Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina
Morogoro\Dar. Wakati Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally akieleza kumwita waziri mmoja anayemiliki ekari 1,000 za ardhi mkoani Morogoro, madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Morogoro wamewahi kumuomba Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kuingilia kati mgogoro uliodumu kwa miaka saba baina Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina na wananchi wa Kijiji cha Dala na Kongwa.
Mgogoro huo ni wa madai kuwa waziri huyo amechukua mashamba ya wananchi hao ekari 700 na nyingine 300.
Ombi hilo lilitolewa Juni 8 mwaka huu na mwenyekiti wa baraza la madiwani wa halmashauri hiyo, Kibena Kingo baada ya Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Morogoro, Jasmine Tiisekwa kuitaka halmashauri hiyo kutoa taarifa ya namna mgogoro huo unavyoshughulikiwa.
Hata hivyo Waziri Mpina alipoulizwa leo Ijumaa Juni 31 kuhusu malalamiko ya wananchi hao na yeye kuhusishwa na mashamba hayo alitaka majungu yaachwe na katibu mkuu aulizwe.
“Hayo unayouliza ni majungu, acha majungu bana na kama katibu mkuu ameongea si umuulize yeye katibu mkuu.
Alipoulizwa kama mshamba hayo ni ya kwake Waziri Mpina alikata simu.
Hata hivyo, katika kikao cha halmashauri ya hiyo, Tiisekwa alidai taarifa alizonazo zinaonyesha kwamba mgogoro huo umefikia hatua mbaya kwani baadhi ya wakulima wameharibiwa mazao yao ukiwemo mpunga na mahindi na watu wanaodaiwa kuwa ni walinzi wa shamba hilo la Waziri Mpina lenye ukubwa wa ekari 700.
“Nikiwa kwenye uzinduzi wa kituo cha mabasi cha Msamvu uliofanywa na Mhe Rais, nilifuatwa na mama mmoja ambaye ni mlemavu huku akilia na kuniambia kwamba shamba lake la mpunga la ekari tano limeharibiwa na watu wanaodaiwa kuwa ni walinzi wa shamba la Waziri Mpina, hivyo naomba kupata majibu mgogoro huu umetatuliwa vipi? Aliuliza Tiisekwa.
Tiisekwa ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii alisema kuwa sheria ya ardhi hairuhusu halmashauri za vijiji kutoa maeneo zaidi ya ekari 50 na kwamba mwenye mamlaka ya kutoa ekari hizo 700 ni kamishna wa ardhi.
Awali akitoa ufafanuzi wa mgogoro huo mkurugenzi wa halmashauri hiyo wakati huo kabla ya kuhamishwa, Sudi Mpili alikiri kuwepo kwa mgogoro huo na alisema kuwa mgogoro wa kwanza ulitokea baada ya Waziri Mpina kujenga tuta kwenye Mto Mbwade kwa ajili ya kuelekeza maji kwenye shamba lake la ekari 300 lililopo Kata ya Bonye ambalo nalo umiliki wake una mashaka.
Alidai kuwa Waziri Mpina alitumia ujanja kwa kuandika majina sita ya watu tofauti tofauti na kuomba ekari 50 kwa kila jina kwa lengo la kumiliki ekari 300 jambo ambalo ni kinyume cha sheria kwani hata alipotakiwa kuwapeleka watu hao kwenye serikali ya kijiji kuwatambua alishindwa kufanya hivyo.
Mpili alidai walinzi wa Waziri Mpina wamekuwa wakilinda tuta hilo usiku na mchana kwa kutumia silaha za moto huku wakulima waliokuwa wakitegemea maji hayo kwa kilimo cha umwagiliaji wakikosa na hivyo kusababisha mazao yao kuharibika.
Mkurugenzi huyo alidai kuwa mgogoro mwingine ulitokea katika Kijiji cha Dala Kata ya Mvuha baada ya Waziri Mpina kuiomba serikali ya kijiji shamba la hekari 700 hata hivyo kabla ya maombi hayo kupitishwa na mkutano mkuu wa kijiji Waziri Mpina alianza kulima na kufukuza baadhi ya wakulima waliokuwa wakilima katika shamba hilo na wengine kuharibu mazao yao.
Alidai kuwa Waziri Mpina alitumia mbinu ya kuwarubuni baadhi ya wajumbe wa serikali ya Kijiji cha Dala ambao walikubali kumuonyesha eneo hilo la hekari 700 bila ya kushirikisha mkutano wa kijiji jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Diwani wa Viti Maalumu Kata ya Mvuha, Rehema Jongo alimshauri mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuandaa mkutano wa kijiji na kumshirikisha Waziri Mpina kwenye mkutano huo ili mgogoro huo uweze kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo.
Jongo alisema kuwa kitendo alichokifanya Waziri Mpina cha kupora ardhi ni uvunjaji wa sheria na ametumia madaraka yake vibaya kwa kuwapora haki wananchi na kwamba baraza la madiwani litahakikisha mgogoro huo unatatuliwa kwa mujibu wa sheria na sio cheo cha mtu.
Comments
Post a Comment