Mbunge wa Malindi (CUF), Ally Saleh
Dar es Dalaam. Mbunge wa Malindi (CUF), Ally Saleh amedai Chama cha Mapinduzi (CCM) kimehamishia nguvu visiwani Zanzibar kuwashawishi wanachama wa vyama vya upinzani wajiunge nacho.
Akizungumza na MCL Digital leo Jumatano Agosti Mosi, 2018, Saleh amesema yeye ni miongoni mwa wanaoshawishiwa kujiunga na chama hicho tawala.
Kabla ya kuzungumza na MCL Digital, Saleh alitoa tuhuma hizo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter huku CCM visiwani humo kikimjibu, kumtaka kutoweweseka badala yake, atulie kushuhudia wimbi la wana CUF watakaokihama chama hicho.
Katika ukurasa wake huo, mbunge huyo aliandika alichoelezwa na aliyemtambulisha kuwa ni mgeni (kutoka CCM) aliyekwenda nyumbani kwake na jinsi alivyomjibu.
Mgeni: Sijatumwa, mimi mwenyewe
Mgeni: Tunataka uje kujiunga CCM
Saleh: Shuka ngazi haraka na mlango wa nyumba yangu usiujue
Akifafanua zaidi alipozungumza na MCL Digital Saleh amesema, “ni kweli alikuja nyumbani kwangu, alipofika sikuwa nikimjua lakini alipoanza kujitambulisha ndio nikamjua.”
“Mtu huyo ni wa hapa Zanzibar lakini kwa sasa sitamtaja majina yake ila akibisha nitamtaja. Labda niseme tu kwamba, mimi sinunuliki, nimezaliwa upinzani na sitarajii kwenda CCM.”
Amesema alimtaka kigogo huyo kutokurudia kumshawishi kwa maelezo kuwa yeye si kama wengine wanaoshawishika.
Akizungumza na MCL Digital msemaji wa CCM- Zanzibar, Catherine Nao amemtaka Saleh kumtaja mtu huyo aliyekwenda kumshawishi, “wanaokuja CCM wanakuja si kwa ushawishi, wanakuja wao wenyewe kwa kuona mambo mazuri anayoyafanya.”
“Hakuna anayeshawishiwa, Rais Magufuli (John) yale anayoyafanya ndio anawafanya wajiunge na CCM, lakini niseme tu, Septemba 15, 2018 tukiwa tunazindua kampeni za uwakilishi wa Jang’ombe, kuna wana CUF wengi watajiunga na CCM, subirini mtaona.”
Comments
Post a Comment