Skip to main content

Featured

Maombolezo: Hii ndiyo Hali Ilivyo Tanzania Bendera Yapepea Nusu Mringoti

Agizo la Rais John Magufuli la Bendera ya Taifa kupepea kwa nusu mlingoti kwa siku tatu kuanzia leo Septemba 22 kufuatia ajali ya kivuko cha MV Nyerere iliyotokea mkoani Mwanza limetekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Ni huzuni kubwa



Dar/Ukerewe. Giza limetanda. Ndivyo unavyoweza kusema kufuatia ajali ya kivuko cha Mv Nyerere iliyozama juzi mchana katika Kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe, Mkoa wa Mwanza, huku idadi ya waliofariki dunia mpaka jana saa moja usiku ikifikia 136.
Jana, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alifika eneo la ajali na kuzungumza na wananchi huku Rais John Magufuli akitangaza siku nne za maombolezo na bendera kupepea nusu mlingoti na kueleza jinsi kivuko hicho kilivyokuwa kimepakia watu kupita kiasi pamoja na bidhaa mbalimbali yakiwemo mahindi.
Kwa mujibu wa Rais Magufuli kivuko hicho kilichokuwa kikitokea katika Kisiwa cha Bugolora kuelekea Kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe kilikuwa kimepakia zaidi ya abiria 100 wanaotakiwa.
Kufuatia hali hiyo, kiongozi mkuu huyo wa nchi aliagiza wahusika wote wa ajali hiyo wakamatwe, akiwemo nahodha wa kivuko hicho anayedaiwa kuwa hakuwa katika kivuko wakati kikizama, badala yake alikuwa amempa mtu mwingine kuendesha.
Katika ajali hiyo, wapo waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki zaidi ya watano huku manusura wakieleza jinsi walivyonusurika na kifo, wakiwemo watu wawili waliokutwa hai wakielea huku wameshikilia tairi la gari.
Akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli alidokeza mambo yaliyosababisha kutokea kwa ajali hiyo ikiwamo tetesi za nahodha wa kivuko hicho kuwa hakuwa yeye.
Alisema kivuko hicho kina uwezo wa kubeba watu 100 au 101 lakini kilibeba watu zaidi.
“Taarifa za awali tulizopata kutoka kwa mashuhuda, kivuko hicho mpaka sasa hivi (saa 1.14 usiku) maiti zilizopatikana zilikuwa 131 na majeruhi 40, hapo tayari imefika 171 na maiti bado wako ndani,” alisema.
Alisema kuna taarifa kuwa kivuko kilikuwa kimepakia mahindi mengi, bia na soda pamoja na vifaa mbalimbali.
“Hata aliyekuwa anaendesha hiyo feri siyo nahodha mwenyewe, yeye hakusafiri na inadaiwa amekamatwa na wote wakamatwe,”aliagiza Rais.
Pia, aliagiza uchunguzi ufanyike na hatua za kisheria zichukuliwe kwa wote waliohusika.
Rais Magufuli alisema tayari Majaliwa, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Hussein Mwinyi, vyombo vya ulinzi na usalama kama Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), jeshi la wana maji, Polisi, Sumatra na kamati ya ulinzi na usalama ya Mwanza, Kamati ya maafa ya ofisi ya waziri mkuu, “Wako kule wanaendelea na operesheni ya kutoa miili iliyonasa ndani ya kivuko.”
Katika hotuba yake ya takribani dakika kumi, Rais Magufuli aliwataka wanasiasa kutokutumia msiba huo kisiasa.
“Tuviache vyombo vinavyohusika na uchunguzi vifanye kazi yake, vifanye uchunguzi vitatoa taarifa. Wale watakaobainika watafikishwa mahakamani na vifo vya Watanzania tusivitumie kisiasa, vyombo vyenye utaalamu vitatoa taarifa yake,” alisisitiza.
Akizungumza na wananchi wa Ukara baada ya kuwasili na helkopta akitokea Dodoma alikokatisha ziara yake ya kikazi, Majaliwa alikuwa ameambatana na Mkuu wa Majeshi, Venance Mabeyo, aliwataka Watanzania kuwa watulivu wakati uokoaji wa miili ukiendelea.
Akizungumza baada ya kutembelea kituo cha afya ilikohifadhiwa miili hiyo, alisema mpaka jana saa 1:06 usiku miili ya watu 72 ilikuwa imeshatambuliwa kati ya 136 iliyoopolewa.
“Kivuko hiki kina uwezo wa kupakia tani 25 na abiria 100 hadi 101, kwa hali inavyoendelea kilizidisha abiria na mizigo,” alisema Majaliwa akibainisha kuwa kivuko hicho kilifanyiwa ukarabati kwa kufungwa injini mbili mpya.
Jana, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi alizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma na kubainisha kuwa Serikali imeagiza wahusika wote kwenye uendeshaji na usimamizi wa kivuko hicho na viongozi wa Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) kukamatwa na kuhojiwa ili kubaini ushiriki wao.
Hata hivyo, jana Mwananchi lilipozungumza na Mkurugenzi wa Sumatra, Johansen Kahatano alisema kwa sasa udhibiti wa vyombo vya majini havipo katika mamlaka hiyo bali unafanywa na Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (Tasac).
Balozi Kijazi alisema uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha ajali hiyo ni kivuko hicho kubeba abiria wengi kuliko uwezo wake.
“Mambo mengine yanazuilika, naamini kama viongozi wangechukua hatua mapema janga hili lingeweza kuzuilika. Kila mahali panapohusisha maisha ya binadamu, tuwe makini, tuwe macho maisha ya Watanzania yasihatarishwe kwa uzembe,” alisema Balozi Kijazi

Comments

Popular Posts