Skip to main content

Featured

Maombolezo: Hii ndiyo Hali Ilivyo Tanzania Bendera Yapepea Nusu Mringoti

Agizo la Rais John Magufuli la Bendera ya Taifa kupepea kwa nusu mlingoti kwa siku tatu kuanzia leo Septemba 22 kufuatia ajali ya kivuko cha MV Nyerere iliyotokea mkoani Mwanza limetekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Nyota zinavyomng’arisha Raila Odinga siasa za 2022



Raila Odinga

Raila Odinga
Rais Uhuru Kenyatta na hasimu wake wa kisiasa Raila Odinga wanaendelea kukuza na kupalilia uhusiano wao mpya kwa hali na mali.
Viongozi hao uhudhuria mikutano rasmi na ile ambayo si rasmi pamoja na kusifiana huku makamu wa Rais, William Ruto akitazama kwa uchungu.
Hadi Februari mwaka huu, chama tawala cha Jubilee kilikuwa kinaimba pambio la “Baada ya Uhuru, Ruto ataingia madarakani kwa miaka mingine 10.”
Wimbo huo ulifikia kikomo pale Uhuru na Raila walipokutana na kuamua kushirikiana kuleta utangamano na maendeleo. Hii ilimkereketa Ruto na wafuasi wake na kuukejeli urafiki baina ya Rais na kiongozi huyo wa ODM.
Lakini sasa, ni wazi kwamba Uhuru na Raila wataendelea kushirikiana hadi 2022 na kuendelea mbele.
Mnamo Agosti 22 wakati wa maadhimisho ya makumbusho ya miaka 40 tangu Rais Mzee Jomo Kenyatta kuaga dunia, Uhuru alimsifu Raila akimwita “ndugu yangu” lakini hakutaja lolote kuhusu makamu wake wa Rais ambaye pia alikuwa kwenye makumbusho hayo.
Baadaye, Rais alielekea Marekani kukutana na Rais Donald Trump huku Raila akiabiri ndege kuzuru Ujerumani ambapo atakutana na Wakenya wanaoishi katika nchi hiyo, miongoni mwa shughuli nyingine muhimu.
Ushirikiano wa wawili hao unatarajiwa kuimarika zaidi wakati kongamano la kuweka msingi dhabiti kati ya Rais na Raila litakapofanyika Septemba 10 jijini Nairobi.
Kongamano hilo lilikuwa limekumbwa na misukosuko kwa sababu ya uhaba wa pesa. Wizara ya Fedha imejizatiti kutafuta pesa za ufadhili kongamano hilo.
Rais na kiongozi huyo wa upinzani wamesema ushirikiano wao unatarajia kujenga madaraja ya amani miongoni mwa Wakenya baada ya miaka mingi ya uhasama na siasa za kikabila.
Wakati huohuo, viongozi hao huenda wanapanga jinsi siasa za 2022 zitakavyokuwa. Raila Odinga ameonyesha dalili za kuwania urais kwa mara ya tano na pengine wa mwisho. Wakati huo atakuwa na umri wa miaka 77.
Wanasiasa mbalimbali wanaamini kuwa Raila ana nafasi nzuri zaidi ya kuwania uongozi 2022 kwa sababu ya uhusiano wao mpya na Rais Uhuru.
Wanasiasa wa upinzani wakiwemo wafuasi wa Raila wanasema kiongozi huo ana risasi ya mwisho ya kufyatua katika vita vya 2022 vya Ikulu.
Mshauri wa masuala ya kisheria wa Raila, James Orengo na kaka yake kinara huyo wa ODM wameashiria kwamba Agwambo (Raila), kama anavyojulikana na wafuasi wake huenda anatayarisha silaha zake za kampeni kutimiza ndoto zake za muda mrefu.
Orengo na Oburu wanasema Wakenya hawajaona mwisho wa Raila huku wakipuuza na kukejeli wale wanaosema Raila hana budi kustaafu na kuelekea katika shamba lake lililoko eneo la Bondo.
“Ningependa kuwashauri wale wanaompuuza Raila kwamba wasithubutu kumrusha mbali ya jukwaa la siasa za Ikulu. Raila ni mwanasiasa mkakamavu na mwenye nguvu na pia mwenye uzingativu wa hali ya juu, Oburu akasema wiki jana.
Wiki jana pia Orengo aliwakumbusha Wakenya kwamba, Raila ambaye sasa ana umri wa miaka 73, na ambaye amewania urais mara nnne bila mafanikio, ni mwaniaji bora zaidi wa upinzani katika uchaguzi mkuu ujao.
Lakini kupitia kwa msemaji wake rasmi, Dennis Onyango, Raila alisema matamshi ya Orengo ni yake binafsi na hayaambatani na fikra za kiongozi huyo wa ODM.
