Licha ya aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Ukonga, Mwita Waitara (Chadema) kutoa sababu lukuki za kukihama chama hicho, mjadala mkubwa kwa sasa ni namna mwanasiasa huyo anavyobadilikabadilika katika kauli na matendo yake.
Ingawa alikuwa mwana CCM tangu mwaka 1998, Waitara alianza kuwika mwaka 2008 alipoamua kujiengua CCM na kujiunga na Chadema wakati uchaguzi mdogo wa jimbo la Tarime.
Uchaguzi huo ulifanyika kufuatia kifo cha ghafla cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Chacha Wangwe aliyefariki dunia kwa ajali ya gari.
Waitara aliiacha CCM kwenye kipindi kigumu katikati ya mapambano ya kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo la Tarime na kusababisha kushindwa katika uchaguzi huo ambao Chadema ilishinda kwa kishindo.
Hata hivyo, miaka 10 baadaye, Waitara yuleyule amebadilika, sasa haitaki tena Chadema, anarudi CCM akishusha lawama zilezile zilizomtoa kwenye chama chake cha awali.
Licha ya kudai kukosa uhuru wa kufanya kazi kama mbunge ikiwa ni pamoja na kuzungumza na wakuu wa mikoa na wilaya, Waitara akiwa Chadema ndiye aliyepeleka hoja binafsi bungeni akiwalalamikia baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya kulidharau Bunge.
Hoja hiyo, ilisababisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Arumeru (sasa Mkuu wa Mkoa wa Manyara), Alexander Mnyeti kuitwa na Kamati ya Bunge ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge kujieleza, Februari 2017.
“Kimsingi hiki ni kipindi ambacho Bunge linaingia kwenye majaribu makubwa ya kudharauliwa, kusiginwa kwa haki zake. Inawezekanaje Kamati ya Bunge inajadili, inawasilisha, tunakula kiapo humu tunaomba Mungu, halafu mkuu wa wilaya anasema hawa ni wapuuzi na mkuu wa mkoa anasema hawa wanasinzia tu, hawanitishi hawanibabaishi,” anasema Waitara alipokuwa akichangia hoja bungeni.
Waitara alieleza kuwapo kwa wabunge waliopigiwa simu na mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam akasema hawa wabunge hawanitishi na hawanibabaishi, jambo alilosema linakiuka Sheria ya Haki, Madaraka ya Bunge.
Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge alisema hoja za Waitara zinakubaliana na Sheria ya kinga, madaraka na haki za Bunge sura ya 296 ya Sheria za Jamhuri ya Muungano.
Mbali na suala hilo, Waitara akiwa Chadema alionyesha kuchukizwa na usaliti ndani ya chama hicho, hasa pale alipomwandikia Zakayo ambaye ni mtoto wa marehemu Chacha Wangwe aliyeamua kuachana na Chadema na kuhamia CCM.
“Zakayo Chacha Wangwe umekimbia mapambano kwa sababu nyepesi sana. Umewasaliti wana Turwa! Baba yako alifia kwenye uwanja wa mapambano. Nilikuunga mkono kwa sababu ya baba yako, nimwombee mdogo wako Bob achukue mikoba ya marehemu Chacha Wangwe,” aliandika Waitara kwenye ukurasa wake wa Instagram.
Mwita Mwikwabe Waitara alizaliwa katika kijiji cha Kangaliani, Wilaya ya Tarime mkoani Mara, Julai 17, 1976.
Aliingia katika siasa kwa mara ya kwanza akiwa anasoma Shule ya Sekondari Azania mwaka 1998 baada ya mkutano wa viongozi wa CCM waliofika shuleni kwao.
Akiwa Chuo kikuu cha Dar es Salaam, Waitara anatajwa kuwa miongoni mwa washiriki wa mgomo wa wanafunzi mwaka 2002 uliosababisha chuo kufungwa.
Aliwahi kuwa Katibu wa UVCCM Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam na baadaye kuhamishiwa Tanga kwa nafasi hiyohiyo na kupanda ngazi kuwa Katibu wa UVCCM Mkoa wa Tanga.
Alihamishiwa Dar es Salaama awe Msaidizi wa Mwenyekiti UVCCM Taifa, lakini aliona ni udhalilishaji kutokana na kutokuwa na nafasi tena ya kuingia vikao vya maamuzi, akahama chama hicho na kuingia Chadema mwaka 2008.
Baada ya Chadema kulitetea jimbo la Tarime mwaka 2008, aliteuliwa kuwa Ofisa wa Sera na Utafiti wa Chadema hadi 2014.
Mwaka 2010 aligombea ubunge wa Tarime kwa tiketi ya Chadema baada ya kushinda kwenye kura za maoni, lakini aliangushwa na mgombea wa CCM, Nyambari Nyangwine.
Mwaka Agosti 2014, Waitara aliingia katika kinyang’anyiro cha uenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mara ambako alikumbana na kigingi baada ya kuwekewa pingamizi na jina lake kuondolewa katika orodha ya wagombea kwa tuhuma za kuhusika kuandaa waraka wa kutaka kumwengua Freeman Mbowe katika nafasi ya uenyekiti.
Waraka huo ambao ulisababisha pia viongozi wawili, aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba na aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu, Profesa Kitila Mkumbo kufukuzwa uanachama, ulieleza kuwa kuna kiongozi mwingine waliyeshirikiana naye aliyetajwa kama M2, kuwa alikuwa amebaki makao makuu ya Chadema, ambaye alidaiwa ni Waitara.
Hata hivyo, Waitara alikana tuhuma hizo akisema kilichofanyika ni njama za kutaka tu kumwondoa asigombee nafasi hiyo.
“Tuhuma hizi ni kubwa, zimenichafua, nataka huyo anayesema mimi ni M2 nilihusika na kina Zitto aje athibitishe na atoe vielelezo,” alisema Waitara alipohojiwa na Mwananchi wakati huo. Hapo ndipo alibwaga manyanga mkoani Mara na kuhamishia nguvu jijini Dar es Salaam.
Mwaka huohuo wa 2014 aligombea na kushinda uenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kivule (wakati huo katika Kata ya Kitunda – sasa Kata ya Kivule) na mwaka 2015 aligombea ubunge katika jimbo la Ukonga na kumshinda mgombea wa CCM, Jerry Silaa.
Kwa uamuzi huo wa Waitara amekuwa mbunge wa pili wa Chadema na wa tatu wa upinzani kuhama chama na kujiunga na CCM. Wengine wa Dk Godwin Mollel (Chadema-Siha) na Maulid Mtulia (CUF-Kinondoni).
Comments
Post a Comment