Tumepokea kwa masikitiko taarifa za kuzama kwa kivuko cha Mv Nyerere kulikosababisha maisha ya watu wengi wilayani Ukerewe kupoteza maisha.
Kivuko hicho kilichokuwa kinatoka eneo la Bugolora, Ukerewe kwenda Kisiwa cha Ukara katika Ziwa Victoria kilizama juzi saa 8:05 mchana na hadi jana Ijumaa mchana miili ya watu zaidi ya 100 ilikuwa imeopolewa. Watu 32 waliokolewa wakiwa hai.
Taarifa za awali zilieleza kuwa kivuko hicho chenye uwezo wa kubeba abiria 94, tani 25 za mizigo na magari madogo matatu kilizidisha mizigo na pia kilibeba lori la mahindi.
Tunatoa pole kwa wafiwa na kuwaombea pumziko la milele waliofariki dunia katika ajali hiyo. Pia tunawatakia majeruhi wapate uponyaji wa haraka.
Pamoja na salamu hizo, tungependa kukumbusha masuala muhimu ya kiusalama katika vyombo vya usafiri majini ambavyo vimeendelea kupata ajali za mara kwa mara zinazoua idadi kubwa ya watu.
Ajali hii imetokea wakati Watanzania hawajasahau ajali nyingine kubwa za majini, hasa ya meli ya Mv Bukoba iliyozama katika Ziwa Victoria na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 800. Ajali nyingine ni meli ya Mv Skagit na Mv Spice Islander zilizozama Bahari ya Hindi.
Vilevile, zimekuwapo ajali nyingine za vivuko na mitumbwi mbalimbali katika maeneo tofauti nchini, nyingi zikitokea Ziwa Victoria.
Tunatambua kwamba hizo zote ni ajali na kwamba upo usemi wa Kiswahili kuwa “ajali haina kinga”, lakini hatukubaliana kwamba kila ajali haina kinga.
Laiti kama tungejifunza ushauri uliotolewa na Tume ya Jaji Robert Kisanga iliyochunguza ajali ya Mv Bukoba mwaka 1996, huenda haya mengine yasingetokea kwa kiwango cha ajali ya Mv Nyerere.
Tume hiyo iliyopokea maoni na ushauri wa wataalamu kutoka sehemu mbalimbali duniani, ilishauri pamoja na mambo mengine kwamba suala la uwezo wa vyombo vya majini na hata angani lizingatiwe na kushauri vyombo hivyo vibebe uzito unaostahili au pungufu yake wakati wote.
Ni ajabu kwamba miaka 22 baadaye tatizo la kuzidisha uzito kwenye kivuko, tena cha Serikali, bado linaendelea. Imeelezwa kuwa Mv Nyerere ilizidisha abiria na mizigo.
Walishauri pia usalama wa vyombo vyenyewe uangaliwe kila mara na kufanyiwa matengenezo ili viwe salama wakati wote. Na hapa kuna maneno na zimesambazwa video za mbunge wa Ukerewe akilalamikia hali ya kivuko hiki bungeni na kuonya kwamba kinaweza kusababisha maafa.
Tume ya Jaji Kisanga pia ilishauri kiundwe kikosi maalumu cha uokoaji katika Ziwa Victoria, ambalo ni la pili kwa ukubwa duniani, ili kuacha tabia ya kufanya kazi kwa mazoea ziwani humo. Hadi sasa hatujasikia kama kikosi hicho kimeundwa
Si hayo tu, tume hiyo ilishauri vyombo vyote vya usafiri viwe na orodha ya wasafiri ili inapotokea tatizo iwe rahisi kujua ni akina nani walikuwamo, lakini hatuna uhakika kama orodha hiyo kwa abiria waliopanda Mv Nyerere ipo na huenda ndiyo maana tunasikia idadi tofauti; wapo wanaosema walipanda watu 100, wengine wanadai ni 400. Limebaki suala la kubahatisha kujua idadi halisi ya watu waliokuwemo kwenye kivuko hicho.
Kwa kuwa masuala yaliyoshauriwa Tume ya Jaji Kisanga yanaonekana hayajafanyiwa kazi kikamilifu, tunashawishika kuamini kwamba hatukujifunza lolote kutokana na ajali hiyo na kazi iliyofanywa kujaribu kupata suluhisho la ajali za majini.
Ni muhimu basi kwa wahusika wote kuchukulia ajali ya Mv Nyerere kuwa ilani ya kuwakumbusha kufanyia kazi masuala yote ya usalama katika usafiri wa majini.
Comments
Post a Comment