Mwenyekiti wa Bodi ya Nation Media Group (NMG), Wilfred Kiboro akizungumza na wafanyakazi wa Mwananchi Communications Limited (MCL), jijini Dar es Salaam leo.
Dar es Salaam. Waandishi wa habari wamehimizwa kuendelea kuchapa kazi na kutovunjika moyo ingawa tukio la kutoweka kwa mwandishi mwenzao, Azory Gwanda ni tukio la kuhuzunisha na kuzusha hofu.
Pia, wametiwa moyo wakiambiwa kuwa kazi wanayofanya ni yenye changamoto nyingi ikiambatana na misukosuko na hata kukatisha tamaa.
Hayo yamebainishwa leo Agosti 31 na Mwenyekiti wa Bodi ya Nation Media Group (NMG), Wilfred Kiboro wakati alipokuwa akizungumza na wafanyakazi wa Mwananchi Communications Limited (MCL) Tabata.
Alisema duniani kote waandishi wa habari wana jukumu la kuitumikia jamii na kuendelea kusema kweli pasipo kutia chumvi wala kupendelea upande wowote.
Hata hivyo alisema inapotokea matukio kama yale ya Azory waandishi wanakuwa katika wakati mgumu.
“Hili tukio la Azory si jambo jema na linahuzunisha. Huzuni yake inakuwa kubwa kwa sababu hujui kama kafa au yuko hai. Lakini tutambue kuwa duniani kote waandishi wa habari wamekuwa wakikumbana na changamoto nyingi jambo la msingi ni kutokata tamaa,” alisema.
Alisema ingawa matukio ya namna hiyo yamekuwa yakitokea duniani lakini hiyo haimanishi waogope kusema ukweli kwa yale yanayojitokeza kwenye maeneo yao.
“Sisi jukumu letu ni kusema ukweli... tuandike kwa njia ya haki na kweli bila kumwogopa mtu na mkifanya hivi naahidi tutaendelea kuwaunga mkono na daima tutakuwa nyuma yenu,” alisema.
Alisisitiza kuwa kitendawili cha kutojua kama mwandishi huyo yuko hai au la ndicho kinachoendelea kuitesa familia yake na hata kwa wanataaluma wenzake.
Azory aliyekuwa akiandikia gazeti la Mwananchi alitoweka katika mazingira ya kutatanisha tangu Novemba, 2017.
Mbali ya hilo, mwenyekiti huyo aliwaasa waandishi wa habari kutotumbukia kwenye mitego ya rushwa akisema mwenendo wa namna hiyo utawafanya wapoteze maadili mbele ya jamii na hivyo kushindwa .
“Epukeni kupokea hizi bahasha za kaki na ili aundike habari yenye ukweli lazima suala hili ulizingatie. Mna jukumu kubwa la kuijenga nchi hivyo vitendo kama hivyo vinaweza kuwawekeni kwenye mazingira magumu ya kusema ukweli,” alisema.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Francis Nanai alisema kampuni imekuwa ikichukua hatua za kuboresha huduma zake ili kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia yanayoendelea kushuhudiwa sasa.
“Tuko kwenye kipindi cha mpito kuelekea ulimwengu wa digitali na sisi huduma zetu zinazingatia zaidi hilo ili kuona wasomaji wetu wanaendelea kutusoma katika kiwango kilekile,” alisema.
Comments
Post a Comment