Dar/Zanzibar. Kuzama kwa kivuko cha Mv Nyerere na tahadhari iliyokwishatolewa na Mbunge wa Ukerewe (Chadema), Joseph Mkundi imewaibua viongozi wa kisiasa wakitaka hatua zichukuliwe kwa waliosababisha kutokea ajali hiyo.
Katika moja ya michango yake ndani ya Bunge, Mkundi alizungumzia kivuko hicho akitaka Serikali kuchukua hatua za haraka kukifanyia matengenezo kwani kinahudumia watu wengi, lakini ni kibovu.
“Naomba kupata kauli ya Serikali, ni suala ambalo tumekuwa tunalishughulikia mara kwa mara, tuna kivuko kinachounganisha Ukerewe na Kisiwa cha Ukara, kivuko hiki kinahudumia watu zaidi ya 50,000,” alisema Mkundi bungeni.
“Kimekuwa kinaleta shida mara kwa mara na nimekuwa nawasiliana na wizara, sipendi siku moja tuje hapa kuomba rambirambi kwa sababu ya wananchi waliozama katika kivuko kile.”
Hata hivyo, Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa), Hassan Karonda aliliambia Mwananchi kuwa kivuko hicho kilifungwa injini mpya Julai mwaka huu, baada ya awali kupata hitilafu na kimekuwa kikitoa huduma kutoka Kisiwa cha Bugolora–Ukara wilayani Ukerewe tangu mwaka 2004.
Licha ya ufafanuzi huo wa Temesa, wanasiasa na watu wengine walikuwa na maoni tofauti pamoja na kutoa salamu za rambirambi.
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, licha ya kutoa salamu za rambirambi, walitaka hatua zichukuliwe kwa wote waliohusika kuzama kwa kivuko hicho.
Katika salamu za Maalim Seif jana kwenda kwa Rais John Magufuli, alisema alisikitishwa na uamuzi wa kusitishwa kwa shughuli ya uokoaji juzi jioni.
Alisema, “nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kuzama kwa kivuko cha Mv Nyerere (juzi) jana jioni, nampa pole zangu za dhati Rais John Magufuli, huu ni msiba wetu sote kama Taifa.”
“Pia nawapa pole ndugu, jamaa na wapendwa wote waliopoteza ndugu zao katika ajali hii, Mwenyezi Mungu awape subira katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo ya kuondokewa na wapendwa wao.”
Kuhusu uokoaji, Maalim Seif alieleza kusikitishwa na kusuasua kwake, hasa kitendo cha kusitishwa kwa muda juzi usiku, ikielezwa ni kwa sababu ya kukosekana kwa taa na injini za boti.
“CUF inawataka viongozi wote wanaohusika na kadhia hii wakiwemo mawaziri wa wizara husika kuwajibika kwa kujiuzulu nafasi zao au kuwajibishwa na mamlaka za uteuzi wao kwa kutochukua tahadhari ya mapema,” alisema Maalim.
Mbowe, ambaye ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya Chadema, Kinondoni jijini Dar es Salaam jana, alisema kuzama kwa kivuko hicho ni uzembe.
Alimtaka Rais Magufuli achukue hatua kwa watendaji wake.
Alisema safari kutoka Kisiwa vya Bugolora hadi Ukara ni ya dakika 45 na kivuko kina uwezo wa kubeba abiria 101, lakini inasemekana kilibeba abiria zaidi na mizigo.
Alisema kumekuwapo na marudio ya matukio ya ajali za namna hiyo na Taifa hadi sasa halina mbinu za kujikinga wala kuokoa.
Mbunge huyo wa Hai alisema boti ilizama mapema saa 8 mchana na hadi inafika saa 12:00 jioni hakuna utaratibu uliofanyika wa kuandaa vifaa vya uokoaji.
“Hatuna vifaa vya kisasa vya uokoaji kwenye maziwa makubwa Nyasa na Victoria, waliokuwa wanajaribu kuokoa ni wavuvi ambao hawana oksijeni wala vifaa vya kisasa vya uokoaji,” alisema Mbowe.
Katika mkutano huo, Mbowe aliitaka Serikali ijiandae kulipa fidia kwa familia zilizopoteza watu na mali. “Kuna taarifa kuwa kulikuwa na maboya machache watu walikuwa wananyang’anyana na yaliyokuwapo yalikuwa kwenye chumba kilichofungwa,” alidai Mbowe.
