Skip to main content

Featured

Maombolezo: Hii ndiyo Hali Ilivyo Tanzania Bendera Yapepea Nusu Mringoti

Agizo la Rais John Magufuli la Bendera ya Taifa kupepea kwa nusu mlingoti kwa siku tatu kuanzia leo Septemba 22 kufuatia ajali ya kivuko cha MV Nyerere iliyotokea mkoani Mwanza limetekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Wadau: TFF iiachie Takukuru



Dar es Salaam. Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limetakiwa kuitumia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza viongozi inaowatuhumu kwa ubadhirifu wa fedha.
Kauli hiyo imetolewa na wadau wa michezo muda mfupi baada ya Mjumbe wa Kamati ya Utendaji TFF, Mbasha Matutu kufungiwa maisha kujihusisha na masuala ya soka.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti jana, wadau wa soka walisema umefika wakati TFF kutumia vyombo huru ikiwemo Takukuru kuchunguza tuhuma zinazowakabili maofisa wake.
Walisema Takukuru ni chombo kilichoundwa kwa mujibu wa sheria za nchi ambacho kina wajibu wa kufanya uchunguzi hasa zinapoibuka tuhuma za ubadhirifu wa fedha.
Wakili Damas Ndumbaro aliyewahi kukumbana na rungu la kufungiwa kujihusisha na soka miaka saba, alisema kabla ya TFF kutoa adhabu kwa wahusika Takukuru ipewe nafasi ya kufanya uchunguzi kwa watuhumiwa.
Ndumbaro mmoja wa wadau wakubwa katika soka, alidokeza Takukuru ina wigo mpana wa kubaini mianya ya rushwa kwa kuwa ni chombo huru na kinasimamiwa na watalaamu waliobobea katika eneo hilo.
Mwanasheria huyo nguli alisema kanuni ya kumfungia mtu kujihusisha na soka ipo Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
“Awali sheria hii hapa kwetu ilitumika kwa waliokuwa wakipambana na ubadhirifu ndio wanafungiwa, lakini sasa imeanza kutekelezwa. Ni vizuri ingefikia mahali hata Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ingekuwa inahusishwa kwani haizuii mtu aliyefanya ubadhirifu kupelekwa huko. Japo madhara yanakuwa makubwa zaidi kwa aliyefanya ubadhirifu kwa kuwa atafungiwa na jela atakwenda,” alisema Ndumbaro.
Aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa TFF, Frederick Mwakalebela alisema kitendo cha kumfungia mtu maisha kujihusisha na soka ni suala kubwa katika mustakabali wa mchezo huo nchini.
“Unajua sitaki kuingia kwa undani kujiuliza kilichosababisha kufungiwa maisha, lakini adhabu hiyo ni jambo kubwa kama imerahisishwa,” alisema Mwakalebela.
Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Idd Kipingu alisema adhabu ya kumfungia mtu maisha kujihusisha na soka ni kubwa kuliko nyingine zote, hivyo kabla haijatekelezwa wahusika wana wajibu wa kutafakari kabla ya kuchukua hatua.
“Kuna wengine mpira ni sehemu yao ya maisha, hivyo kumfungia maisha ina maana pana kidogo, apewe muda wa kujitetea, kujieleza na hata historia yake ya huko iangaliwe na ithibitike kwelikweli isifike mahala pa kuoneana, itakapothibitika basi afungiwe na isifanyike kwa baadhi ya watu na wengine wanaachwa,” alisema Kipingu.
Rais wa TFF Wallace Karia, aligoma kuzungumzia sakata la Matutu na alimtaka mwandishi kuwasiliana na Katibu Mkuu Wilfred Kidao.
“Mimi sipo ofisini siwezi kuzungumzia suala hilo, nipo katika ziara na waziri na watu wengine wa Bungeni, anayeweza kuzungumzia hayo ni Katibu Mkuu,” alisema Karia kwa simu.
Adhabu ya kifungo cha maisha iliyotolewa kwa Matutu anayewakilisha Kanda za Shinyanga na Simiyu, imewahi kuwakumba vigogo wengine wawili wa TFF.
Hata hivyo, adhabu ya kigogo huyo aliyekumbana na rungu Jumatatu wiki hii, imeacha wingu zito katika mustakabali wa soka nchini.
Kamati ya Maadili ya TFF chini ya Mwanasheria Hamidu Mbwezeleni, ilimtia hatiani Matutu kwa makosa matatu ya kimaadili yaliyochangia kupewa adhabu hiyo baada ya kufanyika kikao Jumamosi, Agosti 25 jijini.
Makosa matatu yaliyomtia hatiani Matutu na kusababisha kupewa kifungo cha maisha ni kushindwa kutekeleza majukumu, ubadhirifu, kughushi na kuiba kinyume na kanuni za maadili na Ligi Kuu.
Kiongozi huyo anadaiwa kufanya makosa hayo yaliyosababisha kupotea kwa fedha zilizotajwa kufikia Sh16 milioni zilizotokana na mapato ya michezo miwili ya Ligi Kuu iliyochezwa Uwanja wa Kamabarage mkoani Shinyanga uliohusisha Stand United dhidi ya Simba na Prisons msimu uliopita.
Matutu anakuwa kiongozi wa tatu kufungiwa maisha kujihusisha na masuala ya soka tangu uongozi wa TFF chini ya Rais Wallace Karia ulipoingia madarakani Agosti 12, mwaka jana adhabu ambazo zimeacha sintofahamu kwa wadau wa michezo nchini.
Kabla ya Matutu, kamati ya maadili iliwafungia aliyekuwa Makamu wa Rais wa TFF, Michael Wambura na aliyekuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya shirikisho hilo anayewakilisha Kanda ya Lindi na Mtwara, Dastan Nkundi kwa makosa ya kughushi.

Comments

Popular Posts