Mkuu wa wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani Mh. Jokate Mwegelo amekutana na mwanafunzi Salma Salum wa shule ya msingi Kizota A ambaye ameongoza katika mtihani wa kipimo cha kupata ufadhili wa masomo.
Jokate amemtia moyo na kumuahidi kumsaidia kutimiza ndoto zake mwanafunzi huyo wa darasa la saba ambaye ndoto yake ni kufaulu vizuri mitihani yake na kuchaguliwa kwenda kusoma shule za vipaji maalum.
Mbali na hilo Mh. Jokate kwa kushirikiana na Afisa Elimu Msingi wilayani humo Shomari Banne, wamkutana na uongozi wa shule ya Luther Girls iliyopo wilayani Bagamoto ambayo ndiyo imeendesha mtihani huo na wamemwahidi kuwa watamchukua Salma kwa ajili ya kumwendeleza.
''Uongozi wa Luther Girls umekuja wilayani kwetu na kuwapa mtihani wa majaribio wanafunzi wa darasa la 7 na Salma amefanya vizuri kuliko wote na wamemzawadia 'scholarship' hivyo sasa ataamua yeye kama ataichukua ama atakwenda shule kongwe za serikali maana naamini atafaulu vizuri tu kwenye mtihani wa darasa la 7,'' amesema Jokate.
Katika mtihani huo imeelezwa Salma Salum amefaulu vizuri haswa kwenye masomo ya Kiingereza na Hisabati hivyo kuwa miongoni mwa wanafunzi zaidi ya 10 ambao watajiunga na shule ya Luther Girs kidato cha kwanza mwakani na kulipiwa kila kitu.
Comments
Post a Comment