Alisema wao kama chama, wanasubiri kwa unyenyekevu mkubwa kuungana na Taifa kuomboleza kadri wenye dhamana watakavyotoa maelekezo.
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa alitoa salamu za rambirambi na kubainisha kuwa msiba huo ni wa Taifa.
“Nimepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za ajali ya kuzama kwa kivuko cha Mv Nyerere,” alisema Lowassa.
“Ninawapa pole ndugu wote waliopoteza maisha, mkuu wa Mkoa wa Mwanza na Watanzania wote kwa ujumla.”
Alisema huu ni msiba wa nchi nzima na aliitaka Serikali kujipanga ili ajali kama hiyo isitokee tena. “Ni lazima tujiulize na kujipanga ili haya yasitokee tena.”
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema kuzama kwa kivuko hicho ni ajali ya kujitakia.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika ofisi za makao makuu ya chama hicho, jijini Dar es Salaam jana, alisema zaidi ya asilimia 96 ya majanga yanasababishwa na wanadamu, asilimia nne tu ndiyo ya asilia.
Akizungumzia kiundani kuhusu majanga, alisema kuna aina tatu za majanga na kwamba kuzama kwa meli hiyo ni janga lililokuwa likijulikana na wahusika walijua.
Mbatia ambaye ni mtaalamu wa majanga alisema Taifa linapopata janga moja kubwa, hutoa elimu ya kujikinga ili janga kama hilo lisijitokeze tena.
Alisema, “ukiacha ajali hii ya kivuko, meli za Mv Spice Islanders na Mv Bukoba ambazo zote zilizama zilikuwa elimu tosha na hizi ajali za meli kuzama hazikupaswa kutokea tena.”
“Ukikusanya ajali hizi ukiwa na takwimu sahihi za kutosha na rejea ya majanga, unaweza kujua jinsi ya kuokoa raia, kulinda raia ili yasitokee tena majanga badala ya kulalamika na kunyoosheana vidole, kushikana mashati.”
Mbatia ambaye ni mbunge wa Vunjo, alisema ajali za aina hiyo zinapotokea, wengi huishia kutoa pole jambo ambalo halisaidii.
Alisema iwapo mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Jaji Robert Kisanga baada ya kutokea kwa ajali ya Mv Bukoba mwaka 1996 yangefanyiwa kazi, ufumbuzi wa nini kifanyike inapotokea ajali ya aina hiyo ungekwishapatikana.
Mbatia alishauri kuanzishwa kwa sheria ya wakala wa usimamizi wa maafa kwa lengo la kuwalinda na kuwakinga wananchi.
“Kupanga ni kuchagua, kama walikuwepo wa Chadema walikufa, wa CUF walikufa wa NCCR walikufa, kitengo hicho licha ya kupigiwa kelele hakikuundwa na wanaozungumza ni polisi, mkuu wa mkoa siyo watu maalumu wa maafa wenye elimu ya masuala hayo.
“Mara nyingi ninazungumza bungeni kuikumbusha Serikali wajibu wake namba moja wa kulinda raia. Siasa na kubezana kunapoteza maana,” alisema kiongozi huyo.
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) jana ilitoa salamu za rambirambi kwa ndugu, jamaa, marafiki na wananchi wote walioguswa na ajali hiyo, huku ikiahirisha kikao chake cha Baraza la Wawakilishi jioni ili kuungana na waombolezaji.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mohamed Aboud Mohamed akitoa taarifa ya Serikali ndani ya baraza hilo alisema wamepokea kwa masikitiko taarifa za ajali ya kivuko hicho.
Alisema SMZ na watu wake wote wanaungana na ndugu wa Tanzania Bara katika kipindi hiki kigumu kutokana na ajali hiyo.
“Kwa niaba ya Serikali, tuwatake wale wote walioguswa na ajali hiyo wawe wapole na wastahamilivu katika kipindi hiki kigumu,” alisema.
Wakati huohuo, Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi, Mwanasha Khamis akitoa taarifa za baraza hilo kwa niaba ya Spika alisema msiba huo si wa wana Mwanza pekee, bali ni Watanzania wote.
“Kwa niaba ya Spika napenda kuchukua nafasi hii kutamka kuwa kikao chetu kilichopangwa kufanyika jioni ya leo (jana), kimeahirishwa lengo ni kuungana na wenzetu kuomboleza msiba uliolipata Taifa,” alisema.
Comments
Post a Comment