Skip to main content

Featured

Maombolezo: Hii ndiyo Hali Ilivyo Tanzania Bendera Yapepea Nusu Mringoti

Agizo la Rais John Magufuli la Bendera ya Taifa kupepea kwa nusu mlingoti kwa siku tatu kuanzia leo Septemba 22 kufuatia ajali ya kivuko cha MV Nyerere iliyotokea mkoani Mwanza limetekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Mnyeti alivyowaweka ndani wakili, wateja wake



Babati/Dar. Madai ya wakulima kuhusu pembejeo miaka 19 iliyopita yamesababisha wakili maarufu mjini Arusha na wateja wake wanne kuwekwa ndani kwa amri ya mkuu wa mkoa.
Polisi mkoani Manyara iliwashikilia wakili wa kujitegemea, Menrad De Souza na wafanyakazi wanne wa kampuni ya Balton kwa amri ya mkuu wa mkoa huo, Alexander Mnyeti wakituhumiwa kwa uchochezi kupitia mitandao ya kijamii.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Augustino Senga akizungumza na Mwananchi, alisema watu hao walikamatwa juzi na wangeachiwa jana baada ya kukaa ndani kwa saa 48.
Alisema walituhumiwa kutuma taarifa potofu kwenye mitandao ya kijamii kueleza kuwa walifungiwa chumbani kwa amri ya mkuu wa mkoa.
Akizungumzia madai ya kuwafungia ndani, mkuu wa mkoa, Mnyeti alikana akieleza kwamba alikutana nao juzi kutokana na malalamiko ya wakulima kuidai fidia kampuni ya Balton iliyokuwa wakala wa kusambaza pembejeo mwaka 1999.
Alisema kampuni hiyo ilisambaza dawa ya kuua wadudu waharibifu iliyosababisha kahawa kukauka huku kukiwa na taarifa za watu takriban 20 kufariki dunia kwa nyakati tofauti kutokana na kutumia dawa hiyo kunyunyuzia kwenye zao hilo.
Mnyeti alisema tathmini ilifanyika na kuonyesha kuwa wakulima walipata hasara ya Sh248 milioni, lakini Balton imekuwa ikiwazungusha kuwalipa, hivyo wahusika walikuwa wakitafutwa na polisi.
Alisema kampuni hiyo ilitaka kuwalipa kati ya Sh30 milioni na Sh60 milioni.
Mnyeti alisema alipokutana na wakili na wateja wake juzi, aliwapa dakika 30 za kuzungumza na viongozi wa kampuni hiyo waliopo Dar es Salaam, ndipo taarifa ziliposambazwa kuwa wamefungiwa chumbani. Alisema baada ya taarifa kusambaa mitandaoni aliagiza walazwe mahabusu kwa masuala ya kisheria na wataachiwa kwa namna itakavyoonekana inafaa.
Rais TLS alaani
Kutokana na tukio hilo, rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume alilaani kushikiliwa wakili huyo na wateja wake.
Akizungumza na wanahabari Dar es Salaam, Fatma alisema ofisi ya TLS Arusha inafuatilia suala la wakili huyo aliyekuwa akitekeleza majukumu yake. Alisema Serikali na viongozi wana wajibu wa kuheshimu sheria, utaratibu na mikataba ya kimataifa.
Fatma alisema polisi wanao wajibu wa kumhoji mkuu wa mkoa au wilaya sababu za kumkamata na kumuweka ndani mtu chini ya kanuni za jeshi hilo.
Alisema sheria hailengi kumpatia mamlaka mkuu wa mkoa au wa wilaya kumweka ndani mtu kwa saa 48, badala yake hutumika kwa mtu aliyetenda uhalifu kushikiliwa kabla ya polisi kushirikishwa.
Fatma alisema baada ya saa 48, mtu aliyekamatwa anatakiwa kupelekwa mbele ya hakimu vinginevyo aachiwe huru.
Alisema kutokana na mwenendo wa matumizi mabaya ya madaraka miongoni mwa wakuu wa mikoa na wa wilaya, TLS imeshafungua kesi mahakamani kuomba tafsiri ya sheria ili kukomesha utamaduni wa watu kukamatwa na kuwekwa ndani saa 48 kinyume cha haki walizonazo kisheria.

Comments

Popular Posts