwa mujibu wa taratibu. Nampa siku mbili ajisalimishe kwa RPC (Kamanda wa polisi mkoa wa Lindi),” amesema Lugola.
“Akikaidi nitamuagiza IGP (Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini-Simon Sirro) amkamate popote alipo. Nilishasema na nitaendelea kusema katika uchaguzi huu na zijazo watu wanaotukana viongozi hawatabaki salama.”
Katika hatua nyingine, Waziri Lugola amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro kumchukulia hatua Mkuu wa Polisi Wilayani Kilwa(OCD) kutokana na kumruhusu Zitto kuendelea kufanya mkutano katika jimbo lisilo lake.
“ Na pia namulekeza IGP achukue hatua kwa mkuu wa polisi wa wilaya ya kilwa ocd, ya kwa nini hakuchukua hatua dhidi ya zitto kwa kuendelea kufanya yale tuliyoyakataza,” amesema.
Comments
Post a Comment