Skip to main content

Featured

Maombolezo: Hii ndiyo Hali Ilivyo Tanzania Bendera Yapepea Nusu Mringoti

Agizo la Rais John Magufuli la Bendera ya Taifa kupepea kwa nusu mlingoti kwa siku tatu kuanzia leo Septemba 22 kufuatia ajali ya kivuko cha MV Nyerere iliyotokea mkoani Mwanza limetekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Jukata wataja dawa kukomesha wanaohama vyama, kuwalinda wanaofukuzwa



Dar es Salaam. Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata) limependekeza mabadiliko kwenye sheria za uchaguzi ili kuruhusu wabunge na madiwani wanaovuliwa uanachama kuendelea na nafasi zao hadi  watakapomaliza muda wao wa miaka mitano.
Jukwaa hilo pia limependekeza wabunge na madiwani wanaojivua uanachama, nafasi zao kuzibwa na walioshika nafasi ya pili katika uchaguzi, si kurejea uchaguzi kama ilivyo sasa.
Akiwasilisha mapendekezo hayo leo Ijumaa Agosti 30, 2018 jijini Dar es Salaam mwenyekiti wa zamani wa Jukata, Deus Kibamba amesema sheria imzuie mtu aliyejivua uongozi kutogombea tena kwa miaka 10.
"Hii italeta heshima kwa nafasi ambazo wananchi wanachagua na itaondoa hii ya sasa ya viongozi kuhamahama kila kukicha," amesema Kibamba.
Amebainisha kwamba sheria hiyo imlazimishe mgombea kusaini kiapo kwamba atatumikia nafasi hiyo mpaka muda wake utakapokwisha.
"Mazingira pekee ambayo tunaona kuna haja ya kufanya uchaguzi mdogo ni pale mbunge au diwani anapofariki dunia. Vinginevyo hakuna sababu yoyote, viongozi watapatikana kwa njia ambayo haina gharama," amesema.

Mapendekezo mengine yaliyotolewa na jukwaa hilo wakati wa mkutano na wahariri wa vyombo vya habari ni kubadilisha jina la Tume ya Uchaguzi (NEC) na muundo wake wa utendaji kazi.

Kibamba amesema jukwaa linapendekeza jina la tume hiyo kuwa Tume Huru ya Uchaguzi Tanzania na mwenyekiti wake asiwe sehemu ya sekretarieti.

Kuhusu suala la mgombea binafsi, Kibamba amesema Serikali itekeleze uamuzi wa mahakama ambao uliitaka kufanya mabadiliko ya Katiba na kuruhusu wagombea binafsi.

"Serikali itekeleze hukumu za mahakama za ndani na mahakama ya Afrika ambazo zimeitaka Tanzania kubadili katiba yake ili iruhusu haki mbalimbali ikiwemo fursa ya mgombea huru," amesema.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa Jukata, Hebron Mwakagenda amesema wanaandaa jedwali lenye mapendekezo hayo kisha wataliwasilisha bungeni kupitia wabunge ili yaingizwe kwenye mfumo wa sheria.

"Tumeanza mazungumzo na baadhi ya wabunge ambao watatusaidia kufikisha hoja hii bungeni. Tunaamini sheria za uchaguzi zikifanyiwa badadiliko kwenye mambo haya, tutakuwa na mfumo mzuri wa uchaguzi,” amesema Mwakagenda.

Comments

Popular Posts