“Raila ana shughuli nyingi za kujenga madaraja ya utangamano na ushirikiano miongoni mwa Wakenya na kwa hivyo hana nafasi ya kufanya siasa,” Onyango akasema.
Taarifa hii kutoka ofisi ya Raila ilizua mijadala kwamba pengine Raila huenda anapanga kustaafu.
Punde tu baada ya taarifa hiyo, manaibu wa chama cha ODM kama vile Gavana wa Jimbo la Mombasa Hassan Joho na mwenzake wa Jimbo la Kakamega, Wycliffe Oparanya , walitangaza maazimio yao ya kuwania urais 2022. Walisema wao ni viongozi bora zaidi kuwania kiti hicho kikuu.
Joho alimtembelea Rais Mstaafu, Daniel arap Moi Agosti 25 pengine katika pilikapilika za kutafuta uungwaji mkono kutoka kwa kiongozi huyo wa zamani.
Lakini mwanaye Rais Moi, Gideon pia anapania kuwania urais. Joho na Seneta huyo wa Jimbo la Baringo huenda wanapanga kushirikiana 2022 na kugawa mamlaka. Gideon, Mzee Moi na Joho walifanya mkutano wa faragha uliochukua saa moja.
Ingawa haikujulikana watatu hao walijadili nini, mkutano huo umefanyika wakati Gideon na washiriki wake wamekuwa wakitembelea Pwani ya Kenya haswa majimbo ya Kwale na Mombasa. Umuhimu wa safari hizo za Pwani katika ulingo wa siasa za kimataifa haujafichika. Katika utawala wake Mzee Moi alikuwa na washiriki na wafuasi wa kisiasa katika eneo la Pwani.
Mkutano huo kati ya Moi, Gideon na Joho, wadadisi wa siasa wanasema huenda unatafuta ushirikiano wa Joho ambaye ni mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa katika eneo la Pwani.
Ikiwa Gideon anapania kuwania uongozi 2022 na pia Raila akiwa papo hapo, wanasiasa hao bila shaka wanatafuta umoja kwani siasa za siku hizi zinahitaji ushirikiano mpana. Joho anasema mkutano huo unalenga kuongeza nguvu juhudi za Rais na Raila kujenga madaraja miongoni mwa Wakenya kutoka tabaka na jamii mbalimbali.
Matamshi ya Orengo na Oburu yanaweza kuzua mikinzano katika ODM na kudidimiza matumaini ya magavana kumrithi Raila. Joho na Oparanya wameashiria kubuni vyama vya kanda vitakavyowaweka mamlakani kitaifa.
Wiki jana, Oparanya alinukuliwa akisema yuko tayari kuhama ODM ikiwa viongozi wa magharibi mwa Kenya anapotoka yeye wataungana na kuunda chama cha eneo hilo.
Vitendo vya magavana hao wawili yaonyesha kwa kuwa hakuna uhakika wa Raila kuwania urais kama inavyosemwa, hali hii inawachanganya wale waliokuwa wanapanga foleni kumrithi.
Ingawa hajaongea kuhusu mipango yake ya 2022, wapinzani wake haswa wale wanaounga mkono Ruto wanasema Raila atawania urais 2022. Washiriki wa Ruto wamemtuhumu Raila kwa kutumia ushirikiano wake na Rais Uhuru waliosaini Machi 9 kujiuza kama mwaniaji wa urais 2022.
Kabla ya mkataba wa Rais Uhuru na Raila, Ruto alikuwa katika mstari wa mbele kama mgombea wa urais kwa sababu yuko karibu na kiti hicho kinachomezewa mate na wengi.
Wanaompigia Ruto debe wanadai salamu kati ya Uhuru na Raila zimechanganya na kuvuruga hesabu zao huku Raila akikamua kabisa faida ya uhusiano wake na kiongozi wa nchi kwa kutafuta ufuasi katika ngome za Jubilee.
Seneta wa Jimbo la Nandi, Samson Cherargei ambaye ni mfuasi sugu wa Ruto anaamini Raila atapambana na Ruto 2022.
“Hakuna mshangao. Sisi tulijua atawania urais na tuko tayari kumkabili. Tunajua pia kwamba Raila anatumia salamu zake na Uhuru kutafuta ufuasi na uungwaji mkono katika maeneo ambayo Jubilee ina ufuasi mwingi,” Cherargei akasema.
Mtaalamu mmoja wa masuala ya kisiasa, Dk Tom Mboya aliliambia gazeti moja la kila siku kwamba, ijapokuwa Raila hajafanikiwa kushinda urais tangu awanie kiti hicho 1997, ana ufuasi mwingi nchini kote kuliko mwanasiasa mwingine yeyote.
Wale wanaofikiria Raila atakuwa anawashangilia wawaniaji wa urais 2022, wanajidanganya. Raila yuko katika kinyang’anyiro.

Comments