Skip to main content

Featured

Maombolezo: Hii ndiyo Hali Ilivyo Tanzania Bendera Yapepea Nusu Mringoti

Agizo la Rais John Magufuli la Bendera ya Taifa kupepea kwa nusu mlingoti kwa siku tatu kuanzia leo Septemba 22 kufuatia ajali ya kivuko cha MV Nyerere iliyotokea mkoani Mwanza limetekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Serikali yasema chaguzi ndogo haziathiri idadi ya wabunge viti maalum

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Anthony Mavunde
Dodoma.  Serikali imesema chaguzi ndogo zinazofanyika nchini haziwezi kuathiri idadi ya wabunge wa Viti Maalum wa vyama mbalimbali vya siasa.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne Septemba 4, 2018 na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Anthony Mavunde wakati akijibu swali la mbunge wa Viti Maalum (CCM), Angelina Malembeka.
Katika swali lake Malembeka amesema baadhi ya wabunge wa majimbo walihama vyama vyao na kujiunga na vyama vingine na kufanyika uchaguzi wa marudio na CCM kuibuka kidedea.
“Je ni nini hatima ya wabunge wa viti maalum walioingia bungeni kupitia asilimia za majimbo ya uchaguzi,” amehoji huku akitaka kujua idadi zaidi ya wabunge wa viti maalum kwa tiketi ya CCM, kwa kuwa chama hicho kimeongeza idadi ya wabunge.
Katika majibu yake Mavunde amesema ibara ya 78(1) ya Katiba ya mwaka 1977 imeainisha bayana kuwa vyama vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi mkuu na kupata angalau asilimia tano ya kura zote halali za wabunge vitapendekeza kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi  (NEC) majina ya wabunge wa Viti Maalum.
Amesema majina yatakayopendekezwa yanatakiwa kuzingatia uwiano wa kura ambazo kila chama kimepata wakati wa uchaguzi wa wabunge ili NEC iweze kuteua miongoni mwao wabunge hao wa viti maalum.
“Kwa msingi wa sheria hii idadi ya wabunge wa viti maalum  kwa kila chama inapatikana wakati wa uchaguzi mkuu ambao hufanyika kila baada ya miaka mitano,”amesema.
Amesema mabadiliko yoyote yanayotokea wakati wa uchaguzi mdogo hayaathiri idadi ya viti maalum vya chama husika.
Hata hivyo, amesema Serikali imeendelea kupokea maoni na ushauri kuhusu jambo hilo na kwamba kutokana na hali ilivyo kwa sasa Katiba na sheria za nchi vitaendelea kuwa msingi mkuu wa ufafanuzi na mgawanyo wa wabunge wa Viti Maalum bungeni.

Comments

Popular Posts